Maana ya maendeleo endelevu

Imepakiwa - Thursday, May 16  2019 at  11:01

 

Wachambuzi na waandishi kadhaa wanatafsiri maendeleo endelevu kuwa yale yanayowezesha wananchi kupata mahitaji yao bila kuathiri kizazi cha baadaye.

Kwamba mahitaji ya sasa yapatikane bila kuzuia upatikanaji wa mahitaji ya kizazi kijacho. Mjadala wa maendeleo una tafsiri pana.

Uamuzi juu ya matumizi sahihi ya rasilimali za dunia yanapaswa kufanyika si tu kisayansi bali kimaadili na kiuchumi. Maendeleo endelevu yana tafsiri ya kuweka kwenye mizania maeneo ya jamii, mazingira na uchumi.

Mradi endelevu wowote unatajwa kuzingatia mambo makuu matano yajulikanayo kama P5 zitumikazo zaidi ni P3. P hizi husimama badala ya jamii (people), mazingira (planet) na uchumi (profit).

Moja ya sifa za mradi endelevu ni kubainisha uzalishaji na matumizi ya bidhaa au huduma tarajiwa baada ya mradi kukamilika. Unapaswa kubainisha urafiki wa mradi na mazingira, jamii na uchumi katika kipindi chote cha uwepo wake.

Kwa tafsiri ya kawaida hii ina maana kuwa mradi wowote kabla ya kuanza utekelezaji, kwenye hatua zake za awali ya utambuzi unapaswa kueleza wazi manufaa yatakayopatikana kwa jamii, athari za mazingira na kiuchumi pia.

Mradi unaweza ukawa na manufaa kwa jamii na kiuchumi, lakini wakati huohuo ukawa na madhara kwa mazingira. Unaweza ukawa na manufaa ya kiuchumi lakini ukawa na madhara kwa jamii na mazingira kwa wakati huo pia.

Kabla ya kuwekeza fedha na rasilimali nyinginezo muhimu kuufanikisha mradi wowote tunapaswa kuhakikisha unazingatia maslahi mapana ya jamii, mazingira na uchumi.

Uibuaji na utekelezaji wa miradi unategemea kiwango cha madhara ya utekelezaji katika maeneo makuu matatu ambayo ni jamii, mazingira na uchumi. Wataalamu wa usimamizi wa miradi wanashauri wakati wote kutekeleza miradi ambayo itaweka mizania sawa katika jamii, uchumi na mazingira.

Zipo namna mbili za kuibua miradi katika jamii, namna ya kwanza ni miradi inayoanzia chini kuelekea juu kwa ajili ya maamuzi na utekelezaji (bottom – up) na aina ya pili ni ile inayoanzia juu kwenda chini kwa ajili ya utekelezaji (top – down). Kila aina ina faida na hasara zinazotofautiana kwa viwango.

Miradi inayoanzia chini kwenda juu inatajwa kuwa endelevu zaidi kwa sababu mara nyingi hubuniwa na wananchi kutokana na fursa na vikwazo walivyonavyo katika maeneo yao.

Miradi ya aina hii inatajwa kuwa endelevu na yenye matokeo chanya kwa wananchi zaidi kuliko aina ya pili hivyo kila inapowezekana ni vyema kuipa kipaumbele kwani manufaa yake huwa makubwa zaidi kwa wanufaika.

Ipo mifano mingi katika kundi hili. Baadhi ya miradi ya maji iliyotekelezwa na wizara, wahisani na wadau wengine bila kusikiliza na kufuata ushauri wa wananchi ilikufa baada ya muda mfupi tangu ikamilike.

Miradi inayoanzia juu kwenda chini ni ile ambayo haitokani na mawazo ya wananchi wa eneo husika. Aina hii mara nyingi inatokana na mawazo ya Serikali kwenda kwa wananchi.

Ujenzi wa madaraja ya juu kwenye makutano ya Tazara na Ubungo jijini Dar es Salaam ni mfano wa miradi hiyo. Hata kuhamishia makao makuu ya Serikali jijini Dodoma ni uamuzi unaoingia kwenye kundi hili.

Kwa wastani miradi ya aina hii huwa ya kimkakati zaidi kwa maendeleo mapana ya wananchi wote. Wataalamu wa wizara au taasisi za Serikali hubuni na kutekeleza miradi ambayo inatajwa kuwa na manufaa mapana kwa wananchi wa eneo husika na Taifa kwa jumla.

Wananchi wanapaswa kuwa wamiliki, waendeshaji na wasimamizi wa miradi katika maeneo yao. Kila mradi hubuniwa au kuanzishwa kwa lengo la kutatua aina fulani ya changamoto katika jamii husika.

Hivyo, kwa vyovyote vile, kila mradi unapaswa kuanzishwa kwa manufaa mapana ya wananchi kwa kuzingatia umuhimu wa kulinda mazingira na faida za kiuchumi au huduma.

Katika usimamizi wa miradi, ile endelevu ina sifa kadhaa ikiwamo kuwa na matokeo ya muda mrefu na mfupi. Aidha, kuwa na maslahi ya kizazi cha sasa na baadaye na kuwa endelevu kwa mzunguko wa maisha. Pia hujali jamii, mazingira na uchumi au huduma.

Miradi endelevu ni tofauti na miradi ya kawaida ambayo hujikita zaidi kuzingatia muda, mawanda na bajeti. Miradi endelevu inaenda zaidi ya muda na bajeti.

Mwandishi ni mtakwimu na mtumishi wa ofisi ya Rais Tamisemi. Anapatikana kwa namba 0685 214 949.