http://www.swahilihub.com/image/view/-/4755832/medRes/2107395/-/6mpccm/-/mipango.jpg

 

Mikataba ya PPP yatikisa bungeni, wapinzani wahofia kuwakimbiza wawekezaji makini

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango  

Na Sharon Sauwa

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  12:53

Kwa Muhtasari

Migogoro ya miradi ya PPP itaamuliwa na vyombo vya ndani 

 

Dodoma. Serikali imewasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) wa mwaka 2018, sasa migogoro ya miradi ya PPP itaamuliwa na vyombo vya ndani na kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema jana akiwasilisha muswada huo bungeni kuwa muswada unapendekeza sheria kubainisha mikataba ya PPP na marekebisho yake ni sharti ihakikiwe na mwanasheria mkuu wa Serikali baada ya kukubaliwa na kamati ya uamuzi ya PPP.

Akielezea sababu za kufanyia marekebisho sheria hiyo, Dk Mpango alisema ni kuleta tija na ufanisi katika kutekeleza na kusimamia miradi ya PPP kwa kutatua baadhi ya changamoto.

Alizitaja miongoni mwa changamoto zitakazotatuliwa kuwa ni mlolongo mrefu wa michakato ya uidhinishaji miradi ya ubia ambao unaathiri kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa miradi ya PPP.

“Sheria ya bajeti kutotambua miradi ya PPP katika mchakato wa makadirio ya bajeti ya maendeleo hivyo kusababisha miradi hiyo kuzingatiwa kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya bajeti,” alisema waziri huyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene alisema baada ya majadiliano kuhusu usuluhishi na utatuzi wa migogoro inayotokana na miradi ya PPP, imekubaliana usuluhishi uwe na nyanja mbili. “Uwe kwa njia ya makubaliano yaani ‘negotiation’ na iwapo itaonekana kuna haja ya mgogoro kwenda kwenye mamlaka za usuluhishi na mahakama, basi zitakazotumika ni zilizopo nchini na kutumia sheria za Tanzania,” alisema Simbachawene.

Naye Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee akiwasilisha maoni ya kambi rasmi ya upinzani alisema kuweka kifungu kinachotaka migogoro inayotokana na miradi ya ubia kutatuliwa nchini, kitawafukuza wawekezaji makini wa nje ya nchi.