Mapendekezo ya CAG yafanyiwe kazi

Imepakiwa - Friday, April 12  2019 at  10:24

 

Nani hajaguswa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyosomwa juzi jijini Dodoma?

Kuanzia vyama vya siasa, mashirika ya umma, vyuo, halmashauri na taasisi nyinginezo za kiserikali; kote huko CAG amebaini kuwapo kwa udhaifu mkubwa wa matumizi ya fedha za umma.

Kifupi hali si shwari nchini, kuna tatizo mahali. Ufisadi, ukiukwaji taratibu za fedha na utendaji mbovu, vimetamalaki kwenye maeneo mengi ndani na nje ya Serikali.

Haya yanatokana na ama uzembe wa kiuwajibikaji au ujanja wa makusudi wa watendaji unaosababisha upotevu mkubwa wa fedha. Na hii si kwa ripoti hii mpya inayoishia Juni 2018.

Ni ada ya kila mwaka ripoti hiyo inapotolewa. Hata hivyo, hatuoni kuwapo kwa dhamira ya dhati ya kuumaliza udhaifu huu unaojitokeza mara kwa mara.

Mathalani inasikitisha kuwa katika ripoti ya mwaka huu, kati ya mapendekezo 350 ambayo ofisi ya CAG ilitaka yafanyiwe kazi, ni mapendekezo 80 pekee yaliyofanyiwa kazi sawa na asilimia 22.9.

Hali ni hivyo hivyo hata miaka ya nyuma. Kwa mfano, mwaka 2017 kati ya mapendekezo ya ukaguzi 3,898 yaliyotolewa, ni mapendekezo 1,449 yaliyotekelezwa kikamilifu. Mapendekezo 1,351 yalikuwa bado katika hatua ya utekelezaji, 842 hayakutekelezwa kabisa na mapendekezo 256 yalipitwa na wakati.

Ni dhahiri kuwa kutofanyiwa kazi mapendekezo hayo ndiyo sababu ya kuwapo kwa udhaifu kama wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kushindwa kukusanya Sh400 bilioni, kuwapo kwa kashfa ya Jeshi la Polisi kununua sare hewa kwa Sh16 bilioni.

Udhaifu mwingine ni halmashauri 47 kushindwa kutekeleza miradi kwa sababu ya kutopelekewa fedha au miradi kukamilika lakini haifanyi kazi. Hii ni baadhi tu ya mifano kati ya mingi ambayo CAG ameitaja katika ripoti yake

Tunapofikiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati, hatuwezi kufika huko kwa ndoto za alinacha bali ni pamoja na kufanyia kazi yale yanayopendekezwa na ripoti za CAG mara kwa mara.

Ni vyema tukakumbusha kuwa ukaguzi wa CAG hufanywa kwa mujibu wa Katiba chini ya Ibara ya 143 (4) pamoja na kifungu cha 34 (1)(c) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 sambamba na kanuni zake za mwaka 2009.

Ni ripoti inayokagua mambo mbalimbali ikiwamo matumizi ya fedha, sheria, mifumo ya ndani na masuala ya utawala wa Serikali Kuu; mafaili ya pensheni, ukaguzi maalumu chini ya Serikali Kuu na ukaguzi wa vyama vya siasa na masuala yaliyobainika katika ukaguzi wa miaka ya nyuma lakini hayakutolewa taarifa zake kwa kipindi husika.

Aidha, inatoa taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi wa miaka ya nyuma na maagizo ya Bunge.

Inahusu utawala bora na unaofuata sheria, uwajibikaji, uwazi, upatikanaji wa huduma na bidhaa za umma, haki na upotevu wa mali ya umma.

Kwa majukumu haya, lazima tukiri kuwa ofisi ya CAG ni roho ya uchumi na uendeshaji wa nchi kwa jumla.

Ni kwa sababu hii, kila anachokibaini kwenda ndivyo sivyo na kukitolea mapendekezo hakina budi kufanyiwa kazi kwa haraka na mamlaka husika.