Maelewano ya Polisi,na wananchi ni muhimu

Imepakiwa - Monday, May 13  2019 at  11:56

 

Katika toleo letu la jana, kulikuwa na habari ya ndugu
ambao wamesusia kuchukua mwili wa ndugu yao mkoani
Dodoma wakidai kuwa kifo chake kilitokana na kupigwa
na polisi baada ya kukamatwa.
Mwili wake sasa umeshakaa Hospitali ya Rufaa ya
Dodoma kwa takriban siku 11 tangu alipofariki baada ya
kupelekwa hospitalini hapo akiwa hajitambui.
Mashuhuda wanadai kuwa kijana huyo alipelekwa
hospitali akiwa amefungwa pingu na hajitambui, lakini
hali yake ilipozidi kuwa mbaya, alifunguliwa pingu hizo
na askari hawakuonekana tena hadi alipofariki dunia.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, kamanda wa polisi wa
mkoa, Gilles Muroto alisema amechukua taarifa hizo na
atazifuatilia.
Tuhuma hizo za raia kupigwa hadi kupoteza maisha
akiwa mikononi mwa polisi, si za kwanza na hata safu hii
imeshawahi kuandika mara kadhaa kuhusu matukio hayo,
lakini tunalazimika kuandika kila mara kutokana na
umuhimu wa maisha ya kila Mtanzania na pia umuhimu
wa kufanya kazi kwa kufuata maadili, kutoa ripoti za

matukio nyeti kwa wakati na kusikiliza malalamiko na
tuhuma za wananchi na kuzifanyia kazi kila zinapotokea.
Mara kadhaa wananchi wamesusia kuchukua miili ya
ndugu zao hospitalini kutokana na kutuhumu kuwa
waliuawa baada ya kupigwa na polisi wakati wakiwa
wamekamatwa kwa uchunguzi.
Jeshi la Polisi limekuwa likitoa taarifa ambazo
haziridhishi kwa ndugu hao na ndio maana moja ya maiti
mkoani Mbeya ilikaa hospitalini kwa zaidi ya siku 100.
Hili si jambo jema kwa kuwa halitoi picha nzuri kwa jeshi
letu la polisi ambalo moja ya kazi zake kuu ni kulinda raia
na mali zao.
Lakini kazi hiyo haionekani kutekelezwa kikamilifu na
baadhi ya askari au hata baadhi ya vituo. Baadhi ya askari
wameonekana kufanya kazi zao tofauti na maadili.
Hata hivyo, taarifa zinazotolewa baadaye kuhusu matukio
hayo hazionekana kuwa zina hatua za kumuwajibisha
aliyefanya kitendo hicho kwa sheria za kijeshi au katika
mahakama za kiraia, jambo linalofanya watu wasiamini
kama chombo hicho cha dola kinawajibika ipasavyo kwa
wananchi ambao wanalipa kodi ili kiweze kufanya
shughuli za ulinzi wa maisha na mali zao kwa niaba yao.
Hata pale inapotokea viongozi wa juu kukemea vitendo
hivyo, bado matukio hayo hayaonekani kukoma, kiasi
kwamba kunaweza kujengeka uadui kati ya raia na

wananchi, jambo ambalo ni tofauti na nchi nyingine
ambako polisi ni rafiki wa raia.
Uhusiano huu baina ya wananchi na polisi haujengwi
kutokana na maelewano binafsi, bali kwa kila upande
kutekeleza wajibu wake ipasavyo; wananchi kutii sheria
na kushiriki kutoa taarifa za uhalifu na polisi kulinda raia
na kutumia taarifa zao kukomesha uovu.
Kila mmoja anapotekeleza majukumu yake ipasavyo,
imani inajengeka kwa kila upande na matokeo yake
kunakuwa na uhusiano mzuri unaofanya amani na utulivu
uzidi kudumu kwenye jamii. Hata hivyo, kila upande
ukianza kutuhumiana kufanya uovu na mwingine ukifikia
hadi kuchukua hatua ya kuhukumu, hakutakuwa na
mahusiano mazuri kama inavyoonekana sasa kwa baadhi
ya familia kugomea kuchukua miili ya ndugu zao
waliofariki wakiwa mikononi mwa polisi.
Hali hii haifai iendelee na inatakiwa ikomeshwe mara
moja kwa Jeshi la Polisi kuchukua hatua dhidi ya askari
wake wanaotuhumiwa, na umma uone linachukua hatua
ili kurejesha imani kwa chombo chao.
Taifa hili ni letu sote na kama inavyosema Katiba yetu,
haki na usawa ndizo nguzo muhimu za maisha