Magufuli na Ushairi

Na Na Athumani B. Mitimingi (Vumbi)

Imepakiwa - Wednesday, March 27  2019 at  10:21

 

Uokoe ushairi, Mheshimiwa Magufuli,

Tuokoe jemadari, kwa mawazo hatulali,

Kazi zetu pia ari, za bure hawatujali,

  Ni Rais Magufuli uokoe ushairi.

Hawatujali kabisa,  Baraza la Kiswahili,

Waulizwapo hususa, na pia hawakubali,

Hivi lipi letu kosa, hadi twapigwa kabari,

  Ni Rais Magufuli, uokoe ushairi.

Wenzetu hawana utu, nawashitakia kweli,

Kwa Magufuli thubutu, akiamua hulali,

Asema hapa kazi tu, keshaianza shughuli,

  Ni Rais Magufuli, uokoe ushairi.

Mfano tupo wodini, tupo hoi Muhimbili,

Yaani ni masikini hakuna wa afadhali,

Haraka tuokeni, tusidondoke msuli,

  Ni Rais Magufuli, uokoe ushairi.

Vipi hatupewi posho, mshahara wa halali,

 Lapotea letu jasho, tokea ile awali,

Mboga twala mchemsho, hakuna cha kachumbari,

  Ni Rais Magufuli, uokoe ushairi.

Umuite wao bosi, aje na letu faili,

Ulipekue kiasi, utaziona  dalili,

Kwamba hakuna mabosi, ilotupa serikali,

  Ni Rais Magufuli uokoe ushairi.

Umuulize kiini, Magufuli tafadhali,

Washairi kuwa duni, toka masika na vuli,

Watupe sababu nini, waijibu kwa ukali,

  Ni Rais Magufuli, uokoe ushairi.

Tungo tunazoandika, zinaelimisha kweli,

Jamii yafaidika, mashuleni na mahali,

Hapa mwisho nimefika, Kigoma mwisho wa reli,

  Ni Rais Magufuli, uokoe ushairi.

Mwisho.