http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706768/medRes/2075258/-/eq4gylz/-/mwgl.jpg

 

Mgalu atishia kuwaweka mahabusu wasimamizi wa Rea

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu  

Na Mussa Mwangoka

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  15:05

Kwa Muhtasari

Lengo likiwa umeme upatikane haraka iwezekanavyo

 

Sumbawanga: Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfan Haule kuwaweka mahabusu wasimamizi wa utekelezaji wa mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) iwapo watasuasua katika ujenzi wa miundombinu ya umeme wilayani hapa.

Mgalu alitoa agizo hilo jana katika Kijiji cha Kilyamatundu kilichopo mpakani mwa Mikoa ya Mbeya na Songwe.

Naibu waziri huyo yupo wilayani hapa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa mradi wa Rea awamu ya tatu, unaotekelezwa na Kampuni ya Nakuroi Investment.

Kabla ya kutoa agizo hilo, alionyeshwa miundombinu inayowezesha upatikanaji wa umeme katika kijiji jirani cha Kamsamba Mkoa wa Songwe umbali wa mita 100 huku akihoji kwa nini Kijiji cha Kilyamatundu kilichopo Rukwa hakinufaiki na huduma ya umeme ilhali miundombinu ipo karibu.

“Mkandarasi nataka nguzo na vifaa vingine vifike hapa Alhamisi ijayo kama ulivyoahidi na ujenzi wa miundombinu ya umeme ianze mara moja.

“Mkuu wa wilaya hakikisha unatumia mamlaka yako kuwaweka ndani (mahabusu) kwa saa 48 hawa jamaa kama watasuasua kutekeleza mradi huu. Sisi lengo letu umeme upatikane hapa kijijini haraka iwezekanavyo,” alisema naibu waziri.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Haule aliahidi kutekeleza agizo hilo akisema Serikali imechoka kuendelea kuchonganishwa na wananchi kwa uzembe wa wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali kwa kusuasua hivyo sheria lazima ichukue mkondo wake.

Awali, mbunge wa Kwela (CCM), Ignas Malocha alisema wananchi wa Kata ya Kipeta wanashindwa kumuelewa kutokana na kijiji jirani ambacho mbunge wake anatoka upinzani kina umeme huku yeye wa chama tawala akihaha kuomba vijiji vya jimbo lake kupata umeme.

Jimbo jirani na Kwela ni Momba ambalo mbunge wake ni David Silinde (Chadema).