http://www.swahilihub.com/image/view/-/4960104/medRes/688555/-/c64cglz/-/Wambora.jpg

 

Wambora: Amepitia masaibu chungu nzima tangu achaguliwe Gavana Embu

Martin Wambora

Bw Martin Wambora akiwa mbele ya kamati ya Seneti Februari 14, 2014. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, January 31  2019 at  13:28

Kwa Muhtasari

Katika uchaguzi mkuu wa 2013, Gavana Martin Wambora alichaguliwa kwa tiketi ya TNA japo chama hicho kilivunjwa pamoja na URP ili kuunda mrengo wa Jubilee (JP), ambao ungali madarakani kufikia sasa.

 

MARTIN Nyagah Wambora si mgeni katika milango ya mahakama nchini Kenya.

Ukimuuliza 'tamu na shubiri' ya kufikishwa kortini, atakujibu bila kusita au akuorodhoshee kuanzia 'a' hadi 'z'.

Masaibu ya Bw Wambora ambaye kwa sasa anataniwa kama "binadamu mwenye nyoyo tisa" yalianza 2014, mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa gavana wa kwanza kaunti ya Embu.

Katika uchaguzi mkuu wa 2013 alichaguliwa kwa tiketi ya TNA japo chama hicho kilivunjwa pamoja na URP ili kuunda mrengo wa Jubilee (JP), ambao ungali madarakani kufikia sasa.

Wambora alizoa kura 94,699 dhidi ya mpinzani wake Kithinji Kiragu (APK) 82,814.

Wawakilishi wa wadi (MCA) mwaka wa 2014, walipitisha mswada wa kumng'atua kwa madai ya ubadhirifu pesa za umma. Aidha, alikuwa gavana wa kwanza nchini kuondolewa madarakani tangu utawala wa serikali za ugatuzi ung'oe nanga 2013 kupitia katiba ya sasa iliyoidhinishwa mwaka wa 2010.

Ilidaiwa alifuja pesa katika uagizaji na ununuzi wa mahindi. Bw Wambora anasema mahindi aliyoagiza yaligharimu Sh3.2 milioni ila si Sh32 milioni kama ilivyoripotiwa. "Tulifuata taratibu zote katika kuyaagiza, lakini wengine wakaleta 'fitina'. Hakukuwa na pesa zilizobadhiriwa na ndio maana mahakama kuu Kirinyaga iliniondolea mashtaka hayo," akasema Wambora mnamo Alhamisi kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, siku moja baada ya kupata afueni kumnusuru.

Hata hivyo, alipata afueni alipoelekea katika mahakama kuu ambayo ilibatilisha uamuzi wa bunge la kaunti ya Embu. Baadaye, Februari 2015 kamati ya fedha seneti inayoangazia utumizi wa pesa katika kaunti  ikifanya mchakato wa kuchunguza magavana waliotuhumiwa kwa ufujaji wa mali ya umma ilipendekeza Wambora ang'atuke.

Juhudi zake kupinga uamuzi huo katika mahakama kuu ziligonga mwamba, korti ilipoidhinisha pendekezo la seneti. Alikata rufaa ya mahakama kuu katika mahakama ya rufaa, ambayo ilimpa afueni kuendelea kuhudumu.

Martin Wambora

Aprili 2017 Wambora aliteuliwa kutetea kuhifadhi kiti chake katika mchujo wa Jubilee. Uchaguzini mkuu wa Agosti 8, 2017, alitoana kijasho na aliyekuwa seneta wa Embu Lenny Kivuti alimezea mate kiti hicho kwa Chama Cha Maendeleo.

Bw Wambora aliibuka mshindi kwa kuzoa kura 97,544, mshindani wake wa karibu Lenny akipata 96,597.

Kilichofuata kikawa Bw Lenny kupinga matokeo ya gavana. Tangu 2018, wawili hawa wamekuwa kortini kuanzia mahakama kuu, ya rufaa hadi ile ya juu zaidi na ambayo Jumatano iliidhinisha ushindi wa gavana Wambora.

Amewahi kuhudumu kama DO na DC katika serikali za marais wastaafu, Daniel Moi na Mwai Kibaki, na anasema hakuwahi tuhumiwa kwa sakata yoyote ya ubadhirifu wa pesa, utumizi mbaya wa mali ya umma wala ofisi.

"Nilihudumu katika serikali za marais wastaafu kwa zaidi ya miaka 20, sikuandamwa na mashtaka yoyote kwa sababu ya uadilifu na uaminifu wangu," anasema.

Kupitia masaibu yake, Wambora anasema nchini Kenya viongozi huondolewa madarakani kwa msingi wa ushawishi wa kisiasa. Akionekana kulenga wapinzani wake, gavana huyu anasema amekuwa akiandamwa na 'viongozi' wanaotaka uongozi kupitia milango ya nyuma. Anasisitiza kwamba uamuzi wa mahakama ya juu zaidi wa mnamo Alhamisi ni sauti ya wakazi wa Embu.