http://www.swahilihub.com/image/view/-/4918152/medRes/2211972/-/j0yabk/-/muroto.jpg

 

Matukio ya aina hii yakomeshwe katika jamii

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Wednesday, January 2  2019 at  10:04

Kwa Muhtasari

Tukio la kichanga kuwekwa kabatini ni la aina yake

 

Tangu juzi, vyombo vya habari na mitandaoni kumekuwapo na taarifa juu ya mtoto mwenye umri wa miaka 15 kunyanyaswa na mwajiri wake ikiwamo vipigo vilivyomsababishia majeruha.

Si hilo tu, inaelezwa pia kuwa mtoto huyo ambaye ni mzazi wa mtoto wa miezi mitano, mwanaye huyo amekuwa akifungiwa kabatini na mwajiri wake.

Licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto kudai kwamba madai ya mtoto huyo wa miezi mitano kufungiwa kabatini sio ya kweli, mama mzazi wa kichanga hicho amesimulia jinsi mwanaye alivyokuwa akiwekwa kabatini na mwajiri huyo ambaye hivi sasa anashikiliwa na polisi.

Mzazi huyo ameeleza alivyotumia mbinu ya kutoboa tundu katika kabati alimokuwa akiwekwa mwanaye ili kumyonyesha pia kumwezesha kupata hewa kwa ajili ya kuokoa maisha yake.

Mzazi huyo na mwanaye hivi sasa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa huo ambako inaelezwa kwamba kichanga hicho kinakabiliwa na utapiamlo.

Vievile, mtoto huyo anasema kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu mwajiri wake alipomchukua kijijini kwao, Kigwe wilayani Bahi, amekuwa hamlipi mshahara wake licha ya makubaliano kuwa angekuwa anamlipa Sh30,000 kila mwezi.

Tukio la kichanga kuwekwa kabatini ni la aina yake. Linafanana na lile la mwaka 2014 la Mariamu Said wa Morogoro aliyemficha mtoto wa marehemu mdogo wake kwenye boksi kwa miaka minne.

Mariamu aliyekuwa akiishi Kiwanja cha Ndege mjini humo alishushiwa kipigo na wananchi alipobaini kuwa alikuwa akimficha mtoto huyo, Nasra Rashid kwenye boksi baada ya majirani kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege.

Mhusika huyo alidaiwa kufanya ukatili huo tangu mtoto huyo akiwa na umri wa miezi tisa huku akiwa hamfanyii usafi wala kumtoa nje.

Kama ilivyokuwa kwa tukio hilo la Morogoro, tunawashukuru wasamaria wema waliofanikisha tukio la Dodoma kufahamika, wakiwamo majirani wa mwajiri wake ambao walipaza sauti hadi vyombo vya usalama vikafanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa.

Hili ni moja ya matukio ambayo yapo mengi ndani ya jamii. Kuna wasichana wengi wa kazi wanaopitia manyanyaso ya aina hii. Wapo wasichana wa kazi wanaolazwa mahala pachafu na waajiri wao, wanaolazimishwa kufanya ngono, wanaotumikishwa bila malipo na mambo mengine mengi mabaya.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kazi na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004, unyanyasaji kazini ni kosa la jinai linaloweza kumfanya mwajiri kutumikia kifungo, iwapo mahakama itamtia hatiani.

Vilevile, sheria hiyo inaonya juu ya utumikishaji kazi watoto wenye umri mdogo ambazo hawapaswi kuzifanya, huku ikielekeza namna mwajiri anavyopaswa kuishi na kuwatendea watoto anaoishi nao wanaomsaidia kazi ndogondogo.

Ni vyema tukio la Dodoma liifumbue macho jamii na vyombo vya usalama kukabiliana na walezi, wazazi pamoja waajiri wanaowanyanyasa watoto kwa sababu vitendo hivyo huibua chuki na athari za kisaikolojia ukubwani.