http://www.swahilihub.com/image/view/-/4389194/medRes/1936458/-/53id0nz/-/heda.jpg

 

Ijue kaunti ya Marsabit

Marsabit

Mwanamke aenda kuchota maji Machi 14, 2018, eneo la Dadacha Dakole, Kaunti ya Marsabit. Uhaba wa maji ni changamoto kuu kwa wakazi wa eneo hilo. Picha/PHOEBE OKALL 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, April 12  2018 at  09:30

Kwa Muhtasari

Wakazi wengi katika Kaunti ya Marsabit ni wa jamii za kuhamahama.

 

MARSABIT ni kaunti inayostawi kibiashara licha ya kwamba eneo kubwa ni jangwa.

Iko Kaskazini mwa Kenya.

Kaskazini mwake, kaunti hiyo imepakana na nchi ya Uhabeshi, Ziwa Turkana likiwa upande wake wa Magharibi, Kaunti ya Samburu upande wa Kusini na Wajir iko upande wake wa Mashariki.

Marsabit ina ukwasi wa milima kadha kama vile; Ol Donyo, mlima wenye urefu wa kimo cha mita 2,066 juu ya usawa wa bahari, Marsabit (1,865), Hurri (1,685), Kulal (2,235), na Sololo-Moyale (1,400).

Kaunti hiyo imeundwa kwa maeneobunge manne; Moyale, Horr Kaskazini, Saku na Laisamis.

Je, ulifahamu kuwa Marsabit ni miongoni mwa kaunti kubwa nchini?

Aidha, ina ukubwa wa kilomita 66.923, na kukadiriwa kuwa na zaidi ya watu 291,166 kwa mujibu wa sensa ya 2009.

Kaunti hiyo ndiyo ya pili ukubwa, ikitanguliwa na jirani yake, Turkana, yenye ukubwa wa kilomita 71,597.8 mraba. Wajir inafuata ya tatu kwa kilomita 55, 840.6 mraba, Garissa (45,720.2) na Tana River (35,375.8) za nne na tano mtawalia.

Marsabit, jangwa la Chalbi ndilo limechukua nafasi kuu ya kaunti hiyo.

Bw Michael Kwena, mtangazaji katika kituo cha Redio Jangwani kilichoko kaunti hiyo anasema shughuli za ufugaji ndizo zimesheheni.

"Wakazi wa huku hufuga ng'ombe, mbuzi na kondoo kwa wingi," Bw Kwena ameeleza mtandao huu na akaongeza kuwa wakazi wengi ni wale wa jamii za kuhamahama.

Marsabit ni kivutio cha watalii kutokana na mbuga ya kitaifa ya Marsabit, Volcano ya Bongole pamoja na Mlima Marsabit.

"Mbuga ya wanyama ya Marsabit hualika watalii kutoka sehemu mbalimbali za taifa na hata kimataifa," aeleza Bw Kwenya.

Chini ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, kaunti hiyo imeonekana kuimarika, huku miradi mbalimbali ikionekana kutekelezwa kama vile uundaji wa barabara za lami.

Mradi

Usambazaji wa nguvu za umeme; hasa unaotoka Loiyangalani, karibu na Ziwa Turkana unatekelezwa Marsabit.

Mradi huo uligharimu Sh70 bilioni, na una jenereta 365 za upepo zinazozalisha wati 850 (kW) kila moja.

Waziri wa Leba Ukur Yattani, wakati akiwa gavana wa kaunti hiyo alisema kuwa mradi huo unaendeshwa kwenye ekari 40,000.

"Kaskazini Mashariki mwa Kenya, hasa Marsabit imekua kiuchumi na tunaona wawekezaji wakianza kuhamia huku," akasema 2017 Yattani.

Kutokana miradi ya maendeleo inayotekelezwa kaunti hiyo, biashara zimeonekana kuongezeka na kuimarika. Bw Mohamud Ali ndiye gavana wa Marsabit, baada ya kumbwaga UkurYattani ambaye kwa sasa ni Waziri wa Leba.

Seneta wa kaunti hiyo ni Godana Hargura na Mwakilishi wa Wanawake ni Bi Safia Sheikh Adan.