http://www.swahilihub.com/image/view/-/5026392/medRes/2258885/-/xjcvgw/-/uti+pic.jpg

 

Majibu sahihi ya UTI si chini ya siku mbili

Mkuu wa mafunzo wa Chuo Kikuu cha KCMC mjini Moshi, Profesa Alfred Mteta 

Na Kalunde Jamal, Mwananchi kjamali@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, March 15  2019 at  10:33

 

Dar es Salaam. Fikiria unajisikia vibaya au mwanao ni mgonjwa, unalazimika kumpeleka zahanati au kituo cha afya ili akafanyiwe vipimo vya kitabibu mwilini.

Baada ya kufika anaambiwa atoe mkojo, lakini ndani ya saa moja au chini ya hapo tangu akabidhi haja hiyo ndogo maabara, daktari anakuita na kukuambia anasumbuliwa na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI).

Kwa kuwa umezoea, hushangai, unaona ni kawaida. Hii yote ni kwa kutojua kwani vipimo vya UTI vinapaswa kutoka maabara kati ya saa 48 hadi 72 (yaani siku mbili hadi tatu) kwa kuwa hatua muhimu za kupima mkojo zinahitajika kufuatwa ili kuwa na uhakika wa ugonjwa huo au la.

Mkuu wa mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha KCMC mjini Moshi, Profesa Alfred Mteta ameliambia Mwananchi kuwa, “huo ndiyo utaratibu (wa kutoa majibu kuanzia saa 48 hadi 72) ambao sasa unavunjwa na baadhi ya watu wasio na weledi kwenye taaluma ya afya, ambao huchukua njia ya mkato na kubambikiza wateja UTI ili kuwauzia dawa tu.”

Profesa Mteta alisema ili kujua kama mtu ana UTI au la, mkojo wake unatakiwa kupita kwenye vipimo saba.

Akizumgumza na gazeti hili, mganga mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi alisema waliopewa mamlaka ya kulinda afya za wananchi wanaonekana kusahau jukumu lao na kutoa majibu ndani ya muda mfupi, hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi.

“Tumekuwa tukisema mara nyingi hatua za kupima maradhi hayo, kwanza unaupima mkojo na unaweza kupata mabadiliko ya mkojo kwa kupima kipimo cha kwanza ukahisi ni UTI, ilhali kitaalamu ni lazima kujiridhisha kabla ya kutoa uamuzi wa majibu kwa mgonjwa,” alisema Profesa Kambi.

Zulfa Zayd aliyekuwa akipima afya kwenye zahanati moja iliyopo Kinondoni, alisema, “hee! Huu ugonjwa umening’ang’ania kila nikijisikia vibaya nikipima nakutwa na UTI na dawa ninazopewa ni hizi hizi Ciprofloxacin.”