http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928924/medRes/1506903/-/7b80gqz/-/kairuki.jpg

 

Mambo manne yaliyomponza Kairuki wizara ya madini

Angellah Kairuki, aliyekuwa Waziri wa Madini. Sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji)   

Na Elizabeth Edward, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  11:56

Kwa Muhtasari

Kushindwa kuwajibika ipasavyo, hali inayosababisha nchi kupoteza fedha nyingi

 

eedward@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Sasa ni dhahiri kwamba, Angellah Kairuki aliondolewa katika Wizara ya Madini baada ya Rais John Magufuli kutaja mambo manne aliyoeleza kuwa yalikuwa ni udhaifu katika wizara hiyo.

Mambo hayo ni pamoja na takwimu kuonyesha kwamba licha ya Tanzania kuongoza kwa uchimbaji wa dhahabu Afrika Mashariki haiongozi miongoni mwa nchi zinazouza madini hayo.

Nyingine ni kutokuwapo kwa vituo vya madini kwa ajili ya uratibu, kutofahamu dhahabu zinapouzwa, Taifa linaingiza kiasi gani kutokana na biashara hiyo na pia kukosekana kwa kanuni.

“Tumewaruhusu wawekezaji na wachimbaji wadogo wachimbe dhahabu. Je, Wizara ya Madini mmeshajiuliza dhahabu inayochimbwa inauzwa wapi? Na je, kama wanachimba na wanauza sisi tunapata asilimia ngapi? Hili suala ni la Wizara ya Madini, halikuwa suala la Bunge kujiuliza, wala halikuwa suala la Waziri Mkuu au Rais kujiuliza.

“Kwenye Sheria ya Madini nina hakika kuna mahali imeelekeza kuanzishwa kwa vituo vya kuuzia madini. Je, vimeanzishwa vituo vingapi? viko wapi? Kwa sababu vingeanzishwa vituo hivi tungejua dhahabu inayosafirishwa, wapi imeuzwa na inawezekana tungekuwa na taarifa za kila wiki, lakini hakuna,” alisema Rais Mafufuli jana baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua juzi.

Katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya juzi, alimwondoa Kairuki Madini na sasa anakuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa naibu wake, Dotto Biteko.

Rais Magufuli alisema kuna changamoto katika maeneo kadhaa yakiwamo ya sekta ya madini ambazo zinatokana na uongozi wa wizara hiyo kushindwa kuwajibika ipasavyo, hali inayosababisha nchi kupoteza fedha nyingi.

“Nitaendelea kufanya mabadiliko kila mahali nitakapoona sijaridhishwa, mhusika ataondoka. Hata Biteko nimekuteua nikiona mambo hayaendi ninavyotaka utaondoka,” alisema.

Biteko aliteuliwa Januari 8, mwaka jana kuwa naibu waziri katika wizara hiyo na juzi Januari 8 ikiwa ni mwaka mmoja kamili, alipandishwa na kuwa waziri wa pili kushika wadhifa huo tangu ilipoundwa kutoka wizara ya Nishati na Madini.

Rais Magufuli alisema amemteua Biteko kutokana na utendaji kazi wake na jinsi alivyokuwa na mawazo chanya kwenye sekta hiyo tangu akiwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Madini.

“Niliona Biteko alivyokuwa anaichachafya Serikali na kutoa michango mizito kwenye sekta ya madini. Alipochaguliwa kwenye kamati ya uchunguzi wa madini, ndipo nikaona ipo haja ya kumuingiza serikalini ili atusaidie na kweli amefanya kazi kubwa nimeona awe waziri kamili.”

Alimwagiza Biteko kuanza na uanzishaji wa vituo vya madini vitakavyokuwa na jukumu la kuratibu dhahabu na kushirikiana na Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuanza kununua dhahabu.

“Hivyo vituo ndiyo vitakuwa daftari letu la kujua ni kiasi gani cha dhahabu kinauzwa nje. Wanaouza nje wawe kwenye rekodi, bora tuwe na dhahabu nyingi tumehifadhi pale Benki Kuu itatusaidia hata uchumi ukiyumba.

Pia alitoa wito, “Tume ya Madini ikafanye kazi siyo kuishia kutoa leseni tu, au mnataka mpaka siku moja nijichague mwenyewe kuwa waziri wa madini ndiyo mambo yataenda?” alisema na kuwafanya viongozi waliohudhuria hafla hiyo kucheka.

Aliwataka watendaji wa Serikali kutohofia kufanya uamuzi ambao utakuwa na tija kwa nchi.

“Ni heri ufanye maamuzi kwa nia njema halafu yawe mabaya, kuliko kutofanya maamuzi kabisa.”

Rais Magufuli pia alizungumzia kukamatwa kwa shehena ya dhahabu huko Mwanza hivi karibuni akisema, “Inauma unapoona kilo zaidi ya 300 zenye thamani ya zaidi ya bilioni 30 zinakamatwa zikisafirishwa. Wameshaiona Tanzania ni nchi ambayo unaweza kufanya lolote.”

Alimpongeza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kwa jinsi alivyoshughulia suala hilo.