Maduro alianza kwa sifa yakinifu sasa aonekana kukataliwa

Nicolas Maduro

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela aendesha gari wakati wa mgomo ulioitishwa na upinzani Julai 20, 2017. Picha/AFP 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, August 5  2017 at  13:40

Kwa Mukhtasari

Rais wa Venezuela Nicolás Maduro akiwa kwa sasa taabani na watu wake anaowaongoza ni mfano bora wa paka aliyeitwa na wahenga kuwa na mioyo saba.

 

RAIS wa Venezuela Nicolás Maduro akiwa kwa sasa taabani na watu wake anaowaongoza ni mfano bora wa paka aliyeitwa na wahenga kuwa na mioyo
saba.

Unamtandika paka ukilenga kumuua, unamponda kisawasawa na wakati unaeendea jembe uje uzike maiti yake ukidhania umemuua, unampata ako katika hali shwari ya kiafya.

Miezi mitatu iliyopita, Rais Maduro alijaribu kutumia nguvu zake visivyo kwa nia ya kujithibiti mamlakani ambapo alilenga kusambaratisha upinzani bungeni kupitia washirika wake walio katika mahakama ya juu zaidi katika taifa hilo.

Maandamano ambayo yalizuka yalimlazimisha kutema nje wazo hilo kutoka fikira zake, baada ya watu takriban 120 kuaga dunia katika maandamano
hayo.

Wakati wajuao siasa husema mamlaka ya utawala hufisidi mawazo ya wasiomakinika kiuongozi, Rais Maduro ndiye huyo tena, sasa akilenga kubadili katiba ili kujikusanyia mamalaka yanayosemwa kuwa ya kiimla katika kiti chake cha urais.

Ni katika hatua hiyo ambapo amependekeza upinzani uvunjwe na taifa hilo libakie na utawala wa chama kimoja ambacho ni Maduro, mamlaka
yawe ni Maduro na idhini ya mwisho kuabudiwa iwe ni Maduro.

Wengine wanadai kuwa hata angekuwa na uwezo, angebadili jina la taifa hilo liwe likifahamika kama Maduro.

Ni hatua ambayo imezua shutuma kali kutoka kwa jamii za Kimataifa lakini Kenya sio mojawapo ya mataifa hayo ya kukemeana kwa kuwa hujifanya kuwa taifa lisiloegemea upande wowote katika masuala ya mataifa yanayojitawala.

Kinaya ni kuwa majeshi yake yako katika taifa huru la Somalia, kwa muungano wa huduma za kijeshi za kimataifa, kwa nia ya kuliosha taifa hilo kutokana na jinamizi la magaidi wa Al-Shabaab.

Rais wa Marekani, Donald Trump kwa sasa ametuma ujumbe wa moja kwa moja kwa rais Maduro, akimtaka akome kujiweka katika kundi la uongozi lisilokubalika katika Karne hii ya 21.

Amemtaka Maduro azingatie kupanuka kwa hali ya demokrasia ulimwenguni, akubali kuwa anaweza akakosolewa na anaowatawala na ajiepushe kwa kujituma na miradi ya kukandamiza upinzani katika taifa lake.

Maduro alikuwa dereva wa basi kabla ya kufanikiwa kujitosa katika ulingo wa siasa na akaishia kuwa rais.

Wengi wa Madereva wa mabasi hapa nchini Kenya wako na uzoeefu wa kuwa watundu, ikizingatiwa kuwa ni wiki mbili sasa zimepita tangu mmoja wao
na washirika wake wengine wawili wahukumiwe kunyongwa na mahakama kuu hapa nchini kwa makosa ya kumvua nguo mwanamke, wakamdhalilishia utu wake kupitia dhuluma chafu na za kikatili dhidi ya uke wake na hatimaye wakampora.

Rais Maduro hakuishia kuhukumiwa mauti katika taifa hilo lake lakini amekuwa katika mkondo wa kupanda na kupaa akiishia kwa sasa kuwa rais anayedadisiwa kutojua afanye lingine tena lipi la kumpa hadhi zaidi, akichanganyikiwa hadi sasa kuamua kuwa dikteta wa dhati.

Rais wa wanafunzi

Wazo la uongozi lilimuingia akiwa katika shule ya upili ambapo alichaguliwa kuwa rais wa wanafunzi wenzake shuleni lakini hakufaulu kutimiza lengo lake la kimasomo kwa kuwa alijiondoa shuleni.

Akiwa rais wao wa muda, Maduro na ujana wake alikuwa mwingi wa hotuba za haki za wanafunzi, hakuwa wa kuchochea katika hotuba hizo lakini akisema kitu au suala lolote lile, alikuwa akichukuliwa kwa uzito kupitia ufasaha wake wa kiusemi.

Alipojiondoa shuleni, Maduro aliingia mitaani na akaamua kuwa mtunzi na mwimbaji wa ngoma mtindo wa Rock lakini akawa hajapata kitulizo chake cha maisha na ndipo akaamua kuwa dereva wa basi.

Alianza huduma yake mpya katika mabasi ya mji mkuu wa Venezuela na ambao ni Caracas, na mara moja akaunda ushirika wa mabasi ili kuwapa
wahudumu wenza sauti ya kujitetea.

Ni katika harakati hizo za udereva ambapo alijiunga na mrengo wa raia wa kuunga mkono aiyekuwa rais wa taifa hilo, Hugo Chavez, wakati huo Chavez akiwa kizuizini.

Maduro alikuwa mwingi wa ushawishi na ndipo alifanikiwa kusukuma utawala wa wakati huo kumwachilia huru Chavez.

Mwaka wa 1999, Maduro akachaguliwa kuwa mbunge na Chavez sasa akiwa rais, akamteua Maduro kuwa waziri wa masuala ya kigeni.

Maduro akawa sasa amepata sauti ya kujiangazia kama kiongozi shupavu wa Venezuela na mtetezi sugu wa haki za kibinadamu.

Alisuta gereza linalothibitiwa na Marekani la Guantanamo Bay nchini Cuba kama “kichinjio cha halaiki ya watu".

Chavez alikuwa mwingi wa shukran kwa Maduro, na alipokuwa anaaga dunia kwa kasi kupitia maradhi ya Kansa, akawaelekeza watu wa Venezuela wamchague Maduro kuwa mrithi wa urais.

Alimtaja Maduro kuwa mwerevu kupindukia, mwenye uwezo wa kimaajabu na aliye na uwezo wa kusongesha Venezuela mbele kwa hali zote za
changamoto na ufanisi.

Maduro naye akaamkua kutawazwa kwake na Chevez kwa ueledi mkuu kwa kuwa watu wa taifa hilo walimpenda kwa dhati rais wao ambaye aliaga
dunia muda baadaye ya kumtawaza Maduro kuwa mrithi.

Katika kampeni zake za kuwa rais, Maduro alikuwa akitoa fichuzi za jinsi "Marehemu Chavez amenitembelea jana, leo…Akiwa na umbo la
malaika na akanipa ushauri wa kuwaongoza mkinichagua kuwa rais wenu".

Mapenzi ya Chavez miongoni mwa watu wa Venezuela yakawafanya wamwamini Maduro na mwaka wa 2013, akaishia kuchaguliwa licha ya
upinzani mkali uliomwezesha tu kupata asilimia 1.5 zaidi ya kura.

Alipoingia usukani, aliwatimua mabalozi wa mataifa kadhaa kutoka taifa hilo akisema kuwa ndiyo walimuua Chavez kwa kumpa sumu!

Maduro akiwa mamlakani kwa miaka minne sasa, uchumi wa taifa hilo umesambaratika kwa asilimia 23, kuna janga la njaa na sekta ya afya
iko taabani kupitia ukosefu wa dawa.

Maandamano ndio kiamsha kinywa, chakula cha mchana na cha jioni katika taifa hilo huku Maduro akiwa mbioni kusambaratisha upinzani badala ya kusaka mdahalo wa kitaifa kupata suluhu kwa matatizo yake mwenyewe kama rais, kwa watu wa taifa hilo na kwa imani ya jamii za
kimataifa.

Huku akikabiliana na hali hiyo, kura za maoni taifa hilo zinamuonyesha akiwa na ufuasi wa chini ya asilimia 20 na gazeti la New York Times limemtaja kama “rais aliye mashakani zaidi kisiasa ulimwengu mzima".