http://www.swahilihub.com/image/view/-/3848096/medRes/1624472/-/h5b07a/-/RWE.jpg

 

Michango ya wasomi kwenye Mdahalo wa Lugha uliofanyoka Dar es Salaam

Profesa Rwekaza S. Mukandala

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza S. Mukandala akihutubu awali. Picha/ HISANI 

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Monday, March 20  2017 at  18:06

Kwa Mukhtasari

UAMUZI wa kutumia Kiswahili katika Nyanja mbalimbali nchini Tanzania : Je, ni wakati mwafaka?

Huu ni mdahalo uliofanyika Machi 19, 2017 katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wadau wa Kiswahili ndani ya nchi na nje ya nchi.

 

Wazunguzaji walikuwa wa aina mbili. Kwanza ni wazungumzaji waalumu ambao ni wanne ambao watashiriki, wawili kuunga mkono hoja na wawili pupinga hoja.

Wazungumzaji hawa walizingatia fani za Elimu – (Profesa K. Mkumbo na Dk  G. Kahangwa), Sayansi (Dk M.L. Manoko), Uchumi – Dr Prof A. Mkenda), Hisabati- (Dk S.Sima), Sheria- (Prof Safari), Habari na Mawasiliano A. Ryoba).

Wazungumzaji hawa walikuwa ‘wachokozi’ na waliohudhuria mdahalo huu walipata fursa ya kuchangia mawazo yao. Pamoja na wataalamu na wa Kiswahili waliohudhuria walkuwapo pia waandishi wa Kiswahili, wanachuo wa vyuo vikuu, walimu wa shule za msingi na sekondari kutoka katika shule za Dar es Salaam na miji ya Bagamoyo na Morogoro.

Michango iliyotolewa ni maelezo kuhusu tafiti zilizowahi kufanywa za kupata maoni ya wananchi juu ya uwezekano wa kutumia Kiswahili katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Utafiti uliofanywa hapo awali katika miaka ya 1976 uliongozwa na Profesa Penina Mlama na Dk May Matteru wa Chuo Kikuu cha DSM uliwahusisha walimu wa shule za msingi na sekondari, wakufunzi, wakurufunzi ngazi zote, waandishi wa vitabu na wachapishaji vitabu na viongozi wa elimu wa wilaya, mikoa na wakaguzi wa shule.

Wengi walishauri kuwa Kiswahili kinaweza kutumika kama lugha ya kufundishia ila walitoa tahadhari kama:

Kwanza kuwe na istilahi za kutosha zitakazotumika kutafsiri vitabu na Makala za kitaaluma. Bakita na wadau wengine waongeze kasi ya kutafsiri na kuwashirrikisha wataalamu wengine.

Pili mtalaa wa Kiswahili uhuishwe ili kuendana na kasi ya mahitaji ya wataalamu wa kufundisha Kiswahili nchi za nje.  Hii itawpa vijana wahitimu wa somo la Kiswahili kupata ajira. Inaonekana kuwa Wakenya wameshika hatamu katika nchi za nje kama walimu wa

 kufundisha Kiswahili ambapo Watanzania wamelaza damu.

Tatu tunatakiwa tuwekeza katika Kiswahili kwa maana ya kutenga fedha za kutosha katika bajeti za wizara hasa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia naMafunzo  na mashirika ya umma

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo Mhandisi Stella Manyanya, alihudhuria kama mkereketwa na alitilia mkazo umuhimu wa kuongezwa kwa kasma ya Kiswahili katika bajeti.

Alisema, "Tayari mawasiliano yako katika kila sekta mbalimbali za kukuza Kiswahii hasa kwa upande wa viongozi kwani lugha ni biashara, uchumi, sheria na afya kwani ni njia muhimu ya ya awali na ya msingi na lugha ya Kiswahili itatiliwa mkazo ila ni muhimu lugha inayotumika iwe sanifu na fasaha.”

Mgeni rasmi alikuwa Mama Salma Kikwete, balozi wa Kiswahili barani Afrika. Yeye alisisitiza mchango wa viongozi wa nchi katika awamu zote.  Wote walijitahidi kukuza matumizi ya Kiswahili fasaha. 

Mwalimu J.K. Nyerere ni mfano wa kuigwa akiwa mwasisi wa nchi hii ndiye aliyeweka  msingi imara kwani alikitumia wakati wa kampeni za kupata uhuru na hata baada ya uhuru. Alisema,” Mwalimu alitumia Kiswahili kulihutubia Bunge la kwanza la Kutunga Sheria mwaka 1961.

Aliweka misingi imara ya matumizi ya Kiswahili katika nyanja hasa pale alipotafsiri vitabu viwili vya “Sheakespere” kwa Kiswahili kama “Julius Kaisari” na “Merchant of Venice”. Marais wengine walifuata nyayo zake.

Aliongeza, “Kinachotutia moyo zaidi ni kwa Rais wa Awamu ya Tano, Rais John Pombe Magufuli anavyojitahudi kukitumia Kiswahili katika matukio ya kimataifa kama alivyofanya pale Addis Ababa akizindua Jengo la Kumbukumbu za Mwalimu Nyerere na wakati wa hafla za kitaifa Ikulu”.