http://www.swahilihub.com/image/view/-/4655466/medRes/2039380/-/yoxipb/-/trafk.png

 

Madereva wanaotoa rushwa kwa matrafki 'watakiona cha moto'

Askari wa usalama barabarani akichukua rushwa kwa dereva 

Na Lauden Mwambona

Imepakiwa - Tuesday, July 10  2018 at  11:34

Kwa Muhtasari

Askari wajiepushe na  tabia ya kutaka kumkomoa dereva

 

Suala la ajali ni la kawaida barabarani, lakini ukweli ajali zinaumiza na kuua wengi.

Kwa mfano, ndani ya siku 30, watu 40 wamefariki dunia mkoani Mbeya huku wengine karibu 100 wakijeruhiwa.

Vifo hivyo vimewashtua wengi, akiwamo Rais John Magufuli ambaye hakusita kuelezea hisia zake alipozungumza kwenye hafla ya kuwaapisha mawaziri aliowapangia kazi mpya akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Kwa miaka mingi imekuwa kawaida kutokea kwa ajali maeneo mbalimbali nchini, huku makamanda wa polisi wakitoa sababu tofauti.

Kwa mfano, taarifa za polisi kuhusu ajali zilizotolewa mwishoni mwa mwaka jana mkoani Mbeya zilionyesha jumla ya makosa yote ya ajali pamoja na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani kwa kipindi cha mwaka 2017 yalikuwa 82,211 wakati kipindi kama hicho mwaka 2016 yalikuwa 66,172.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba ajali zilizosababisha vifo mwaka 2017 zilikuwa 141, wakati mwaka 2016 zilikuwa 182 na watu waliofariki dunia mwaka 2017 walikuwa 170, wakati mwaka 2016 walikuwa 286.

Kwa kifupi, makamanda wa polisi wanatoa taarifa za matukio ya ajali kwa kirefu, lakini vyanzo vya ajali havielezwi kwa kina au kutajwa mara kwa mara huku watu kadhaa wakiwatupia lawama wasimamizi hawa wa sheria.

Watu wengi wanaamini vyanzo vya ajali ni usimamizi mdogo wa sheria za usalama barabarani, huku wakisisitiza rushwa imetawala kwa baadhi ya askari wa usalama barabarani.

Kwa kawaida askari hawa ni muhimu sana kuwapo barabarani wakati wote, kwani wanasaidia kusimamia sheria za usalama barabarani pia kupata taarifa za uhalifu, ikiwa ni pamoja na kuzuia mwendo kasi wa magari.

Pamoja na umuhimu wao, wamekuwa wakilaumiwa kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa jambo ambalo naamini wanatakiwa wajisafishe wenyewe.

Kwa mfano, wamiliki na madereva wa magari mbalimbali yakiwamo mabasi hususan ya kutoka jijini Mbeya kwenda Kyela, Mbarali, Tunduma na Chunya wanawalalamikia askari wa barabarani kwa madai ya kupenda rushwa.

Ni jambo la kawaida kuwasikia hata baadhi wa abiria wakiwa ndani ya mabasi wakiwakashifu matrafiki wanaosimamisha mabasi barabarani.

Bila shaka kashfa hizo na kejeli nyingi zinatolewa kutokana na ukweli kwamba baadhi ya trafiki ni kama vichekesho wawapo katika kazi zao huko barabarani.

Ni kawaida madereva na makodakta kufanya mawasiliano na wenzao waliotangulia mbele wakitambulisha maeneo ya trafiki na hata kuyataja majina ya trafiki waliopo sehemu hizo.

Baada ya kupata taarifa, kondakta na dereva hujadiliana ndani ya basi kuhusu kiasi cha fedha za kuwapa trafiki, huku abiria wote wakisikia na kuona mchezo wote hadi trafiki wanavyopewa mshiko huo.

Matukio ya aina hii ndiyo yanayosababisha abiria wengi waamini trafiki wanaishi kwa rushwa.

Mbeya wanaamini bajaji zinabeba watu sita ni kwa sababu ya rushwa. Mbeya wanaamini daladala na mabasi ya kwenda wilayani hayatoi tiketi kwa sababu ya rushwa.

Kama kitengo cha usalama barabarani kinataka kujinasua katika hili, wakati umefika kuwakamata madereva au makondakta watakaoteremka kwenye magari yao na kutoa rushwa.

Trafiki wanaweza kuweka mkakati kwamba, kuanzia saa kumi na moja asubuhi hadi saa kumi jioni iwe operesheni ya kuwakamata madereva au makondakta watakaoteremka wakiwa na fedha mikononi. Hata hivyo, askari nao wajiepushe tabia ya kutaka kumkomoa mmiliki ama dereva.