Mapambano ya kusaka mshindi hayatupa sheria bora

Imepakiwa - Wednesday, April 3  2019 at  08:25

 

Miongoni mwa malengo ya kutungwa kwa sheria ni kuboresha sekta husika na kukabiliana na changamoto zinazoiathiri.

Ndio maana katika mchakato huo maoni ya wadau huzingatiwa kwa kuwa sheria inawahusu wadau husika.

Hata hivyo, kumekuwapo na changamoto katika utungwaji wa sheria kadhaa hapa nchini kutokana na kutokuwa na uelewa unaofanana baina ya watunzi wa sheria na wadau.

Jambo hili linachangiwa na sababu kadhaa ikiwamo kutoaminiana kwa pande zote, ushiriki hafifu wa wadau na kukosekana kwa maridhiano katika utungwaji wa sheria husika.

Inawezekana kila upande ukawa na hoja nzuri katika sheria husika lakini kutokukaa pamoja kwa pande zote na kuridhiana imekuwa ni tatizo linalosababisha kila kukicha kuongezeka kwa malalamiko juu ya baadhi ya sheria zetu

 Pia kwa bahati mbaya kumekuwapo na tatizo la wadau wa sheria kadhaa kujitenga na kutoa maoni wakati michakato ya sheria inapoanza.

Mara kadhaa kazi ya kudai sheria nzuri inaachwa kwa asasi chache za kiraia kitendo kinachominya uwakilishi wa wadau wenyewe.

Kutokana na hali hiyo mara kadhaa tumeshuhudia sheria zikipita huku wadau husika wakizilalamikia kuwa hazina tija kwa kada husika. Hali hii pia imejitokeza katika Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari iliyopitishwa mwaka 2016 ambako kwa mujibu wa wadau wa habari imekuwa mwiba kwa kada hiyo.

Mapema wiki hii, Mahakama ya Afrika ya Mashariki imetoa uamuzi wa kukubaliana na baadhi ya hoja juu ya mapungufu ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.

Katika kesi ambayo ilifunguliwa na Baraza la Habari (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), Mahakama ya Afrika ya Mashariki imekubali kuna baadhi ya upungufu katika sheria hii.

Miongoni mwa upungufu huo unakinzana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo na mikataba ya haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia kimataifa.

Baadhi ya vifungu hivyo ni vile ambavyo sasa vinafanya makosa ya uandishi wa habari kuwa ya jinai yaani, akiandika habari anayodaiwa kumkashifu mtu, basi atafungwa jela au kulipa faini kuanzia Sh3 milioni au vyote kwa pamoja.

Mwandishi ambaye atatiwa hatiani kwa kuandika habari za uongo au uchochezi atashtakiwa kama kosa la jinai na kulipa fidia au kufungwa.

Jambo hili ni tofauti na taaluma nyingine na makosa ya kitaaluma ambayo hutatuliwa na bodi za wanataaluma na kama bodi zikishindwa ndipo vyombo vingine vinaingilia kati.

Jumla ya vipengele 18 vililalamikiwa na wadau hao na kuiomba mahakama hiyo itamke kwamba vinakiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuilazimisha Serikali kuvifuta kabisa.

Hata hivyo, licha ya mahakama hiyo kukubaliana na hoja hizo na kutoa uamuzi wake, tayari kuna tamko la kukata rufaa kupinga sehemu ya uamuzi huo.

Naamini kwa sasa jambo hili linahitaji maridhiano kuliko kuonyeshana umwamba kwa njia ya mahakama kwani sheria zipo kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote.

Sidhani kama inapaswa kutafutwa mshindi badala yake pande zote zishirikine ili kupata sheria bora.

Naamini kwa mazingira ya sasa yatupaswa kujitenga na malumbano na ni muhimu kwa pande zote kuelewa umuhimu wa shera yenyewe.

Inawezekana kabisa kila upande una dhamira njema, lakini kama nilivyosema awali kutoaminiana kwa pande zote kunaweza kuwa ni sehemu ya tatizo.

Ni ukweli ulio wazi kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinaumiza watu wengi na hata kupoteza maisha yao kutokana na habari za uzushi na uongo, lakini pia kuna ukweli sheria zimekuwa kali sana.

Sheria mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari ina maeneo mengi ambayo ni mazuri kwa mustakabali wa kuboresha tasnia ya habari, lakini yapo machache yenye utata, hivyo bado kuna fursa ya kuifanyia marekebisho zaidi.

Pia sheria hii inapaswa kuzingatia hali halisi ya sasa ya vyombo vya habari hasa vile vya binafsi ambavyo vingi vimedhoofika kutokana na kukosa matangazo na kuwa na hofu katika kutoa habari.

Wito wangu kwa wadau wa sheria hii kuendelea kutafuta maridhiano.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha, anapatikana kwa namba 0754-296503.