http://www.swahilihub.com/image/view/-/4097032/medRes/1753187/-/s8y8knz/-/pacha.jpg

 

Maria na Consolata wametuachia funzo kubwa

Maria na Consolata

Hawa ni Maria na Consolata; pacha walioungana katika picha hii baada ya kukamilisha masomo ya kidato cha sita. Picha/HISANI  

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, June 8  2018 at  08:39

Kwa Muhtasari

Juzi tuliwasindikiza katika safari yao ya mwisho pacha walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti baada ya kuishi duniani kwa miaka 21.

 

PACHA hao waliokuwa yatima walilelewa na Shirika la Masista la Maria Consolata, walifariki dunia Juni 2 na kuzikwa katika makaburi ya masista, Tosamaganga mkoani Iringa.

Maisha ya pacha hao kwa jumla yameelezwa kwa namna mbalimbali lakini kubwa ni aina ya mafunzo ambayo jamii imeyapata, hasa kwa kuwa walikuwa mfano bora wa kutokata tamaa.

Pamoja na changamoto za kimaumbile walizokuwa nazo na baadaye zile za kiafya, Maria na Consolata waliendelea kuwa na furaha, kujiamini na kupambana kuelekea ndoto yao ya kupata elimu.

Mabinti hao walikuwa wamelenga kuisaidia jamii wakiwa walimu.

Pamoja na kuwa ari kama hiyo hujengwa na aina ya malezi apatayo mtu, jambo linalosisitizwa na mkuu wa Shirika la Masista la Maria Consolata, Jane Nugi, pacha hao pia wenyewe walitia nia na juhudi binafsi kufanikisha jambo hilo.

Ujumbe wa Nugi kuwa pacha hao wamepitia katika mikono ya watu wengi waliochangia ndoto zao kufikiwa, pia ni funzo kwa jamii na Watanzania kwa jumla, kujenga utamaduni wa kuwapenda na kuwasaidia watu wenye ulemavu kadri tuwezavyo.

Hii ni pamoja na kutowaficha na kuhakikisha wanapata huduma muhimu na elimu ili waweze kufikia matarajio yao. Hata hatua ya shirika hilo kuwachukua na kuwalea baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa wadogo ni mfano wa mafunzo tunayopaswa kujifunza.

Pengine mtu anaweza kusema kuwa Maria na Consolata wamekuwa hivyo – yaani wenye upendo na waliojaa tabasamu usoni na moyoni, kwa sababu tu ya kulelewa kwenye misingi ya kumcha Mungu, kujiamini na kuona kuwa hakuna kigumu mbele yao – lakini hilo pekee halitoshi.

Sisi tunaamini kuwa hata juhudi binafsi walizoweka, kujitambua na kujikubali jinsi walivyokuwa pia ilikuwa silaha yao katika kufikia maisha na elimu waliyokuwa nayo mabinti hao.

Ni kutokana na hali hiyo, ndiyo maana tunakubaliana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kuwa Watanzania wanapaswa kuwaenzi pacha hao kwa kujituma kwao katika kazi na kusaka elimu.

Pacha hao ambao walikuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (Rucu) wakichukua shahada ya elimu, wamedhihirisha kwamba katika maisha hakuna kinachoshindikana.

Jambo hili liko wazi kabisa kwa kuwa watu wengi, wenye ulemavu na hata wengine ambao wana viungo vyote vya miili yao, wanakata tamaa katika kujiendeleza kielimu ama kutokana na uvivu au vikwazo katika hatua mbalimbali. lakini wao walisoma tangu elimu ya awali hadi chuo kikuu.

Katika juhudi na bidii, ingawa ndoto yao haikufika mwisho, pacha hao wamedhihirisha kwamba katika maisha lolote linawezekana pale mtu anapotia nia. Hivi ndivyo Maria na Consolata walikuwa wanapigania elimu bila kujali ulemavu wao.

Kutokana na maisha ya pacha hao, ni wakati wa jamii inatakiwa kuamua kuondokana na tabia ya kuwaona watu wenye ulemavu kama mizigo kwa kuwa hali hii inawafanya wengi kukosa kujiamini.

Badala yake tubadilike tuanze kuwaandalia watu hao mazingira ya kujiamini kwamba wanaweza kujitegemea.

Tuwape nafasi sawa na makundi mengine kwa sababu wote wanastahili kupata huduma na haki katika jamii kwa kuwa ulemavu siyo kulemaa akili na maarifa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647