http://www.swahilihub.com/image/view/-/4800894/medRes/2137242/-/juiby4/-/mari.jpg

 

Mambo yanayokwaza maendeleo ya elimu Zanzibar yadhibitiwe

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis  

Na Kulwa Magwa

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  09:43

Kwa Muhtasari

Kumekuwa na ongezeko la walimu wanaokwenda harusini saa za kazi huku wanafunzi wakiwa darasani bila walimu

 

Walimu katika Mkoa wa Kaskazini Pemba wapigwa marufuku kuhudhuria sherehe za harusi muda wa kazi, badala yake wazingatie masomo ili kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne na sita.

Agizo hilo lililotolewa na mkuu wa mkoa huo, Omar Khamis limekuja baada ya hivi karibuni kudaiwa kuwapo kwa ongezeko la walimu wanaokwenda harusini saa za kazi huku wakiwaacha wanafunzi wakiwa darasani bila watu wa kuwafundisha.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa jambo hilo ni kinyume na sheria ya utumishi wa umma kwa sababu inazuia mtumishi wa Serikali kufanya kazi nyingine nje ya ile aliyoajiriwa kwayo katika muda wa kazi.

Kabla ya kutoa agizo hilo, Omar alifanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Mjananza Wete kuangalia mafanikio na changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema, “ni marufuku mwalimu kwenda harusini saa za kazi, kama ni harusi waende baada ya saa za kazi.” Kisha aliwataka walimu wakuu kutotoa ruhusa za aina hii.

Licha ya kuchelewa kutolewa kwa agizo hilo tunaliunga mkono kwa sababu linalenga kuinua kiwango cha ufaulu na kuboresha sekta ya elimu katika mkoa huo ikizingatiwa kwamba Zanzibar haipati matokeo mazuri sana katika elimu ya sekondari kitaifa.

Tunajua kwamba kilio kikubwa cha shule nyingi ni uhaba wa walimu, hivyo kuwapo walimu wanaokwenda harusini saa za kazi kunachangia wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma kwa sababu wanakosa msaada kutoka kwa walimu hao katika muda huo.

Aidha, katika kuunga mkono agizo la mkuu huyo wa mkoa tunaiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iangalie utaratibu wa kupiga marufuku shughuli zote binafsi ikiwamo harusi zisiingiliane na zile za kiserikali au zisiathiri zile za Serikali.

Tunaamini kwamba hili likiwa ni agizo kwa kila mkoa visiwani humo litasaidia kuchochea zaidi maendeleo ya wananchi pamoja na kuinua sekta ambazo ziko nyuma kwa sasa ikiwamo elimu na afya.

Kama Taifa, hatuwezi kupiga hatua kubwa ya maendeleo iwapo mambo kama haya yataachwa yaendelee bila kuwekewa msimamo mkali wa kisera au kutungiwa sheria ili kila mwananchi atimize wajibu wake kwa Taifa.

Kwa upande wa wazazi, ni vyema wabadilike na kuitumia kila fursa wanayoiona mbele yao katika kuhakikisha kuwa kiwango cha elimu visiwani humo kinapanda, badala ya wao kuwa sehemu ya kukwamisha mafanikio.

Zipo taarifa zinazodai kuwa baadhi ya wazazi hawana mwamko wa elimu kwa watoto wao hususan wa kike, jambo linalosababisha wawakatishe masomo na kuwalazimisha kuolewa. Hili kamwe lisipewe nafasi katika jamii.

Mathalan zipo taarifa kwamba wanafunzi watatu wa darasa la sita wenye umri wa miaka 14 walitaka kuolewa katika Shule ya Msingi Mjananza Wete, lakini Serikali iliingilia kati na kufanikiwa kuwarejesha shule wawili ambao na kwa sasa wanaendelea na masomo.

Haiwezekani mwanafunzi aamue kuacha masomo na kutaka kuolewa bila wazazi kuwa na mchango katika suala hilo. Ndiyo maana tunawaona wazazi kuwa na mchango tofauti katika kufanikisha malengo ya mtoto na elimu kwa jumla, hivyo ni vyema wakaendelea kutekeleza wajibu wa malezi ipasavyo.