Mikakati dhidi ya tishio la njaa ianze sasa

Imepakiwa - Friday, March 29  2019 at  11:09

 

Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeshatangaza uwezekano wa kuwapo kwa ukame katika baadhi ya mikoa.

Ukame huo unatokana na uhaba wa mvua ambao TMA inasema umeikumba mikoa ya Morogoro (upande wa Kaskazini), Pwani, Tanga, Manyara na Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa TMA hata ikiwa mvua hizo zitanyesha, upo uwezekano wa kunyesha chini ya wastani na kwa muda mfupi tofauti na inavyotarajiwa.

Hali hii ndiyo iliyolitia hofu Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), ambalo katika taarifa yake ya juzi, limeishauri Serikali kuchukua tahadhari mapema, kwa kuwa inahatarisha upatikanaji wa chakula katika siku zijazo.

Jambo linalotia moyo ni kuwa Serikali haijabweteka; inajua fika hali hiyo na ndio maana hivi karibuni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alinukuliwa na gazeti hili akiwasihi wakulima kupanda mazao yanayohimili ukame.

Kama haitoshi siku chache baadaye Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba naye akasema Serikali inafahamu kuwapo kwa tishio hilo la ukame linaloweza kuhatarisha upatikanaji wa chakula, hivyo mamlaka husika zimeshaanza kuchukua hatua kadhaa ikiwamo kufanya tathmini ya hali ya upatikanaji wa chakula na kusitisha kukiuza katika nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Malawi.

Jingine linalotia moyo kwa mujibu wa Mgumba ni uamuzi wa Serikali kuiagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kununua chakula cha kutosha ambacho bila shaka kitakuja kusaidia hali ikiwa mbaya siku za mbele.

Kama tulivyoanza kwa kusema kuwa hali ya hewa inaweza kuwa siyo nzuri, hivyo kama Serikali inavyopigania suala hili kwa kuhakikisha kunakuwapo kwa unafuu wa upatikanaji wa chakula, wajibu huu usiishie kwa Serikali na vyombo vyake, bali ni wajibu wa kila Mtanzania kwa nafasi yake.

Kwa ngazi ya mtu binafsi au familia hiki si kipindi cha kutapanya chakula wala kula na kusaza. Wakulima nao kama alivyosema Waziri Hasunga wajikite katika kuzalisha mazao yanayohimili ukame.

Bahati nzuri tangu kuanza kwa taarifa hizi za uhaba wa mvua katika baadhi ya maeneo nchini wataalamu wetu wa kilimo hawajajiweka kando, wamekuwa wakitoa ushauri wa nini cha kufanya katika kipindi hiki.

Ni ushauri unaotakiwa kufanyiwa kazi hasa na wakulima. Kwa mfano, wataalamu wanasema katika kipindi kama hiki mazao yanayostahili kupandwa ni pamoja na mtama, uwele, mbaazi, muhogo na viazi vitamu. Mbegu za mazao haya zilizofanyiwa utafiti katika vituo mbalimbali vya utafiti wa kilimo zipo na zinapatikana madukani.

Sambamba na upandaji wa mazao yanayostahimili ukame, ni muhimu pia kuwakumbusha wakulima kuhusu matumizi ya mbinu mbalimbali za kilimo hasa zile zinazoendana na mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo, haya yote yanabaki kuwa ni juhudi na mikakati ya muda mfupi. Ikiwa tunataka kweli kuwa na uhakika wa chakula na ziada kwa mwaka mzima, hatuna budi kuwekeza ipasavyo kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Aina hii ya kilimo ndio mwarobaini wa kukabiliana na ukame na mabadiliko ya tabia nchi.