http://www.swahilihub.com/image/view/-/4128580/medRes/1773489/-/e7be1gz/-/muja.jpg

 

Kaunti ya Meru: Kilimo cha ndizi kimeizolea sifa

Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta (kulia), Gavana wa Meru Kiraitu Murungi (kati) na Peter Munya wakiwa sokoni Laare, Igembe Kaskazini ambapo walihutubia umati Oktoba 6, 2017. Picha/PHOEBE OKALL 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Saturday, March 31  2018 at  15:49

Kwa Muhtasari

Meru imetambulika kwa kilimo cha ndizi.

 

KAUNTI ya Meru inapatikana Mashariki mwa Kenya.

Umbali wake ukitoka jiji kuu Nairobi ni kilomita 225.

Aidha ina ukubwa wa kilomita 6,936 mraba, na kwa mujibu wa sensa ya 2009 kaunti hiyo inakadiriwa kuwa na zaidi ya watu 1,365,301.

Gavana wake ni Profesa Kiraitu Murungi, ambaye alimbwaga kiongozi wa PNU Peter Munya katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 aliyeongoza Meru tangu 2013.

Hata hivyo, Januari 2018 Rais Uhuru Kenyatta alimteua kuwa waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakati akitangaza baraza la mawaziri ya serikali yake anayoiongoza kwa kushirikiana na Naibu Rais William Ruto.

Aliyekuwa mbunge wa Igembe Kusini Mithika Linturi, Agosti 8 alitwaa useneta wa kaunti hiyo, huku Bi Kawira Mwangaza akichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Wanawake.

Meru imepakana na kaunti ya Isiolo upande wake wa Kaskazini, Nyeri na Tharaka Nithi Kusini Maghariki mwake, na Laikipia upande wa Magharibi. Imeundwa na maeneobunge tisa; Igembe Kusini, Igembe ya Kati, Igembe Kaskazini, Tigania Magharibi, Tigania Mashariki, Imenti Kaskazini, Buuri, Imenti ya Kati na Imenti Kusini.

Jina Meru inaaminika kutoka kwa jamii ya Maasai, ambayo ilitamka Misitu ya Tigania na Imenti kama 'Mieru', kwa maana ya 'misitu mtulivu'.

Jamii hiyo pia, ilitambua kabila ambalo halikuelewa lugha yao ya Maa kama 'Mieru'.

Awali, muungano wa jamii za Mlima Kenya Gema ndio walikuwa wakiishi kaunti hiyo, lakini kwa sasa chini ya serikali za ugatuzi na taifa kukengeuka, karibu makabila yote Kenya yametangamana na kuishi Meru.

Wakazi wa kaunti hiyo wana imani za kidini kwa kuzingatia kwamba kuna makanisa, misikiti na madhehebu.

Jamii ya Meru aghalabu humtambua Mungu kama Murungu, Arega ama Kuthera.

Kando na historia hiyo fupi, Meru ni kaunti inayothamini kilimo.

Mchanga wake ni wenye ukwasi wa rutuba, ambapo mimea ainati hukuzwa. Kiwango cha joto huwa nyuzi 16 msimu wa baridi, na nyuzi 23 msimu wa joto. Meru hupokea mvua yenye wastani wa milimita 500 hadi 2600 kwa mwaka.

Kilimo cha miraa ndicho kinafahamik sana kuendeshwa kaunti hiyo. Mmoja anapofunga sfari kuelekea Meru, hutaniwa "Ukienda Meru nijie na miraa". Hata hivyo, ulijua kuwa kauli hiyo sasa imebadilika na kuwa, "Ukienda Meru nijie na ndizi"?

Ripoti iliyotolewa mwaka 2016 ilifichua kuwa kilimo cha ndizi Meru huizolea Sh3.7 bilioni kwa mwaka.

Wizara ya Kilimo, chini ya aliyekuwa waziri wake Willy Bett, ilisema wakazi wengi wa kaunti hiyo wamezamia kilimo cha ndizi, ambacho wanasema kina natija chungu nzima.

"Karibu ekari 9,715 Meru zinakuzwa migomba na huvuna zaidi ya tani 382,390 za ndizi, msimu mmoja," ikasema ripoti hiyo.

Ndizi

Aidha ilibainika Meru imepiku kaunti ya Kisii katika kilimo cha ndizi.

"Meru imeonekana kuinuka katika sekta ya kilimo, awali nilifahamu Kisii ndiyo hukuza ndizi kwa wingi lakini Meru imeipiku," akasema waziri Bett, wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Nairobi 2017.

Kwa sasa kaunti hiyo ndiyo inaongoza nchini kwenye uzalishaji wa ndizi, ikifuatwa kwa karibu na Tharaka Nithi, chini ya gavana wake Bw Muthomi Njuki. Bw Munya alisaidia pakubwa wakulima wa Meru kupata soko la zao hilo.

Mbali na kilimo cha ndizi na miraa, ukuzaji wa kahawa, pareto, mahindi, mtama, maharage, wimbi, ngano, viazi mbatata na tumbaku, pia unaendeshwa Meru.

Sekta ya Afya kaunti hiyo pia imeimarika pakubwa, ambapo ina zaidi ya vituo 200 vya afya. Hospitali kuu ni kama vile; Chuka District, Meru District, Tigania, Miathene, na Kanyakene.

Meru ina zaidi ya shule 712 za msingi na 112 za upili. Pia, ina vyuo vikuu na taasisi za juu za elimu.

Kaunti hiyo ni kivutio cha watalii kwa ajili ya mbuga ya wanyama ya Kitaifa ya Meru.

Ni miongoni mwa kaunti zilizo na watu mashuhuri nchini kama vile; balozi Francis Muthaura, wakili na mwanasiasa Gitobu Imanyara na aliyekuwa kamishna mkuu wa polisi Mathew Iteere.