http://www.swahilihub.com/image/view/-/3042756/medRes/1233939/-/6u6sbe/-/DNDIGITAL1512j.jpg

 

Maamuzi ya kiholela hayaleti suluhisho

Fred Matiang'i

Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang'i ahutubu wakati wa kuzindua upakiaji wa matini ya kidijitali kwa wanafunzi wa darasa la kwanza katika Taasisi ya Kukuza na Mtaala (KICD). Picha/GERALD ANDERSON 

Na MHARIRI

Imepakiwa - Monday, January 1  2018 at  21:18

Kwa Mukhtasari

JUMANNE shule zinapofunguliwa na watu wanaporejea kazini baada ya mapumziko marefu ya Mwaka Mpya, kuna wasiwasi huenda baadhi ya shughuli zikatatizwa.

 

Waziri wa Elimu, Dkt Fred Matiang’i alipotangaza shule zifunguliwe Januari 2, ni kama alichukua uamuzi huo bila kuzingatia uhalisia wa mambo.

Ni wazi kuwa miongoni mwa Wakenya, mwisho wa mwaka ni muda wa kutembelea wazazi na kuwapelekea wajukuu wao mashambani.

Familia nyingi hupenda kuadhimisha Krismasi na Mwaka Mpya wakiwa na jamaa zao kwao mashambani. Ndio sababu hata sasa hivi, jiji la Nairobi halina msongamano wake wa kawaida.

Watu wanapoenda makwao, hutumia siku ya Mwak Mpya kusafiri usiku na kufika katika miji wanakoishi au kufanya kazi Januari 2. Kwa hivyo, kuwataka walimu siku hiyowaitumie kuchapa kazi madarasani ni kutozingatia uhalisia wa mambo.
Inaonekana wazi kuwa waziri na maafisa wenzake katika wizara walichukua hatua ya kutangaza siku hiyo bila ya kufikiria athari zake kwa wahusika.

Kisha wizara hiyo hiyo ikaunga mkono tangazo la Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kwamba walimu wakuu wa shule wahamishwe kutoka shule zao na kwenda katika shule nyingine, nje ya kaunti zao.

Agizo hilo halijapokewa vyema na vyama vya walimu (KNUT) na Kuppet kwa msingi kuwa lilifanywa tu kando ya barabara bila ya kuwahusisha wadau.

Na sasa kuna tangazo la Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama wa Barabarani (NTSA) kupiga marufuku safari za usiku kwa magari ya uchukuzi wa umma pekee.

Huenda nia ya kuchukua hatua hiyo ni njema, lakini ni uamuzi uliochukuliwa bila ya kuzingatia athari zake. Kwanza NTSA yapaswa kujua kuwa ajali nyingi zilihusisha matatu au mabasi kugongana na matrela. Ni kwa nini marufuku yalitangazwa dhidi ya magari ya kubeba abiria pekee.

Ina maana watakaokufa kwenye malori hawana thamani? Kama nia ni kuzuia vifo vya kiholela barabarani, basi malori pia yafaa kuzuiwa kusafiri usiku kwa sababu sasa yatakuwa yakiwagonga waendeshao magari ya kibinafsi.

Kutokana na marufuku ya safari za usiku, maelfu ya watoto walilazimika kulala njiani na wengi watakosa kufika kazini.

Wakati mwingine serikali ipime mambo badala ya kutangaza kiholela.