http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706216/medRes/2074861/-/t7nqcxz/-/majuto.jpg

 

Mzee Majuto ametuachia funzo kubwa

King Majuto

Rais John Magufuli akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa mwigizaji nguli wa vichekesho nchini, Mzee King Majuto katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  09:21

Kwa Muhtasari

Tasnia ya sanaa Tanzania na Taifa kwa jumla ipo katika maombolezo ya kifo cha msanii maarufu wa vichekesho, Amri Athuman maarufu King Majuto au Mzee Majuto aliyefariki usiku wa Agosti 8, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu tangu alipofikishwa Julai 31.

 

TASNIA ya sanaa Tanzania na Taifa kwa jumla ipo katika maombolezo ya kifo cha msanii maarufu wa vichekesho, Amri Athuman maarufu King Majuto au Mzee Majuto aliyefariki usiku wa Agosti 8, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu tangu alipofikishwa Julai 31.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali kuhusu wasifu wake, Mzee Majuto ambaye alizaliwa mwaka 1948 mkoani Tanga alianza shughuli ya kuigiza akiwa mtoto mdogo wa miaka tisa na alijiendeleza hadi kufikia kuwa mtunzi, muigizaji, mwandishi wa mswada aliyebobea na haishangazi kusikia kwamba ndiye muigizaji wa kwanza nchini kuandaa kazi zake katika mikanda.

Ameshiriki kuigiza filamu na michezo mbalimbali ambayo hadi leo hii inaendelea kukonga mioyo ya watu wengi hususan wale wanaofahamu au kujifunza Kiswahili.

Alikuwa mwigizaji wa aina yake aliyekubalika na makundi rika ya aina zote kuanzia watoto, vijana na wazee kwani kazi zake nyingi za sanaa ziliyasadifu na kila moja kuhisi kuwakilishwa vyema na msanii huyo.

Kutokana na umaarufu huo kampuni na taasisi nyingi zilimkimbilia kwa ajili ya kutengeneza matangazo ya biashara zikiamini kwamba alikuwa kiigizo chema katika jamii, hivyo kuwa rahisi ujumbe wao kukubaliwa na wananchi.

Mzee Majuto amefariki dunia lakini kazi zake zitaendelea kubaki katika mioyo ya Watanzania wengi, zina mafunzo mengi ambayo uwasilishaji wake umejengwa katika misingi ya kuburudisha hivyo kumbukumbu yake kutoondoka kirahisi.

Maandiko ya dini yanatuambia kwamba kifo ni mawaidha tosha, kinatupa fursa ya kujitathmini na kukumbuka kwamba kila mmoja wetu naye ataondoka kwa namna au sababu tofauti. Jambo la kujiuliza ni namna tutakavyoacha alama katika jamii inayotuzunguka na hata mbali zaidi.

Hayati Mzee Majuto analiliwa na kila kundi rika kutokana na jinsi alivyoishi. Hakuwa na tabia ya majivuno wala kujikweza licha ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao ndani na nje ya nchi. Alimheshimu kila mtu na kushirikiana naye.

Aliishi kazi yake na ndiyo maana aghalabu kila aliyebahatika kumuona akipita barabarani au kushiriki katika tukio lolote, aliishia kucheka hata kabla Mzee Majuto hajazungumza. Kimsingi alikubalika katika jamii.

Kujifunza

Hivyo basi, ni jukumu letu na hususan wasanii wenzake kujifunza mengi kutoka kwake; kuanzia kazi zake hadi jinsi alivyoishi na watu.

Kama ilivyoelezwa, alikuwa mtunzi, muigizaji, mwandishi wa mswada, hizi si kazi zinazohitaji kuwa na ujuzi na kipaji pekee, bali kujituma, kutokata tamaa na kuwa tayari kukosolewa. Kazi nyingi za Mzee Majuto au King Majuto kama mashabiki wake walivyokuwa wakimtambua, zitaendelea kuishi kutokana na sifa hizo, hivyo ni wajibu wa kila msanii kujipima kama naye kazi zake zinatoa mafunzo kwa jamii na kama zitaendelea kudumu hata atakapomaliza safari yake hapa duniani.

Aidha, kama tulivyoeleza, licha ya umaarufu aliokuwa nao Mzee Majuto hakuwa na makuu, hayo ndiyo maisha ambayo wasanii wote wanapaswa kuyaishi.

Kuna kauli maarufu isemayo, msanii ni kioo cha jamii, hakuna shaka kwamba Mzee Majuto alikuwa kioo cha jamii. Swali linabaki kwetu na hususan wasanii waliochwa kama nao wanastahili kwa kazi zao na vitendo vyao?