http://www.swahilihub.com/image/view/-/4564740/medRes/1974923/-/n3lj1mz/-/lijumba.jpg

 

Maragua: Mji wenye mambo mengi

Maragua

Jumba ambalo miaka ya themanini (1980s) lilikuwa benki ya Barclays kabla ya kufungwa baada ya uchumi wa eneo kusambaratika. Picha/ MWANGI MUIRURI 

Na MWANGI MUIRURI na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  06:30

Kwa Muhtasari

Mji wa Maragua uko pembeni mwa barabara kuu ya Kenol kuelekea Murang’a.

 

MARA kwa mara magari ya uchukuzi wa umma hukwepa kuuingia mji wa Maragua kwa kuwa kaunti ya Murang’a hutoza ushuru kwa kila moja yao.

Ukitaka kuufika Mji huu, ukiwa na bahati gari utakalotumia litaingai ndani ya Mji huu, lakini ukiwa na bahati mbaya utashukishiwa katika lango kuu la kituo cha polisi cha Mji huu ambacho kiko kando mwa barabara kisha usafirie bodaboda au uingie kwa miguu ikiwa unaufahamu.

Kutoka Nairobi hadi Maragua, kuna umbali wa kilomita 66 huku kutoka Mombasa hadi Maragua ikiwa ni Kilomita 460.

Kutoka Maragua hadi Nanyuki kuna umbali wa Kilomita 89 na pia kwa ufahamu zaidi, kutoka Maragua hadi Nakuru ni Kilomita 194, hadi Eldoret ni 251, hadi Bungoma ni kilomita 323.

Kutoka Maragua hadi jijini Berlin, Ujerumani kuna umbali wa Kilomita 6,291 na kutoka Maragua hadi London ni umbali wa Kilomita 6,739.

Kutoka Maragua hadi Paris ni Kilomita 6,398 huku hadi Rio de Janairo ikiwa ni umbali wa kilomita 8,961 na kadhalika, hizi zikiwa ni takwimu za Wizara ya Uchukuzi nchini chini ya ufichuzi wa Katibu msaidizi, Francis Mung’athia.     

Ni wenye baa nyingi kwa wanaokunywa pombe.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Murang’a, Naomi Ichami, Mji huu huwa na mkusanyiko wa watu ambapo kwa mchana utapata ukiwa na takriban watu 150,000 na usiku upate kuna watu 100,000.

“Huo ni ukadiriaji wetu wa kiusalama, kumaanisha wengi wa walioko mchana huwa na shughuli zao hasa za kibiashara au kusaka raha, huku wapangaji wakibakia usiku pamoja na wale watalii wa kusaka raha kwa baa na katika maeneo ya mahaba. Ni mji ulio na mkusanyiko wa wasio na ajira na walio katika biashara na ajira pia, hivyo basi kuzua mazingara ya ujambazi,” asema Ichami.

Anasema kuwa Mji huu huwa na taasisi za kiserikali kama maafisa wa utawala wa kimaeneo na maafisa wa polisi sambamba na walio katika ajira ya serikali kama madaktari na wasaidizi wao.

Ni mji ambao haujaendelezwa sana kimaendeleo kwa kuwa barabara zake ni mbovu na pia makazi yamejigawa kwa vipande viwili—makazi ya walio na pesa kama njugu na wale wa kipato cha chini.

“Maeneo yanayoangaziwa kama ya walio na pesa ni kama Milimani karibu na kituo cha polisi cha Maragua na ambapo utapata kuna utulivu kwa kuwa usalama hujiangazia kufuatia maafisa wa polisi kuonekana marea kwa mara wakivuka barabara za eneo hilo huku maeneo kama Boarder, Mathare, Soweto na Rurii yakiorodheka katika maeneo yasiyo na uhakika wa usalama,” asema Ichami.

Katika maeneo hayo ya wakwasi, utapata nyumba nzuri ya makazi ya Sh8,000 kwa mwezi, huku kwa walio wa kawaida wakiipata kwa Sh2,000.

Katika maeneo ya kipato cha chini, kodi ni kati ya Sh100 na Sh250 na maeneo hayo ndiyo unashauriwa uzingatie usalama wako ukiyatembelea.

Mitaro

Ni mji ambao hauna mitaro ya maji taka na kwa wakati, mji huo hugeuka kuwa bahari kubwa na maji taka katika msimu wa mvua.

Ujambazi ambao huripotiwa kwa wingi ni ubakaji, uvamizi wa majeruhi na pia mauti, utekaji nyara na wizi wa pikipiki.

Bi Ichami anasema kuwa wale ambao hutumia bhangi mtaani humo huishia kutekeleza kila aina ya ujambazi dhidi ya jamii “ukiwemo ule wa ubakaji, mauaji na wizi”.

Miaka ya 1980 mji huu ulikuwa na kila dalili ya kuinuka kiuchumi lakini ukafifia kutokana na sera mbovu za kiutawala katika serikali ya Daniel Moi.

“Ni mji ambao ulikuwa na kituo cha gari moshi la kutoka Nairobi hadi Nanyuki na kahawa ikiwa na utajiri wakati huo. Lakini kuanguka kwa miradi hiyo miwili ikaishia kuzua umasikini mkuu, watoto wengi wakageuzwa kulewa ndani ya biashara ya chang’aa na bhangi na matokeo yakawa ni hali ya sasa,” asema aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Elias Mbau.

Ni mji ambao unategemea pakubwa kuzinduliwa kwa viwanda ili wenyeji wapate ajira, wawekezaji wavutiwe ili waimarishe miundo mbinu ya sekta ya ujenzi na pia serikali ya Kaunti hiyo izingatie kuimarisha barabara za mjini nayo idara ya polisi ikihitajika kujikakamua kudumisha usalama wa kila mtu.