Mafundi wa mitaani waongezewe ujuzi vyuoni

Imepakiwa - Thursday, May 2  2019 at  11:23

 

Kutokana na kuwapo kwa changamoto za maisha, watu wengi wamejifunza masuala ya ufundi mitaani na kujiajiri.

Hata hivyo, wengi wao wanafanya kazi zao kwa kutegemea vipaji na ujuzi mdogo walioupata kutoka kwa wenzao bila kuingia darasani.

Wengi hufanya hivyo kutokana na kutokuwa na fedha au kiwango kidogo cha elimu ambacho kiliwanyima fursa ya kwenda chuo cha ufundi kusoma.

Hivyo, wanaposhinda nyumbani au katika eneo lililo karibu na ofisi inayohusika na masuala ya ufundi iwe wa umeme au magari, huvutiwa kufanya kazi hizo.

Mafundi hao wa mitaani kutokana na uzoefu walionao wakiongezewa mafunzo wanaweza kufanya mambo makubwa katika sayansi na teknolojia.

Kutokana na jitihada binafsi za mafundi hao pamoja na kiwango kidogo cha ujuzi, ni vyema Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), kwa kushirikiana na wadau wengine wakawasaidia vijana hao kuwapa elimu.

Ni wazi kuwa elimu watakayoipata itawaongezea ujuzi na kazi zao kuboresheka zaidi.

Mbali na hilo, lengo jingine ni kuwawezesha kufanya kazi zinazokidhi viwango vya ubora bila kuharibu au kuleta madhara kwa mali za wateja wao.

Hiyo italisaidia Taifa kufikia azma ya kuwa na Tanzania ya viwanda kwa kuwa na mafundi bora.

Pia, mafunzo hayo ya Veta yatawasaidia kupata vyeti na kutambulika kwa mujibu wa sheria.

Faida nyingine ni kwamba, endapo kutatokea nafasi ya kazi mahali popote, wakiomba wanaweza kupokewa na kuifanya kazi kwa weledi kutokana na kuwa na vyeto vinavyothibioisha kuwa ‘wameiva’.

Miongoni mwa kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na mafundi hao ni kutengeneza umeme, magari, nyumba na vitu mbalimbali kwa kujifunza kutoka kwa ndugu jamaa au marafiki.

Kutokana na elimu hiyo kuipata kwa ‘kuibia ibia’ kazi zao zinakuwa hazina ubora unaotakiwa ila wakapopatiwa mafunzo ya Veta, kazi zitaboreka.

Hiyo pia itawasaidia kupata kazi nyingine walizokuwa wanazikosa kutokana na kutokuwa na vyeti, hivyo mteja kutokuwa na imani nao.

Jambo hilo la kukosa kazi za uhakika kutokana na kutokuwa na vyeti, limekuwa likiwarudisha nyuma na kuwafanya washindwe kufikia ndoto zao kwa wakati.

Kila siku wanajikuta wanafanya kazi za kuwapatia kipatao kidogo kutokana na kutokuwa na elimu inayowatambulisha kwamba wamefunzwa wakafunzika.

Umuhimu wa elimu hiyo ya muda mfupi ni kwamba, itawasaidia kujua namna ya kutafuta masoko na kutengeneza bidhaa zenye ubora zinazokubalika ndani na nje ya nchi.

Mafunzo hayo yanaweza kutolewa kwa mfumo wa semina kwa kuwakusanya mafundi wa mitaani kulingana na fani wanazohitaji kuzisomea.

Pia, wanaweza kuchangishwa fedha kidogo kwa ajili ya walimu watakaokuwa wanafanya kazi hiyo ya kuwafundisha, lengo likiwa ni kuwa na vijana wanaojitambua katika kazi zao na nini wanachopaswa kufanya katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.

Pia, watakuwa na uwezo, wabunifu na kutafuta fursa mbalimbali kwenye maeneo tofauti mbali na wanakofanyika kazi zao.

Kuna watu wamesomea ufundi lakini hawaipendi kazi hiyo, hivyo hawa ambao wanaipenda na wamefanya jitihada za kutumia uwezo na uzoefu walionao katika kujifunza utengenezaji wa bidhaa mbalimbali wawezeshwe ili waweze kukubalika mahali popote.

Wadau na taasisi mbalimbali zijitokeze kuwaandalia mafunzo kwa kushirikisha mamlaka husika, ili vijana waweze kukamilisha ndoto zao kitaaluma na kwa ufanisi wa hali ya juu.

Kwa kuwa kuna watu wanajifanya mafundi, lakini kumbe hawana hawajui kufanya chochote wanachotafuta ili mradi mkono uende kinywani, mafunzo hayo yatawasaidia wananchi kuwatambua wenye ubora kwa sababu mtu atakuwa akihitaji fundi mwenye cheti ili kupata uthibitisho kwamba si ‘kishoka’.

Hii itasaidia wale wanaofanya kazi za ufundi bila kufuata miongozo au taratibu zinazotakiwa.

Pia itawasaidia wananchi au wateja kuepuka majanga ya moto utokanao na umeme na ajali za barabarani kwa sababu watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya mafundi wawatakao na pia ambao ni mahiri na bora.

Uchambuzi huu umeandikwa na mwandishi wa gazeti hili anayepatikana kwa namba 0755-634762