Mauaji haya ya watoto sasa yakome

Imepakiwa - Wednesday, May 15  2019 at  11:53

 

Matukio ya mauaji ya watoto wapatao 10 yaliyotokea mapema mwaka huu mkoani Njombe bado hayajafutika katika fikra za Watanzania walio wengi.

Mauaji hayo si tu kwamba yaliwagusa na kuwanyima raha wazazi na ndugu wa karibu au wakazi wa mkoani Njombe, bali hali hiyo ilikuwa kote Tanzania.

Kutokana na ukubwa wa tukio hilo haikushangaza kuwasikia viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini akiwemo Rais John Magufuli wakikemea na kutaka hatua zichukuliwe.

Kwa namna ambavyo tukio lile liligusa hisia za Watanzania wa kada mbalimbali wakiwamo viongozi wa ngazi za juu, tulidhani kwamba hali hiyo ingetosha kuwa sababu ya matukio ya aina hiyo kutojirudia tena.

Hata hivyo katika hali ya kushangaza na kusikitisha matukio hayo bado hayajakoma na mfano wa wazi ni tukio la hivi karibuni mkoani Mbeya linalomhusu mtoto wa miaka sita, Rose Nguku ambaye aliuawa kwa kunyongwa maeneo ya Igurusi wilayani Mbarali.

Tukio hili hapana shaka limewakumbusha kwa mara nyingine Watanzania matukio ya Njombe lakini pia linatukumbusha kwamba tatizo bado lipo na hivyo ipo haja ya kuja na mkakati wa kukabiliana nayo.

Tukio la mtoto huyo lilianza kwa kupotea ambako baada ya juhudi za kumtafuta ilibainika kwamba aliuawa na kufukiwa kwenye shimo akiwa amefungwa katika mfuko wa plastiki.

Kwa tukio hilo ni dhahiri kwamba Watanzania walio wengi wanabaki wakijiuliza mwisho wa matukio ya aina hii ni lini?

Tunahoji hilo kwa sababu haiingii akilini hata kidogo kuona watoto wanauawa kama wanyama na jamii ikakaa kimya. Hiyo itakuwa jamii ya hovyo.

Wakati vyombo vya usalama vikiendelea na uchunguzi wa tukio la mtoto Rose, tunadhani upo umuhimu wa Serikali kuja na mkakati maalumu.

Kwa mtazamo wetu mkakati huu tungependa kuona ukihusisha utoaji elimu kwa jamii, elimu itakayosaidia kumaliza matukio haya.

Tunalisema hili kwa sababu yapo madai kwamba kwa kiasi kikubwa mauaji haya yanahusishwa na imani za kishirikina kwa baadhi ya watu kuaminishwa kwamba watapata utajiri kwa kuuza baadhi ya viungo vya watoto na hivyo huamua kuwaua watoto hao ili wawe matajiri.

Hii ni imani potofu ambayo kiini chake ni watu kutotambua ukweli kwamba mafanikio au utajiri unapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na hakuna zaidi ya hilo.

Matajiri wote wakubwa duniani au watu wote ambao wamepata mafanikio ukiwauliza siri kubwa ya mafanikio yao pamoja na mipango yao mizuri lakini kubwa watakalokwambia ni kufanya kazi kwa bidii.

Dhana ya kufanya kazi kwa bidii ndiyo ambayo tunaamini imekosekana kwa wale wanaodiriki kuua watoto na ndio maana tunaikumbusha Serikali itoe elimu ikiwezekana ya dhana nzima ya ujasiriamali na umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii.

Watu waelimishwe ukweli kwamba hakuna njia ya mkato ikiwamo kuua watoto katika kutafuta mafanikio, badala yake mafanikio yatapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii.

Bila ya watu kuelimishwa tunaweza kushuhudia matukio ya aina hii yakiendelea kujitokeza mara kwa mara na hivyo kuendelea kuwaacha Watanzania katika hali ya unyonge pamoja na kuchafua heshima ya nchi yetu kimataifa.