http://www.swahilihub.com/image/view/-/4927122/medRes/1506903/-/gi7fw1/-/kairuki.jpg

 

Mabadiliko ya Kairuki, Biteko yawakuna wadau

Angellah Kairuki, mteule, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) 

Na Waandishi Wetu

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  09:30

Kwa Muhtasari

Wateule wote wataapishwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam.

 

mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar/ Arusha. Wakati Rais John Magufuli akimhamisha Angellah Kairuki kutoka Wizara ya Nishati kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), baadhi ya wadau wamesema mabadiliko hayo yatachochea utendaji.

Kabla ya kuteuliwa kwenye wizara hiyo mpya, Kairuki aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala), baadaye alihamishiwa Wizara ya Madini wakati Rais Magufuli alipoigawa na ile ya Nishati.

Kuondolewa kwa Kairuki katika nafasi hiyo kumekuja mwaka mmoja kamili tangu Rais Magufuli alipozinyooshea kidole wizara za Kilimo na Madini akisema hafurahishwi na utendaji wao.

Rais Magufuli alieleza hayo Januari 8 mwaka jana alipomteua Dotto Biteko kuwa naibu waziri wa Madini akisema, “Labda ataenda kuamsha waliolala katika hiyo.

“Wizara ya madini ina changamoto nyingi na niseme, tu ukiachia mambo machache wizara ya madini haifanyi kazi vizuri na nikizungumza kwa kupamba nitakuwa mnafiki,” alisema Rais.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema jana kwamba katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri ambayo Rais ameyafanya jana, Kairuki atayeshughulikia uwekezaji kwa lengo kuongeza msukumo wa kuimarisha masuala ya sekta hiyo hasa baada ya kuamua Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kiwe chini Ofisi ya Waziri Mkuu na nafasi yake kuchukuliwa na Biteko.

Walipotakiwa kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko hayo, baadhi ya wadau walisema wawekezaji wamepata mtetezi atakayeshughulikia kero zao kikamilifu.

“Mwanzoni TIC ilivyokuwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kulikuwa na ugumu kwa baadhi ya mawaziri kuambizana kuhusu kutatua changamoto fulani inayohusu wawekezaji,” alisema Frank Dafa ambaye ni ofisa wa sera na masuala ya biashara wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte aliungana na Dafa akisema ni jambo zuri kuwapo kwa wizara hiyo kwani changamoto zinazowakabili wa wawekezaji zitatatuliwa kwa wakati.

“Wizara hii itakuwa mwarobaini wa changamoto za uwekezaji na itasababisha mazingira mazuri kwa watu wa sekta hii. Tunamkaribisha mama Kairuki na tutamtafuta haraka iwezekanavyo kwa lengo la kufanya majadiliano ya sekta hii,” alisema Shamte.

Wachimbaji na wanunuzi wa madini ya Tanzanite Mirerani, wamepongeza uteuzi wa Biteko na uhamisho wa Kairuki wakisema sasa sekta za madini na uwekezaji zinakwenda kukua zaidi.

Mkurugenzi wa Tanzanite One, Faisal Shabhai alisema uteuzi huo unalenga kukuza sekta ya madini na kwamba, “Waziri Biteko anaijua sekta ya madini kwani amekuwa katika kamati ya madini na ni mtendaji mzuri sisi kama wadau tuna imani naye.”

Shabhai alisema hata uteuzi wa Kairuki utasaidia Taifa kwani anajua sekta muhimu ambazo zinahitaji uwekezaji kama nishati na madini.

“Uamuzi wa Rais mzuri na tunaamini utasaidia kuongeza mapato ya Serikali,” alisema.

Walioteuliwa

Mbali ya mawaziri hao, Balozi John Kijazi alisema Rais Magufuli amembakiza Stanslaus Nyongo katika nafasi yake ya naibu waziri wa Madini.

“Kwa kuwa wizara hii ilikuwa na manaibu waziri wawili, sasa itabaki na naibu waziri mmoja ambaye ni Nyongo,” alisema Balozi Kijazi.

Alisema kutokana na baadhi ya makatibu wakuu kustaafu na ili kuimarisha utendaji, Rais Magufuli amemteua Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi) akichukua nafasi ya Mussa Iyombe aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Nafasi ya Nyamuhanga ambaye alikuwa katibu mkuu Ujenzi imejazwa na mtendaji mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Elius Mwakalinga.

Pia, Dk Zainab Chaula ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Afya, akichukua nafasi ya Dk Mpoki Ulisubsya aliyeteuliwa kuwa balozi ambaye kituo chake cha kazi kitatangazwa baadaye.

“Kabla ya uteuzi huu Dk Chaula alikuwa naibu katibu mkuu Tamisemi (Afya). Nafasi ya Dk Chaula imechukuliwa na Dk Dorothy Gwajima ambaye ni mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya,” alisema Balozi Kijazi.

Dorothy Mwaluko aliyekuwa naibu katibu mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) anakuwa katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) akichukua nafasi ya Profesa Faustine Kamuzora aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera akienda kujaza nafasi ya Athuman Diwani aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Nafasi ya Dk Mwaluko imechukuliwa na Dk Francis Michael ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” alisema.

Wateule wote wataapishwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam.