http://www.swahilihub.com/image/view/-/4339136/medRes/1906996/-/n9ma9w/-/odhiambo.jpg

 

Millie Grace Akoth Odhiambo: Alikosha sana kwa kutembea peku bungeni

Millie Grace Akoth Odhiambo Mabona

Mbunge wa Suba Kaskazini, Millie Grace Akoth Odhiambo Mabona alikosha sana kwa kutembea peku bungeni. Picha/HISANI  

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  08:10

Kwa Muhtasari

Mbunge wa Suba Kaskazini, Millie Grace Akoth Odhiambo Mabona alizaliwa mwaka wa 1966 huku Rais Uhuru Kenyatta akizaliwa mwaka wa 1961.

 

MBUNGE wa Suba Kaskazini, Millie Grace Akoth Odhiambo Mabona alizaliwa mwaka wa 1966 huku Rais Uhuru Kenyatta akizaliwa mwaka wa 1961.

Ndiye tu mwanasiasa wa kike hapa nchini ambaye amesikika hadharani akimpapura Rais Kenyatta ambapo Desemba 2016, aliangaziwa kwa waliomuona kama ni mtu wa kutumia lugha chafu kwa kiongozi wa nchi.

Ni tukio ambalo lilimwingiza katika utata mkuu na vyombo vya kiusalama ambapo taharuki aliyosambaziwa ilimwelekeza hadi mahakamani kuomba maagizo asikamatwe na pia akawa ameenda mafichoni.

Mwanamama huyu alikosha sana kwa kutembea peku bungeni - miguu tupu bila vyatu; akiwa amevibeba vyatu vyenyewe mkononi.

Hata hivyo, iliishia kuwa hakuna aliyekuwa na haja ya kumnasa au kumkamata lakini idara hizo za kiusalama huwa na mbinu zake za kukupa taharuki kuu.

Ni mfuasi sugu wa Raila Odinga na hakuna uaminifu mwingine yeye hukiri hadharani isipokuwa Odinga na vyama vyake vya kisiasa.

Elimu ya msingi aliifuata katika shuole ya msingi ya St Francis Rangala na kisha akajiunga na ile ya Limuru Girls kwa elimu ya sekondari.

Alijiunga na chuo kikuu cha Nairobi ambapo alifuatana na taaluma ya uwakili akizingatia masuala ya haki za kibinadamu.

Hatimaye alipaa angani akiabiri ndege kusaka elimu zaidi ya uwakili katika chuo cha New York

Ni mbunge wa awamu ya pili na nyingine moja akiwa mbunge maalum na kuifanya tajiriba yake bungeni kuwa miaka 11 sasa akielekea kuafikia miaka 15 kama mbunge.

Awali, alikuwa akijihusisha na masuala ya haki za kibinadamu na pia mara kwa mara kushiriki maandamano ya kuunga mkono upinzani kwa serikali mamlakani hasa ile ya Mzee Mwai Kibaki.

Baada ya kushinda mchujo wa ODM katika siasa za Aprili 2017, nyumba yake iliyoko katika kijiji cha Urianda iliteketezwa katika kisa ambapo alikitaja ni jaribio la kumuogofya na hata kumuua baada ya kuibuka na ushindi katika mchujo huo.

Alipoteza babake akiwa mdogo na akalewa na mamake katika familia ya watoto wanane.

Anasema hisia zake 'mbaya' kwa utawala wa Rais Kenyatta alizirithi kutoka kwa babake akiwa hai kwa kuwa “babangu alikuwa hasidi mkuu wa utawala wa Hayati Mzee Jomo Kenyatta akiwa Rais mwanzilishi wa taifa”.

Ameandika kitabu kuhusu changamoto zake za kutafuta kiti cha kisiasa katika eneo hilo la Luo Nyanza kikifahamika kama: Political Leadership Unpackaged: Lessons for Aspiring Women Leaders.

Kisa cha sarakasi kisiasa kilizuka bungeni mwaka wa 2016 wakati mrengo wa Jubilee ukisukuma sheria za kiusalama kupitishwa kwa hali na mali.

Anasema kuwa mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria alimtusi kwa maneno makali na akamgonga konde la ashakum si matusi - makalio, huku wengine wawili ambao hawataji wakijaribu kumvua nguo.

“Niliwahisi waking’ang’ana kunitoa chupi na niliwasaidia ambapo mimi niliiteremsha na nikawarushia,” akasema Bi Mabona.

Anasema kuwa yeye hana aibu na uchi wake na aliwasaidia kujianika uchi ili waelewe hilo haliwezi likatumiwa kama silaha ya kumuaibisha kisiasa au kijamii.

Ameolewa ndio, lakini anasema kuwa awali mchumba huyo wake walikuwa wakionana naye mara nne kwa mwaka lakini "siku hizi tunaonana mara nyingi".

Hivi majuzi alikuwa katika mitandao ya kijamii akisema kuwa kuna kijana rika ya mtoto wake ambaye anamsumbua kwa msingi wa kimahaba.

Alimsuta kwa msingi kuwa anafaa kuchukulia maisha yake kama mwanafunzi kwa uzito na pia asake huduma za utaalamu wa ushauri kutoka kwa aidha kiongozi wa dini au mwalimu wake mkuu.

Hana mtoto lakini anasema kuwa hilo halimsumbui kwa kuwa Mungu ndiye ajuaye sababu ya hali hiyo.