Miaka 55 ya Muungano ni ukomavu wa kuondoa kero.

Imepakiwa - Tuesday, April 30  2019 at  11:31

 

Maadhimisho ya miaka 55 ya kumbukumbu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yamefanyika bila kuwa na sherehe lakini ilikuwa siku ya mapumziko.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kiasi cha Sh988.9 milioni ambazo zilipangwa kwa ajili ya sherehe za Muungano mwaka huu, zitapangiwa kazi nyingine.

Ni utamaduni ambao umeanza kuzoeleka kutofanyika sherehe za kitaifa ili kuokoa mamilioni ya fedha ambayo hutengwa.

Katika dhana ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha nyingi katika kutatua kero za wananchi hili ni jambo jema na hakika fedha nyingi zinaokolewa.

Waliowengi watakubaliana nami kuwa fedha nyingi ambazo hutengwa katika maadhimisho ya sherehe mbali mbali, hunufaisha wanjanja wachache kulipana posho, kushona sale, kukodi magari, chakula na kulipa vikundi vya hamasa.

Hata hivyo, naamini kuahirishwa kwa sherehe hizi ni kipindi cha mpito na mambo yakikaa sawa, tutaendelea kuona maadhimisho yake lakini pia kutakuwepo uadilifu katika matumizi ya fedha.

Hii inatokana na ukweli kwamba kutofanyika kwa sherehe hizi za kitaifa kuna athari nyingi kwa vizazi vijavyo kwani itafika wakati watashindwa kutambua sherehe hizi muhimu katika historia ya Taifa lao.

Sasa nirejee katika mada yangu ya leo, April 26 Watanzaia wamesherehekea nyumbani siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao sasa umetimiza miaka 55.

Muungano huu utaendelea kuwa wa mfano duniani, kwani mataifa mengi yameshindwa kuungana na wapo ambao wanautazama muungano huu kwa jicho jema na wengine jicho la husda.

Waasisi wa Taifa hili, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume walikubali nchi zao kuungana mwaka 1964 kwa kutambua kuwa mara zote umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Hata hivyo, hakuna jambo linalo iosa changamoto ndivyo ilivyokuwa katika Muungano huu kwani kila upande una tabia zake, historia yake na mahitaji tofauti.

Hata katika ndoa ni agharabu sana kukosa misukosuko kwani kila mmoja ametoa katika malezi tofauti na tabia zake haziwezi kufanana na mwingine.

Lakini ambacho kinawafanya wanandoa kukaa pamoja licha ya changamoto zote huwa ni kuvumiliana, kusameheana na kuheshimiana kutokana na tofauti ambazo zinajitokeza.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bado unakabiliwa na changamoto kadhaa, zipo ambao zimefanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi lakini bado ambzo hazijafanyiwa kazi mpaka leo.

Zipo changamao kadhaa za Muungano huku nyingi zikitokana na historia ya Muungano wenyewe, kwani kuunganisha mataifa mawili na kuendelea kubaki mawili ni kitu kikubwa.

Hivyo maneno ya upande mmoja kumeza upande mwingine yamekuwapo na ndio sababu mara kadhaa masuala ya Muungano yamebaki kuwa ni nyeti sana katika historia ya Taifa hili.

Hivi karibuni kuliibuka mjadala mzito bungeni ambako naibu waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji na waziri wa zamani ya wizara hiyo Dk Saada Mkuya ni ishara tosha bado kuna kero za Muungano na lazima ufumbuzi upatikane.

Mjadala huu ulitokana na hoja za mbunge wa Ubungo Saidi Kubenea, aliyehoji ni lini Serikali itapeleka bungeni mabadiliko ya sheria ili kuruhusu Zanzibar kuruhusiwa kukopa fedha kwa ajili ya miradi yake.

Ni wazi kuwa baada ya mjadala ule, Serikali itaendelea kuchukuwa hatua kuondoka manung’uniko.

Kama nilivyosema awali umoja nyingi ni nguvu hivyo mataifa yanapoungana sauti yao huwa na uzito zaidi kuliko taifa moja na hata katika uchumi muungano unafaida kubwa.

Lakini pia Muungano mzuri ni ule ambao unajengwa kwa msingi wa maridhiano kila upande kuridhia kwa dhati mambo ambayo yanawaunganisha.

Naamini changamoto za Mungano wetu ndizo ambazo huibua hoja ya kuwa na Serikali tatu au moja, kwani kuna mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi ili uendelee kudumu.

Kwa bahati nzuri, pande zote za Muungano hakuna hata mmoja ambao unataka kuvunjwa na hili ni jambo la kujivunia sana kwani faida zake zinaonekana dhahiri. Kama nilivyosema awali, kila Muungano una changamoto zake na dawa huwa ni kuzipunguza na hatimaye kuziondoa kwani Watanzania wengi wanatamani siku moja ziishe kabisa.