http://www.swahilihub.com/image/view/-/4797888/medRes/2037625/-/dd4c51/-/lugola.jpg

 

Malezi bora yatasaidia kukomesha udhalilishaji

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Tuesday, October 9  2018 at  09:55

Kwa Muhtasari

Wanafunzi 19 wa shule za sekondari za Boma na Hai Day walifanyiwa vitendo viovu vya ulawiti

 

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ameagiza ufanyike uchunguzi nchi nzima ili kubaini idadi ya wanafunzi wa shule za sekondari waliofanyiwa vitendo vya kifedhuli na udhalilishaji ikiwemo kulawitiwa. Waziri amechukua hatua hiyo baada ya kufichuka habari wiki iliyopita kwamba wanafunzi 19 wa shule za sekondari za Boma na Hai Day walifanyiwa vitendo viovu vya ulawiti na makundi mbalimbali ya jamii.

Kwa mujibu wa mmoja wa wanafunzi waliodhalilishwa kingono kutoka shule hizo, makundi ya waendesha pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda, madereva wa pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) na wauza santuri au CD ndio wamekubuhu.

Ndiyo maana, Waziri Lugola mwenye dhamana ya kusimamia usalama wa kila mtu nchini alimpa agizo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuwaagiza makamanda wa polisi wa mikoa (RPC) wafungue majalada ya uchunguzi katika shule zote nchini ili kila mwanafunzi aliyefanyiwa vitendo hivyo awe wa shule ya msingi au sekondari ajipeleke mwenyewe kituoni kufanyiwa uchunguzi.

Tunampongeza na kumuunga mkono waziri huyo kwa juhudi anazochukua sasa kulinda si tu usalama wa watu na mali zao, bali afya na utu wa kila mmoja. Vilevile tunampongeza kwa kuwazindua maofisa wa polisi kwamba wasisubiri tu kupelekewa matatizo, bali wazunguke na kuyadhibiti matukio ya uhalifu kabla hayajatokea.

Hata hivyo tunapenda kuikumbusha jamii isijisahau katika malezi na kufichua maovu. Kwamba, wajibu wa kudhibiti ubakaji, ulawiti na utekaji wa watoto unapaswa kuwa wa jamii nzima na si polisi pekee.

Tabia ya watu kudhani “hilo halinihusu” au anayefanyiwa ukatili “si mtoto wangu” au “si kazi yangu kufichua wahalifu” ndiyo imetufikisha hapa. Ikiwa jamii haitabadili tabia, haitataka kushiriki kudhibiti na kuwafichua wahalifu ili wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwafumbia macho wabakaji na wadhalilishaji baada ya kupewa rushwa kutasababisha maovu haya kuzidi kuongezeka.

Pengine tungeikumbusha jamii kwamba wanahabari waliwahi kutoa mchango mkubwa kuanzia miaka ya 1990 pale Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) kilipofanya kampeni nchi nzima kuielimisha jamii namna ya kukabiliana na janga la ubakaji na ulawiti lililokuwa likiota mizizi.

Maofisa wa Tamwa, wakiwa hawana nguvu za kisheria bali nguvu ya ushawishi walifanya mikutano mbalimbali na baadaye walifanikiwa kuwaeleza waheshimiwa wabunge kuhusu ukubwa na madhara ya tatizo hilo kwa waathiriwa ambao ni wanawake, wasichana na hata wavulana. Matunda ya kampeni ile, mwaka 1998 ilitungwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ikifikiriwa kwamba ulipatikana mwarobaini wa tatizo hilo kwani wote waliokamatwa, kushtakiwa na kupatikana na hatia walifungwa jela vifungo vya muda mrefu na baadhi yao vya hadi maisha.

Tunaikumbusha jamii kwamba ili sheria iweze kufanya kazi inahitaji ushirikiano wa dhati na wanaopata taarifa za uhalifu wazipeleke polisi ili wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua.

Zipo taarifa kwamba baadhi ya ndugu wa karibu ni miongoni mwa wahusika wa vitendo vya ubakaji na ulawiti, na ndiyo maana watoto wakifanyiwa ukatili nyumbani au barabarani huwa vigumu kuripoti na wakiripoti wahusika hawachukuliwi hatua. Tunawasihi wazazi kuwa karibu na watoto wao ili waweze kuwaambia yaliyo mioyoni mwao kabla hawajaathirika zaidi na wahalifu waripotiwe na kuchukuliwa hatua bila kukawia.