http://www.swahilihub.com/image/view/-/4930236/medRes/2220951/-/mop7ua/-/richard.jpg

 

Mali za abiria viwanja vya ndege ziwe kipaumbele

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  10:03

Kwa Muhtasari

Kuwepo mikakati itakayodhibiti kutokea kwa vitendo vya wizi

 

 

Kwa hulka ya Watanzania hasa wanapokuwa katika mjumuiko mkubwa, mathalani katika sherehe, burudani na hata mikutano, si rahisi kuona wengi wakijitokeza iwe kuanza kucheza au kuuliza maswali.

Lakini mmoja akianza, huongezeka na mwishowe wanaweza kufikia hata kugombea kupata fursa hiyo.

Hivyo, ikiwa mshereheshaji au mtoa burudani atafadhaishwa na mwitikio mdogo wa dakika chache za mwanzo, anaweza ama kuahirikisha shughuli au kubadili ratiba akidhani kwamba wengi hawajahamasika.

Ndivyo wengi walivyo. Hawapendi kujitokeza kupiga kelele kwa mambo mengi ambayo hawakubaliani nayo, lakini inapotokea mmoja wao ameamua kusema hapo utaona idadi kubwa ikijitokeza, kila mmoja akitoa ushuhuda wake wa madhila yaliyomfika kwa tukio linalofanana na hilo.

Mfano malalamiko ya baadhi ya watumiaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ambao wamedai kuwapo kwa tabia ya wizi wa mali za abiria kwenye mizigo wanapopita uwanjani hapo.

Walitoa madai hayo baada ya andiko la msanii nyota wa filamu nchini, Vincent Kigosi “Ray” kuandika kwenye akaunti yake ya Instagram (raythegreatest), akidai kuibiwa vitu mbalimbali kama viatu katika begi lake wakati akielekea Dubai.

Nyota huyo wa filamu anahoji sababu za uongozi wa uwanja huo kutowachukulia hatua kali wafanyakazi wenye tabia ya udokozi kwa kuwa wanaharibu sifa ya uwanja huo muhimu.

Baada ya kauli hiyo, baadhi ya wananchi nao wanaofuatilia ukurasa huo walianza kutoa madai yanayofanana na hayo kila mmoja akieleza namna alivyopoteza mali zake uwanjani hapo.

Baadhi ya waliosoma mikasa ambayo wenzao walidai kuipata uwanjani hapo, waliwashauri waliopoteza mali zao kutoa taarifa sehemu husika badala ya kutumia mitandao ya kijamii, ili tatizo hilo lishughulikiwe kwani uwanja huo una kamera za ulinzi.

Kauli inayofanana na hiyo ilitolewa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela ambaye alishangaa kitendo cha mtu anayeibiwa nyumbani kwake kukimbilia au kulalamika kwenye mitandao ya kijamii.

Mayongela anashauri wanaoibiwa waripoti kwenye vyombo vya dola ili hatua zichukuliwe na akaahidi kuwa matukio hayo yatachunguzwa na ikibainika ukweli wahusika watawajibishwa.

Nasi tunaunga mkono kauli ya mkurugenzi huyo wa TAA ya kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika na tukio hilo na mengine yanayopaka picha mbaya kwenye uwanja huo.

Ingawa ametoa malalamiko kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu husika kufikisha kilio chake, tunadhani kwamba kasoro hiyo haiwezi kuzuia kufanyika kwa uchunguzi wa kubaini kama vitendo hivyo vipo na kisha kuchukua hatua kali ili uwanja huo uendelee kuwa sehemu salama kwa kila anayeutumia. Cha muhimu zaidi ni kuweka mikakati itakayodhibiti kutokea kwa vitendo hivyo ili kufanya eneo hilo liwe salama, hasa wakati huu ambao Serikali inafanya jitihada kuhakikisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linaimarika na kuwa na uwezo wa kuleta wageni wengi ambao wanahitaji kuwa na uhakika wa usalama wa mali zao.