Mambo ya kuzingatia unapopata ajira mpya

Na Christian Bwaya

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  16:47

Kwa Muhtasari

Pata dondoo kubwa mbili zinazoweza kukuongoza katika mafanikio hasa unapoanza kazi katika ofisi mpya

 

Nidhamu ya kazi

Ufanisi katika kazi, kwa kiasi kikubwa, unategemea nidhamu. Namna gani wewe kama mwajiriwa mpya unaheshimu kazi yako kwa kuwahi kazini, kuwasilisha mrejesho wa kazi kwa muda uliopangwa. Hiyo ndiyo inaitwa nidhamu ya kazi.

Hakikisha unawahi kazini mapema. Kama ofisi ina utaratibu wa kusaini kitabu cha mahudhurio, usiache kusaini ndani ya muda uliopangwa. Usiwe mtu wa kukosa vikao vinavyoitishwa kazini. Unapokosekana kwenye vikao, ni rahisi kuonekana huna nidhamu ya kazi inayotakiwa.

Pia, nidhamu ya kazi ni pamoja mpangilio mzuri wa jumla wa majukumu yako ya kila siku. Huwezi kupangilia majukumu yako kama huwezi kutunza muda wako vizuri.

Tumia kitabu cha kumbukumbu za kila siku kuainisha majukumu unayotakiwa kuyakamilisha kila siku. Unapofanya hivyo, utaweza kupima utendaji wako na hivyo kukamilisha na kukabidhi ripoti zako kwa muda unaotarajiwa.

Heshimu utamaduni wa taasisi

Kila eneo la kazi lina utamaduni wake. Huu ni utaratibu usio rasmi uliozoeleka katika taasisi ambao kila mmoja anajikuta akiufuata ingawa haujaandikwa kokote.

Unawajibika kudadisi na kujua taasisi yako inaongozwa na utamaduni upi. Kwa mfano, kuna taasisi zisizoruhusu mavazi ya namna fulani kuvaliwa kazini. Kuwa mwepesi kujifunza mambo kama hayo.

Kila taasisi inaongozwa na ‘siasa’ zake za ndani na nje. ‘Siasa’ ni taratibu zisizo rasmi zinazoongoza uhusiano baina ya wafanyakazi ndani ya taasisi na namna taasisi inavyojenga taswira yake katika jamii. Unalazimika kufanya kazi ya ziada kuzielewa.