http://www.swahilihub.com/image/view/-/5015238/medRes/2274065/-/r23ler/-/hadhi+pic.jpg

 

Mambo haya yanashusha hadhi yako mwanamke

 

Na Jackline Masinde

Imepakiwa - Friday, March 8  2019 at  12:26

 

 Leo ni Siku ya Wanawake Duniani ambayo kihistoria siku hii inalenga kumuonyesha mwanamke upendo na heshima kutokana na mafanikio yake ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Siku hii pia inalenga kutoa hamasa kwa wanawake kutojiona viumbe dhaifu, bali wenye uwezo katika kuleta maendeleo ndani ya jamii zao na Taifa kwa jumla.

Pamoja na heshima hii ambayo dunia imetupatia, ni wakati sasa wa wanawake tujitafakari. Je, tunaitendea haki heshima na upendo huu?

Waswahili wanasema ukiheshimiwa, basi nawe heshimika. Ukishikwa basi shikika. Licha ya kuwapo kwa wanawake wanaofanya mambo mazuri na tena ya kuigwa ndani ya jamii, lakini bado kumekuwapo na mambo mabaya yanayofanywa na wanawake walezi wa vizazi vya Taifa la leo na kesho.

Mambo haya yanashusha hadhi na heshima ya mwanamke kiasi kwamba hata wanaume wanatucheka na kuendelea kutudharau wakituona kuwa kama ni viumbe visivyojitambua.

Miongoni mwa mambo yanayoshusha hadhi ya mwanamke bila kujua ni haya ninayoyasimulia katika mkasa huu.

Siku moja nilikuwa barabarani nikitembea. Nikakutana na kundi la wanaume, mara ghafla akapita mwanamke akiwa ameweka nywele za bandia kichwani, amebandika kope bandia kwenye macho, kucha ndefu, amevaa nguo fupi zinazoonyesha sehemu ya mwili wake uliojaa michirizi iliyosababishwa na vipodozi vikali.

Mmoja wa wanaume akashika kichwa kama anashtuka na kusikika akisema “jamani hawa wanawake sijui nani amewaroga”.

Mwanamume mwingine pia alidakia akisema “aliyewaroga amekufa.” Mwingine akasema “tatizo la dada zetu huwa hawajiamini kabisa na madhara yake ndio haya tunayoyaona.”

Hakika niliona aibu hata kukatiza mbele ya wanaume hao ambao waliishia kumzomea mwanamke huyo.

Kiukweli mavazi na mwonekano wake bado havikumtambulisha kama mwanamke anayetakiwa kupewa heshima na upendo, bali anayetakiwa kudharauliwa, kutukanwa na kuzomewa kwa kuwa hakuwa na staha hata kidogo.

Siku nyingine tena niliingia katika moja ya ofisi ya mkurugenzi wa taasisi moja kufuatilia jambo muhimu ikiwa ni sehemu ya majukumu yangu.

Mkurugenzi huyo alinikaribisha akisema “hongera sana binti yangu.” Nilimuuliza “hongera ya nini?” akanijibu akisema “kwenye ofisi yangu huwa siongei na watu bandia. Wewe siyo bandia ni ‘original’ ndio maana nakupa hongera.”

Akasema “ninaamini ninaongea na mtu anayejitambua na kujielewa. Sasa niulize maswali yako yote nitakujibu.”

Mkurugenzi huyo alisema hayo akimaanisha huwa hapendi kuzungumza mambo muhimu na wanawake wanaojichubua na kuvaa nusu uchi kwa madai kuwa uwezo wao wa kufikiri ni mdogo.

Ni kweli kwamba hakuna mtu anayemkataza mwanamke kujipamba na kujiweka vizuri kimwonekano, maana hata vitabu vya dini vinaruhusu mwanamke ajipambe kwa mapambo ya kupendeza, lakini isiwe kwa kubadilisha kabisa uhalisia wa ngozi na mwili wake na kupita kiasi

Wanawake wa leo wamekuwa wa ajabu machoni mwa jamii na kila ninapotembea barabarani siishiwi kuona vituko vya wanawake wenzangu wakiwa wamevaa vitu vya ajabu na wakifanya mambo ya aibu ikiwamo ‘kuvaa’ makalio ya bandia. Kiukweli mnaofanya hivi mnatia aibu kama sio kinyaa.

Pengine niwaambie leo wanawake wenzangu kuwa, utamaduni huu wa kubadili uhalisia unatushushia hadhi na kutunyima fursa za kiutawala katika nyanja mbalimbali na ndio wanaume wanaendelea kutudharau na kutushusha hadhi.

Wananchi wanaojitambua hawawezi kumchangua mwanamke kuwa mbunge au kiongozi wao wakati mwenyewe hajikubali na kujiamini kwa namna alivyo.

Nimewahi kuambiwa na mkufunzi wangu mmoja katika mafunzo ya uongozi kwa wanahabari wanawake kuwa, kiongozi ni mtu mwenye uwezo wa kujitambua, kujiamini, kujitathimini, kujiongoza na kuongoza wengine.

Huwezi kuwa kiongozi bora kama wewe mwenyewe huwezi kujiongoza, kujitambua, kujiamini na kuongoza. Kitendo cha kubadili mwonekano wako kinakuondolea hadhi iliyotukuka kwenye nafasi ya kuwa kiongozi wa familia, Taifa na watoto wako.

Kwa sababu hiyo basi binafsi natarajiwa kumuona mwanamke mwenye sifa hizo na si yule anayejichubua na kubadili mwonekano wake wa asili wakati anajua kufanya hivyo ni kujipatia madhara makubwa kiafya.

Wewe tutakuita ni kipofu usiyeona na huna sifa za kuitwa mwanamke ambaye leo dunia inamsherehekea kwa upendo na heshima kubwa.

Wanaume wamenituma niwaambie haya leo; hawapendi tunavyojibadili mwonekano wetu kwa kuvaa vitu bandia, tupambeni lakini tubaki na uasilia wetu.

Jackline Masinde ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi anapatikana kwa namba 0716-471604