Mfumo wetu wa elimu utazamwe upya

Imepakiwa - Thursday, May 2  2019 at  11:25

 

Wabunge ndani ya Bunge la Muungano wameichambua sekta ya elimu nchini wakisema mfumo wake unahitaji kufumuliwa ili uwe na tija kwa mustakabali wa kizazi kilichopo na kijacho.

Kauli za wabunge hao zilijitokeza wakati wakichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya 2019/2020.

Wabunge wengi waliopata fursa kuchangia bila kujali itikadi za kisiasa kwenye michango yao, kila mmoja aligusia changamoto inayoikabili sekta ya elimu.

Tunafahamu kwamba Serikali imefanya mambo makubwa katika kuendeleza elimu, lakini zipo changamoto ambazo inabidi izifanyie kazi kwa kushirikisha wadau.

Wabunge wanasema Tanzania inatakiwa kuwa na mfumo wa elimu utakaomwezesha mtu anapohitimu aweze kuishi bila kutegemea kuajiriwa na mtu au taasisi yoyote.

Pia, walizungumzia sheria iliyoanzisha sekta ya elimu kwamba imepitwa na wakati kwa kuwa ilitungwa siku nyingi na haiwezi kujibu matatizo ya yanayoikumba nchi kwa sasa.

Hoja za wabunge zinafanana na zile zilizowahi kutolewa mara mbili, kwa nyakati tofauti na Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyependekeza uanzishwe mjadala wa kitaifa kuhusu sekta ya elimu nchini kwa ajili ya mustakabali wa sekta hiyo.

Mkapa ambaye ni mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), alisema kuna janga katika sekta elimu na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi wa kitaifa utakaoshirikisha makundi yote ya kijamii.

Mkapa alikuwa akizungumzia suala hilo kwa mara ya pili baada ya Novemba 11, 2017 kuwaambia washiriki wa kongamano la wanataaluma Udom, kwamba Tanzania haijaweka msukumo katika kutafakari upya mfumo wa elimu.

Mbali na Mkapa, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete aliwahi kunukuliwa akisema Afrika inaweza kuwa inapiga hatua katika kuendeleza elimu, lakini inahitaji kuongeza juhudi hasa kutoka elimu ya msingi hadi sekondari.

Tunaamini sauti za wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi ni sauti za Watanzania walio wengi, matokeo mabaya katika sekta ya elimu yanaliweka pabaya Taifa.

Pia, ifahamike elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa kwani wataalamu mbalimbali wakiwamo madaktari wa hospitalini, wanasheria na wajenzi wa miundombinu wanatokana na elimu bora.

Tanzania ni mwanachama wa nchi za Afrika Mashariki; Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na zingine nyingi ambako kote huko kuna fursa nyingi za ajira na biashara zinazohitaji wasomi. Pia, kama yalivyo mataifa mengine, imekaribisha wawekezaji wa kigeni ambao wameleta ushindani katika soko la ajira.

Hiyo ina maana kwamba kama elimu yetu itaendelea kuwa hafifu, itakuwa ni ndoto kwa watu wetu kupata ajira nono kwenye kampuni za wawekezaji, badala yake wataishia kuwa vibarua wanaolipwa ujira mdogo.

Rai yetu ni kuwa, bado hatujachelewa na wahenga walisema “ukubwa ni dawa,” hivyo mawazo yaliyotolewa na viongozi wetu wastaafu tunapaswa kama Taifa kuyatafakari kwa mapana yake. Wabunge wameonyesha njia, hoja zao zinapaswa kubebwa kwa uzito wake na waziri mwenye dhamana na wizara hiyo ili zifanyiwe kazi haraka kwa manufaa ya watu wetu na Taifa letu.