http://www.swahilihub.com/image/view/-/4555972/medRes/1969196/-/bi93qlz/-/mshindo.jpg

 

Dkt Mahathir Mohamad: Akiwa na umri wa miaka 92 amechaguliwa kuongoza Malaysia

Mahathir Mohamad

Waziri Mkuu mpya aliyechaguliwa Malaysia, Bw Mahathir Mohamad, 92, azungumza na wanahabari Mei 11, 2018, jijini Kuala Lumpur. Picha/AFP 

Na SAMMY WAWERU na MASHIRIKA

Imepakiwa - Monday, May 14  2018 at  10:08

Kwa Muhtasari

Waziri Mkuu wa Malaysia aliyeapishwa mapema Mei 2018 ndiye kiongozi mkongwe zaidi duniani kuingia madarakani akiwa na umri wa miaka 92

 

DKT Mahathir Mohamad ambaye aliwahi kuhudumu katika wadhifa huo miaka ya zamani, alizaliwa mnamo Julai, 1925. Kati ya 1981-2003, alishikilia wadhifa wa uwaziri mkuu na ndiye kiongozi aliyehudumu chini ya wadhifa huo kwa muda mrefu.

Dkt Mohamad amekuwa katika ulingo wa siasa kwa zaidi ya miaka 70, tangu ajiunge na chama cha United Malays National Organisation (UMNO) mnamo1946. Hata hivyo baadaye aliunda chama chake cha Malaysian United Indigenous Party mwaka wa 2016.

Ingawa safari ya kiongozi huyo katika ulingo wa siasa haikukosa kukumbwa na changamoto za hapa na pale. Alikuwa mwanachama machachari wa UMNO hata kabla hajaingia bunge la Malaysia 1964.

Bungeni alihudumu kwa awamu moja pekee; kisha akazozana na waziri mkuu wa nchi hiyo wakati huo Tunku Abdul Rahman.

Songombingo ya wawili hao ilisababisha kutimuliwa kwake katika chama hicho.

Waziri huyo alipojiuzulu, Dkt Mohamad alirejea bungeni na katika chama cha UMNO ambapo alipandishwa madaraka kujiunga na baraza la mawaziri la Malaysia.

Kufikia 1976 alikuwa amekwea hadi wadhifa wa naibu waziri mkuu, na 1981 akaapishwa kama waziri mkuu kufuatia kujiuzulu kwa Hussein Onn aliyemrithi waziri Rahman.

Chini ya utawala wa Dkt Mohamad, Malaysia ilikua kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuimarika kiteknolojia. Aidha, alifanya miradi mbalimbali ya kuimarisha barabara na mawasiliano. Juhudi zake zilimfanya kuongoza nchi hiyo kwa awamu tano mtawalia. Mohamad aliweka misimamo kali ya usalama wa ndani, ambapo wanaharakati, mashirika ya kutetea haki za kijamii, wakosoaji wake na wasiokuwa wakristu walitiwa nguvuni. Naibu waziri mkuu wake Anwar Ibrahim, alikuwa mmoja wa wakosoaji wake ambaye alimtimua kazini 1998.

Uhusiano wake na mataifa ya kigeni kama vile Marekani na Uingereza, miongoni mwa mengine ulianza kudorora.

Mnamo 2004, Abdullah Ahmad Badawi alimrithi ingawa Dkt Mohamad alikuwa mkosoaji wake mkuu wa utawala wake. Aliongoza hadi 2014, akafuata Najib Razak aliyekuwa nahodha wa wadhifa huo hadi Muhamad akarejea mamlakani.

Chama kusajiliwa rasmi

Mwaka wa 2016, Dkt Mohamad alijiuzulu uanachama wa UMNO na mwaka huo huo Septemba 9 ndipo chama chake cha Malaysian United Indigenous Party kilisajiliwa rasmi na akakitumia kuwania uchaguzi mkuu uliokamilika. Katika uchaguzi huo wa hivi punde, alipata ushindi wa kihistoria. Aidha, kiongozi huyo aliweza kukiangusha chama cha Barisan National ambacho kimekuwa madarakani tangu 1957. UMNO imekuwa ikituhumiwa kujihusisha na sakata za rushwa na ufisadi.

Dkt Mohamad akiwa na umri wa miaka 92, wiki iliyopita alishinda kwa idadi ya wingi wa kura,na kukibwaga chama hicho kilichotawala kwa zaidi ya miaka 60.

Utawala wa Razak umekumbwa na shutuma nyingi za ufisadi. Bw Ibrahim Suffian, ni mtafiti wa masuala ya uchaguzi wa kujitegemea wa mji wa Kuala Lumpur, na anasema matokea hayo yalileta mshangao kwa kila mmoja. "Sote tumeshangazwa na ushindi wa Dkt Mohamad, ilikuwa vigumu kutabiri nani angeibuka mshindi jinsi kura zilivyoemdelea kutiririka na kuhesabiwa," anasema.

Malaysia katika utawala wa awali, imekuwa ikishuhudia kupanda kwa gharama ya maisha na ongezeko la visa vya utengano wa kikabila, jambo ambalo mtafiti huyo anasema Dkt Mohamad aliweza kushawishi wapiga kura ndiposa wakamchagua kwa wingi wa kura. "Ameweza kutambua maswala yanayokumba nchi hiyo kama vile kupanda kwa gharama ya maisha, kodi ya nyumba na kero la ufisadi lililomhusisha mtangulizi wake, na aliahidi kutatua hayo yote ndio maana akachaguliwa bila pingamizi," anafafanua Ibrahim.

Anaongeza kuwa kiongozi huyo amefahamu kwa kina masaibu ya Malaysia kwa zaidi ya miaka 60. Anasema waziri Razak alishindwa kudhibiti mengi kwa kuwa anahusishwa na kashfa ya kudaiwa kujipatia kiasi cha dola 700 kutoka kwa taasisi moja ya maendelea ya Malaysia na mamlaka zinaendelea kuichunguza.

Dkt Mohamad amesomea udaktari. Alisomea taaluma hiyo katika King Edward VII College of Medicine, Singapore mojawapo ya taasisi ya Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Singapore.

Ni mume wa Bi ambapo wamejaaliwa kupata watoto watatu, ingawa ana wengine idadi sawa na hiyo wasiokuwa wake kuzaliwa na anawalea.

Waziri huyo kabla ya kujitosa katika ulingo wa siasa, alihudumu kama wa daktari wa serikali ya Malaysia.

Malaysia ni nchi ya Asia Kusini, iliyoko kando ya Bahari ya Kusini ya China.

Kisiasa nchi hiyo ni shirikisho la majimbo 13. Ina sehemu mbili ambazo ni, Bara la Malaysia na Kisiwa cha Malaysia. Aidha, imepakana na Uthai, Singapore, Brunei na Indonesia.

Taifa hilo lilianzishwa mwaka wa 1963 wakati shirikisho la Kimalay liliungana na Singapore, Sabah na Sarawak.