http://www.swahilihub.com/image/view/-/4612396/medRes/1929850/-/ysal20/-/faustine.jpg

 

Mbinu mpya ya ukeketaji yabuniwa

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile  

Na Bakari Kiango

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  16:13

Kwa Muhtasari

Wahusika wamebuni mbinu ya kuwakeketa watoto wachanga

 

Arusha. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amewaagiza waganga wakuu kuweka utaratibu wa kuwakagua watoto wachanga wanaokwenda kliniki ili kubaini kama wamekeketwa.

Agizo hilo limekuja baada ya mkuu wa wilaya ya Arusha, Fabian Daqaro kumweleza waziri kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji vimeshamiri huku wahusika wakibuni mbinu ya kuwakeketa watoto wachanga, tofauti na ilivyokuwa awali.

Dk Ndugulile alitoa agizo hilo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kitaifa mkoani hapa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali yakiwamo mashirika ya Plan International na World Vision.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Kuelekea uchumi wa viwanda, tusimwache mtoto nyuma.’

Ndugulile alisema Serikali itoe waraka kwa waganga wakuu wa mikoa yote, watoto wanapopelekwa kliniki kupimwa afya, wafanyiwe ukaguzi ili kuwabaini kama wamefanyiwa vitendo vya ukeketaji.

“Mtoto yeyote atakayebainika amekeketwa, wazazi husika watachukuliwa hatua. Jambo hili linawezekana na ni agizo na utekelezaji wake uanze mara moja,” alisema Dk Ndugulile.

Ndugulile alitumia nafasi hiyo kuitaja mikoa mitano inayoongoza kwa vitendo kwa vya ukeketaji kuwa ni pamoja na Manyara unaoongoza kwa asilimia 58, Dodoma (47), Arusha (41), Mara (32) na Singida (31).

Awali, akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Daqaro aliiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuwakagua watoto hao pindi wanapoenda kliniki ili kudhibiti vitendo vya ukeketaji.

“Tusiangalie tu mtoto analishwa nini bali pia, namna ya kumlinda dhidi ya ukeketaji. Lazima tufanye hivi ili tuwasaidie na tusipofanya hivi hatuwezi kufanikiwa katika jitihada hizi,” alisema Daqaro.

Kwa upande wake, naibu mkurugenzi wa Plan International, Dk Benatus Sambili alisema kwamba lengo la shirika hilo ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika suala zima la haki za watoto.