http://www.swahilihub.com/image/view/-/4920698/medRes/2214783/-/7wam2q/-/paul.jpg

 

Mikakati inahitajika kunusuru vyuo vyetu

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU), Paul Loisulie  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, January 4  2019 at  09:26

Kwa Muhtasari

Wasomi wenye sifa wanakimbia vyuo vikuu kwa sababu ya masilahi

 

Utafifi uliofanywa na Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu (THTU), mwaka 2017 unaonyesha kuwa taasisi za elimu ya juu zinakabiliwa na upungufu wa watumishi wa aina zote wakiwamo wanataaluma na wafanyakazi waendeshaji.

Kamati maalumu iliyoundwa na chama hicho ilitembelea baadhi ya taasisi na kutoa ripoti iliyoonyesha kuwapo kwa upungufu wa asilimia 44 ya watumishi wanataaluma katika taasisi za umma.

Kamati pia ilibaini kuwa asilimia 53 ya watumishi wanataaluma katika ngazi ya uandamizi na kuendelea waliopo kwa sasa wamestaafu na hivyo wanafanya kazi kwa mikataba au wanatarajia kustaafu hivi karibuni na wataingia kwenye ajira za mikataba.

Pia, inaonyesha kuna upungufu wa wastani wa asilimia 41 ya watumishi wasiokuwa wanataaluma katika taasisi zilizotembelewa na kamati hiyo.

Athari ya hali hii ni vyuo vingi kuwa na wahadhiri wengi ambao bado wako kwenye madaraja ya wahadhiri, wahadhiri wasaidizi au wakufunzi badala ya wahadhiri waandamizi na maprofesa.

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), vyuo vyetu vina jumla ya wahadhiri 3,448. Inasikitisha kuwa katika orodha hii, maprofesa wapo 274 pekee.

Wengine katika idadi hiyo ni maprofesa washiriki 376, wahadhiri waandamizi 783, huku waliobaki 2,015 wakiwa ni wahadhiri wa kawaida.

Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa vyuo vikuu vinavyomilikiwa na sekta binafsi, ndio maana katika miaka ya karibuni tumekuwa tukishuhudia TCU ikivizuia baadhi kudahili kutokana na kuwa na udhaifu mkubwa ikiwamo kuwa na wahadhiri wasio na sifa. Kwa hali hiyo haishangazi kuona hivi sasa elimu ya juu ikinyooshewa kidole kwa kutoa wahitimu wenye uwezo mdogo.

Hatuna budi kukubali ukweli kuwa hili ni tatizo la kimfumo na kimasilahi, ambalo linahitaji uwekezaji mkubwa ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Ni kweli wasomi wenye sifa wanakimbia vyuo vikuu kwa sababu ya masilahi, lakini uko ukweli wa sababu ya kimfumo tuliojiwekea kwa muda mrefu kama nchi ambapo wahadhiri wakiwamo waliobobea wanahamishwa vyuoni na kupangiwa majukumu katika taasisi mbalimbali za umma.

Moja ya njia za kulitatua suala hili linalohatarisha mustakabali wa elimu ya juu nchini ni kuunganisha kuwaendeleza wahadhiri vyuoni na mipango mbalimbali ya maendeleo ya Taifa kama vile Dira ya Taifa ya 2025 na mingineyo.

Tunapojipanga kuelekea katika Tanzania ya uchumi wa kati unaohanikizwa na sera ya kuwa na viwanda, hatuwezi kufanikiwa kama tutalipa kisogo suala la kuwa na wataalamu mahiri na makini na hawa lazima wapitie kwenye mikono ya walimu wenye sifa vyuoni.

Serikali isiviache vyuo vikabaki mtoto yatima, ni wakati wa kuvitazama kwa jicho la huruma kwa kuviwezesha kirasilimali ili viweze kuendeleza wataalamu wake na hatimaye kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la uhaba wa wahadhiri wenye sifa.

Hata hivyo, Serikali isichague wala kupendelea vyuo vilivyo chini ya taasisi zake. Vyuo binafsi navyo vinapaswa kukumbukwa kwa kuwa navyo vina mchango mkubwa tu katika kuzalisha wataalamu wa Taifa letu.