http://www.swahilihub.com/image/view/-/2204802/medRes/444110/-/d1lkmx/-/Wambui.jpg

 

Mary Wambui: Alimrambisha sakafu Gichuki Mugambi uchaguzi wa 2013

MaryWambui.

Aliyekuwa Mbunge wa Othaya, Bi Mary Wambui. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  13:35

Kwa Muhtasari

Aliyekuwa Mbunge wa Othaya, Mary Wambui anafahamika kwa ukarimu wake, uwazi wake na maneno na kuwa na roho ya kufunguka.

 

ALIYEKUWA Mbunge wa Othaya, Mary Wambui atabakia kuwa kitendawili kisicho kigumu kutegua kwa kuwa ukarimu wake, uwazi wake na maneno na kuwa na roho ya kufunguka huchangia pakubwa kueleweka.

Kuhusu kama kwa kweli alikuwa au ana uhusiano wowote na Rais Mstaafu, Mwai Kibaki, na sio tu uhusiano hivihivi kama mwanasiasa na mwanasiasa, anakuambia: “Enda umwambie anikane.”

Ni suala ambalo katika utawala wa Mwai Kibaki wa kati ya 2002 hadi 2013 ulikuwa ukizua cheche za makabiliano Ikulu, huku Mama wa Taifa wakati huo, Lucy Kibaki akijitokeza kila kukicha kuonya kuwa boma lake "hatuko wake wawili".

Hata kuna wakati mmoja rais Kibaki mwenyewe alijitokeza hadharani akianza kwa kutangaza kuwa “niko katika hisia mbovu” na akaendelea kutangaza kuwa “nina mke mmoja tu kipenzi changu na ni Lucy Muthoni Kibaki na ambaye tuko na watoto naye".

Wambui akasema hilo halimjalishi, bali kile angetaka ni nafasi yake tu, sakata hiyo ikizidishiwa makali na jamii ya Wambui ambayo ilimwagiza Mzee Kibaki ajitokeze kwao akiandamana na wazee ili akarejeshewe mahari aliyolipa…  Mambo yakifika hapo, hayatuhusu.

Wambui alizaliwa katika Kaunti ndogo ya Othaya iliyoko katika Kaunti ya Nyeri na aliishia kuchaguliwa kama mbunge wa Othaya katika uchaguzi mkuu wea 2013.

Hakujishindia awamu ya pili kwa kuwa katika mchujo wa Jubilee wa Aprili 2017, alitemwa nje na Gichuki Mugambi aliyerithi wadhifa huo akiwa amevunjika miguu katika ajali ya barabara.

Licha ya kuwa na changamoto zake za ufasaha wa lugha, alijijikakamua bungeni na akapata kunukuliwa akichangia hoja mara 105 tangu Machi 2013.

Alisomea katika shule ya msingi ya Munyange na akaishia kuwa mwalimu ambapo alifundisha shule ya msingi ya Mukima na pia ile ya Cheetah, zote zikiwa katika Kaunti ya Laikipia.

Mwaka wa 1974 alijiunga na kazi ya siasa ambapo alisajiliwa kama karani katika afisi ya Kanu Mjini Nyeri na ambapo Kibaki alikuwa amehamishia siasa zake kutoka Nairobi ambako alikuwa mbunge wa Bahati.

Mfanyakazi wa Kibaki

Aliishia kuwa msaidizi wa Kibaki na wakati 1978 Kibaki aliteuliwa kuwa Naibu wa Rais, alimuajiri Bi Wambui kama meneja wa shamba lake lililoko Rware, Kaunti ya Nyeri.

Alipewa gari aina ya Peugeot 504 na pia akahama kutoka makazi yake ya Kijiji cha Mumbi na akaishia katika mtaa wa hadhi wa Ring Road.

Alimfanyia Mzee Kibaki kampeni kwa dhati hadi 2013 ambapo aliwania kurithi ubunge wa Othaya kutoka kwake na akafanikiwa, licha ya kupigwa vita na familia ya Kibaki.

Ni msimamo wake Wambui kuwa aliolewa rasmi na Kibaki mwaka wa 1972 na ambapo alilipiwa mahari na taifa lilijua kuhusu hilo mwaka wa 2002 ambapo Kibaki alishinda urais na uhasama wa wake wawili ukawa suala la kitaifa badala ya hapo mbeleni ambapo walikuwa wanamenyana mashinani.

Uzuri wa Wambui ni kuwa, hakuna hata wakati mmoja alionyesha kuwa alikuwa anakerwa na kukataliwa kwake na Lucy Kibaki na hakuna hata wakati mmoja alitoa maneno yasiyostaarabika kuhusu hali hiyo.

Bi Wambui mwaka wa 2006 alihusishwa na mandugu wawili wa Armenia wakifahamika kama Artur Brothers na ambao walisemwa kuwa mafia wa kushirikisha njama zisizo halali hapa nchini chini ya uelekezi wake.

Waliishia kutimuliwa kutoka nchini na aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani, John Michuki.

Ana ukwasi ajabu na ametoa kwa jamii mamilioni ya pesa kama msaada na amejibakishia zake zisizo za kuhesabika.

Mwekezaji katika viwanda, mashamba, uzalishaji mifugo na hisa, bado ako katika sekta ya ujenzi ambapo ni mumiliki wa manyumba kadhaa ya kifahari.

Awe alikuwa mke wa Kibaki au la, amejitunza vyema kiuwekezaji na watoto wake watano hawawezi wakajuta kuwa na mama mwenye bidii kama yeye.