http://www.swahilihub.com/image/view/-/4958050/medRes/2237702/-/qcfrtl/-/ukiki.jpg

 

Manolo ajisuka upya baada ya Recapp kuvunjika

Manolo

Emmanuel Mwongela maarufu Manolo. Picha/PAULINE ONGAJI 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  11:32

Kwa Muhtasari

Msanii Emmanuel Mwongela maarufu Manolo anaendelea kujisuka upya.

 

TAKRIBANI miaka miwili baada ya Recapp kuvunjika, mmojawapo wa wanachama waliojumuisha kikundi hiki cha injili ameanza kujiundia jina kama mwanamuziki binafsi.

Sio mwingine ila ni Emmanuel Mwongela maarufu Manolo, aliyekuwa muimbaji mkuu wa kikundi hiki, ambapo ustawi wake ulidhihirika akiwa katika kikundi hiki ambapo pamoja walijivunia albamu mbili huku wakitwaa tuzo mbali mbali ikiwa ni pamoja na nane za Groove Awards.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio mwaka 2018, alisema kwamba 2019 utakuwa mwaka wa ufanisi kwake, na tayari ameanza kuonyesha ishara hii kwani wiki chache tu tangu mwanzo wa mwaka, tayari amewapa mashabiki sababu ya kutabasamu.

Juzi alizindua kibao chake kipya, Mwingine, wimbo uliotanguliwa na kibao chake cha kwanza, One by One, alichoangusha mwaka 2018.

Je unakumbwa na woga wa kushindana na maafikio ya kikundi hiki?

MANOLO: Bila shaka kuna shinikizo kwa sababu tumeshuhudia baadhi ya wanamuziki wakishindwa kujiendeleza kimuziki baada ya kikundi walichokuwemo kuvunjika.

Ulijitosa katika muziki mwaka wa 2012 kama kiongozi muimbaji wa Recapp. Hii inamanisha kwamba sehemu kubwa ya safari yako kama mwanamuziki imekuwa kupitia kikundi hiki. Unajiundia vipi kitambulisho kama Manolo?

MANOLO: Mara nyingi mojawapo ya sababu zinazowafanya wasanii kushindwa kutamba baadaye ni kubadilisha kitambulisho chao. Kwa mfano iwapo ulikuwa mwanarepa, sasa unakuwa mwanamuziki, au unabadilisha mtindo wa muziki kabisa. Kuna wale ambao hata hubadili mitindo ya mavazi au hata rangi ya nywele. Matokeo ni mwanamuziki tofauti kabisa, ambapo inakuwa ngumu kumtambulisha tena kwa mashabiki. Kwa upande wangu nitasalia kuwa Manolo aliyekuwa kwenye Recapp. Mtindo ni ule ule.

Wimbo One by one unazungumzia jinsi unaweza jitegemea na kushamiri kimuziki pasipo kuwepo katika kikundi hiki, suala ambalo linaibua wazo kwamba huenda hamkutengana kwa uzuri. Ni kweli?

MANOLO: Siwezi pinga kwamba mwanzoni tulikuwa na msukumano, lakini ulitokana na wasi wasi wa iwapo uamuzi wetu ulikuwa wa busara. Mbali na hayo uhusiano wetu ni mzuri. Sote katika kikundi hiki tulitaka kujiimarisha na kufuata mikondo mipya katika taaluma zetu. Ujumbe wa kibao hiki ulielekezewa baadhi ya watu walioingiwa na shaka kuhusu iwapo nitang’aa kama mwanamuziki binafsi, sawa na ilivyokuwa kama mwanachama wa kikundi hiki. Kwa ufupi nilikuwa nawaambia kwamba mambo ni shwari.

Baada ya kikundi hiki kuvunjika, ilikuchukua muda kabla ya safari yako kama msanii binafsi kung’oa nanga. Yawezekana ulikuwa unasubiri kwa matumaini ya kuwa huenda kikundi hiki kikarejea pamoja?

MANOLO: La hasha! Sababu yangu ya kutulia ilikuwa kuweka mawazo pamoja na kukabiliana na changamoto tulizokumbana nazo kama kikundi, kabla ya kujitosa kama mwanamuziki binafsi.

Changamoto? Changamoto zipi hizi?

MANOLO: Changamoto zilikuwa nyingi, kama vile malipo duni kutoka kwa waandalizi wa shoo, na kutokuwa na uthabiti wa kurekodi muziki. Wasanii wanaochipuka hukumbana na tatizo la malipo ambapo baadhi ya hawa waandalizi huwakandamiza kwa kudai kwamba wanawapa mwangaza badala ya malipo. Pia katika kikundi hicho tulikuwa na tatizo la kuwa thabiti inapowadia wakati wa kuzindua muziki, ambapo tungerekodi wimbo mmoja au mbili, suala lililokuwa likiturudisha nyuma. Sikutaka kushuhudia hayo tena.

Kwa hivyo nini unafanya tofauti?

MANOLO: Sasa nina usimamizi thabiti unaoshughulikia masuala ya majadiliano ya malipo. Pia, kwa sasa narekodi muziki kila mara, badala ya kurekodi tu wakati ninapotaka kuzindua nwimbo. Hii inafanya iwe rahisi wakati wa kurekodi video. Pia nimezingirwa na watu walio na umuhimu sana na tunakua sote pamoja hata ninavyoendelea kukuza kitambulisho changu.