http://www.swahilihub.com/image/view/-/4554088/medRes/1968093/-/ko9xyuz/-/uwaja.jpg

 

Kamati ichunguze kwa makini deni la Machinga Complex

Machinga Complex

Serikali ya Tanzania imeunda kamati kushughulikia sintofahamu iliyopo iliyopandisha deni la Machinga Complex kutoka mkopo wa Tsh12.4 bilioni za ujenzi wa jengo hilo la wafanyabiashara ndogondogo, zilizotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kufikia Tsh57 bilioni. Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, May 10  2018 at  10:15

Kwa Muhtasari

Serikali ya Tanzania imeunda kamati kushughulikia sintofahamu iliyopo iliyopandisha deni la Machinga Complex kutoka mkopo wa Tsh12.4 bilioni za ujenzi wa jengo hilo la wafanyabiashara ndogondogo, zilizotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kufikia Tsh57 bilioni.

 

KWA mara nyingine gazeti la Mwananchi lilichapisha habari kuhusu deni la Machinga Complex kuzidi kuongezeka na sasa kufikia Tsh57 bilioni.

Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo imetokana na kauli ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Serikali imeunda kamati kushughulikia sintofahamu iliyopo iliyopandisha deni hilo kutoka mkopo wa Tsh12.4 bilioni za ujenzi wa jengo hilo la wafanyabiashara ndogondogo, zilizotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Meya anasema kamati hiyo ambayo itakuwa na wajumbe wa jiji na wa NSSF, ikimaliza kazi itawasilisha taarifa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Bw Selemani Jafo.

Suala hilo limekuwa likijirudiarudia mara kwa mara lakini hakuna suluhisho la maana linalotolewa, ila riba ya mkopo huo inazidi kuongezeka.

Hali hiyo iliziweka fedha za wastaafu zilizowekezwa katika kitega uchumi kisicho na faida kuwa hatarini kupotea bila maelezo ya msingi.

Tunadhani kamati hii iliyoundwa sasa iwe ya mwisho, ije na mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na hatimaye suala hilo limalizwe kwa makubaliano ambayo hayataleta hasara kwa upande wowote na hasa kulinda fedha za wafanyakazi waliotumia jasho lao kulitumikia Taifa hadi kustaafu.

Tunasema hayo tukitambua kuwa mapendekezo ya kamati hiyo hayatakuwa ya kwanza, kwa kuwa inafahamika kuwa hatua mbalimbali ziliwahi kuchukuliwa kuhusu deni hilo na sababu za jengo husika kushindwa kuzalisha fedha zilizokusudiwa.

Hata wakuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa sasa) na aliyepita, Saidi Mecky Sadiki wamewahi kuchukua hatua mbalimbali kuhusu jengo hilo bila mafanikio.

Hivyo, tunaamini kuwa kamati iliyoundwa sasa itazingatia madai ya pande zote husika na kwenda mbali zaidi katika kusaka suluhisho lenye masilahi ya pande zote na yale ya Taifa kwa kupima taarifa za awali zilizoangalia suala hilo kwa mapana yake.

Mathalan, katika mapendekezo ya tathmini ya Makonda, alipendekeza kuvunjwa kwa mkataba huo na NSSF kuchukua eneo lao, kwa makubaliano ya kwamba, halmashauri ya jiji walipwe kodi ya ardhi, jambo ambalo linaweza kufanyika kwa urahisi kupitia NSSF na halmashauri ya jiji kumiliki hisa kwa pamoja; au NSSF wakabidhi jengo kwa halmashauri ya jiji, lakini wakae na kukubaliana upya na hivyo kuandika mkataba tofauti na ule wa mwanzo.

Kulingana na tathmini hiyo, Makonda alibainisha kuwa deni hilo halilipiki kwa kuwa kiasi cha pesa kinachodaiwa kutoka kwa halmashauri ya jiji haiwezi kukilipa na kuwa mkataba baina ya pande hizo ni wa ovyo na haukupaswa kusainiwa.

Mbali na hayo, vilevile kamati hiyo ichunguze hata uhalali wa ongezeko la riba.Kwa mfano Mwita anasema deni hilo limeongezeka hadi Tsh57 bilioni mwaka 2018 kutoka Tsh42 bilioni za mwaka 2017, sawa na ongezeko la Tsh15 bilioni kwa mwaka mmoja.

Pamoja na ukweli kuwa jengo hilo lipo sehemu ambayo mzunguko wa biashara ni mdogo unaosababisha wafanyabiashara kutopata faida, ukubwa wa ongezeko la riba kwa mwaka mmoja unaozidi hata gharama za awali za ujenzi, ni jambo linalohitaji kuthibitishwa.

Ni imani yetu kwamba kamati hii itafanya haya yote kwa weledi na haraka na suluhisho litapatikana.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647