Mfumo wa stakabadhi ghalani una faida nyingi

Imepakiwa - Thursday, April 4  2019 at  09:08

 

Kwenye bajeti iliyopo ya Serikali, kilimo ni miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele katika utekelezaji wa azma ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda. Kilimo kinatakiwa kutoa malighafi muhimu zitakazozalisha bidhaa zinazokusudiwa.

Kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakilalamika kilimo hakiwatoi kimaisha japo wanajitahidi kulima kwa bidii.

Mfuko wa Mazao wa Umoja wa Mataifa (CFC), ulianzisha mfumo wa stakabadhi ghalani wenye lengo la kumwezesha mkulima kupata fedha au mkopo kutoka taasisi za fedha bila kuhitaji dhamana, isipokuwa mazao yake yaliyopo ghalani.

Nchini, kumbukumbu zinaonyesha ulianza kutumika mwaka 2000 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ukiwahusisha pia wadau wa sekta binafsi kama taasisi za fedha, waendesha maghala, viwanda vya kusindika mazao, kampuni ya kusimamia dhamana pamoja na bodi za mazao.

Kumekuwapo na malalamiko dhidi ya viongozi wa vyama vya msingi na ushirika kukopa mazao ya wakulima na kuyauza pasipo kuwalipa wahusika kwa wakati, hivyo kudidimiza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.

Mfumo wa stakabadhi ghalani ni mwarobaini wa kututoa kwenye mtindo huo wa kizamani ili tuanze kuwalipa wakulima kwa wakati badala ya kukopa mazao yao.

Takwimu zinaonyesha kuwa bado mwitikio wa benki kujihusisha na mfumo ni mdogo kwani ni NMB na CRDB na chache nyingine ndizo zenye mfumo huu. Ni vyema benki zote nchini zikautazama mfumo huu ambao ni mkombozi kwa mkulima, huku ukiwa na fursa za kuzipa biashara kubwa itakayosaidia kufanikisha malengo ya benki husika.

Mfumo wa stakabadhi ghalani ni utaratibu ulioanzishwa kisheria kuruhusu mazao kuwa dhamana ya kupata mkopo kutoka taasisi za fedha. Mfumo huu unampa mkulima uwezo wa kupata mkopo utakaomwezesha kuendelea na uzalishaji na kujikimu mpaka bei itakapokuwa nzuri ili auze mazao yake kwa faida na kulipa mkopo wa benki.

Mfumo huo una hatua kadhaa zinazojumuisha kuwa na makubaliano baina ya benki na wakulima husika kuhusu mikopo itolewayo kwa dhamana ya mazao kupitia umoja wao ama chama cha ushirika.

Kila mkulima ni lazima apeleke mazao yake ghalani baada ya kukaguliwa ubora, uzito, ujazo na thamani, na benki kutaarifiwa kulingana na stakabadhi iliyotolewa kwa mkulima husika.

Baada ya kupata stakabadhi hiyo, mkulima ataipeleka benki itakayoamua kumpa au kutompa mkopo kulingana na taarifa za mazao zilizobainishwa.

Endapo benki itamkopesha mkulima, mazao yaliyopo ghalani yataendelea kuwa mali ya benki mpaka mkopo utakapolipwa.

Mteja atakapopatikana atayalipia kwenye benki husika ambayo itakata mkopo iliyotoa na gharama zinginezo na kiasi kitakachobaki kitaingizwa kwenye akaunti ya mkulima.

Baada ya malipo kufanyika, benki itaruhusu mazao yatolewe ghalani.

Mfumo huo una faida kwa benki, mkulima na Taifa kwa jumla. Kwanza ni unapanua wigo wa ukopeshaji. Benki nyingi za biashara nchini zinajitahidi kuweka mikakati itayozisaidia kuongeza wateja wa kuwakopesha na mfumo huu una uhakika wa kufanikisha nia hiyo.

Faida nyingine ni kuimarisha taswira ya benki machoni pa wateja, hivyo kuwafanya waiamini na kuendelea kushirikiana nayo katika mambo mbalimbali ya kibiashara.

Kitendo cha benki kuwakopesha wakulima na kuwawezesha kuuza mazao yao kwa bei nzuri ni kiashiria cha wazi cha benki husika kuwasaidia kuwaongezea nguvu ya soko itakayosaidia kupata faida. Faida ikipatikana maisha yao yatakuwa bora zaidi.

Mfumo huu unatoa fursa kwa mkulima kuongeza thamani ya mazao bila kuwa na haraka ya kuwahi soko, hivyo kupata bei nzuri katika soko la ndani na kimataifa.

Endapo mfumo huu utatumika kikamilifu utaliwezesha Taifa kupata fedha nyingi za kigeni kupitia soko la kimataifa kwani mazao yatakuwa na ubora wa ushindani kwenye soko la kimataifa.

Mfumo wa stakabadhi ghalani ni rafiki kwa benki na mkulima na unamwezesha mkulima kupata faida ya mazao yake kwa wakati hivyo kuchochea uzalishaji endelevu.

Vilevile, mfumo huu ninyenzo muhimu kwa sera ya uchumi wa viwanda ambao ukichangamkiwa na benki za biashara mafanikio yake yatakuwa mtambuka.

Mwandishi ni mkufunzi wa Chuo Kikuu Ardhi. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa namba 0765 666 255