http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802684/medRes/2138410/-/2vl6bz/-/majaliwa.jpg

 

Majaliwa awanyooshea kidole watumishi wazembe, wadokozi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Kongwa ambaye ni Spika wa Bunge, Job Ndugai (kulia) baada ya kuwasili wilayani Kongwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Dodoma, jana. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu  

Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  11:30

Kwa Muhtasari

Watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao watapa shida kwenye Serikali hii

 

 

mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wawe waadilifu na waaminifu wanapotekeleza majukumu yao kwani vitendo vya udokozi wa mali ya umma havitavumiliwa na Serikali.

Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa jana katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara mkoani Dodoma, alisema Serikali haitamvumilia mtumishi wa umma ambaye si mwadilifu, mvivu na walarushwa hawana nafasi.

Alisema ni lazima kila mmoja awajibike na ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao watapa shida kwenye Serikali hii.

“Hakuna mchezo kwenye Serikali hii, watumishi wa umma wanapaswa kulitambua hili,” alisema.

Majaliwa aliwataka watumishi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020. Pia, aliwataka wahakikishe wanapanga ratiba ya kwenda kuwatembelea wananchi hususan waishio vijijini na kushirikiana nao katika kutatua kero zinazowakabili si kukaa ofisini.

Awali, Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye ni pia Mbunge wa Kongwa, aliishukuru Serikali kwa kutatua kero mbalimbali ikiwamo changamoto ya ukosefu wa maji na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mbande hadi Kongwa ambapo aliomba ujenzi huo uendelee hadi Mpwapwa.

Pia, aliiomba Serikali kugawa kwa vipande eneo la Ranchi ya Taifa lililopo wilayani hapo kwa wafungaji kwa kuwa limekuwa halitumiki.

“Napendekeza wananchi wapewe vitalu wafuge kwa njia ya kisasa kwa kupatiwa mbegu bora. Hii itasaidia kuzalisha bidhaa bora za nyama na maziwa pamoja na wananchi kupata ajira,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi aliishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha za kutekeleza miradi mbalimbali wilayani humo, hadi sasa wameshapokea zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema mafanikio ya Kongwa ni matokeo ya uwepo wa amani na utulivu.

Hata hivyo, alimuomba Waziri Mkuu baada ya Rais kusaini sheria ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi ni muhimu ikapewa kipaumbele na miji mingine midogo inayozunguka jiji la Dodoma kupata fedha za kupima maeneo.

Juzi, Majaliwa alihutubia wananchi kwenye uwanja wa Shule Msingi Mpwapwa na kupokea malalamiko ya wananchi juu ya ukosefu wa dawa. Wananchi hao walidai dawa pekee wanazopewa ni za kutuliza maumivu.

Katika mkutano huo huo alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri afanye uchunguzi kuhusu matumizi ya Sh70 milioni zinazotolewa kila mwezi na Serikali kwa ajili ya kununulia dawa kwenye wilaya hiyo.

“Kilichokuwa kinasemwa na wabunge bungeni nilidhani sicho, nikasema nakuja niyasikie mwenyewe. Kweli wananchi hawaridhiki nimeona. Mkuu wa wilaya shughulikia hili ili kubaini fedha za dawa zinakwenda wapi,” alisema.