Mimba kwa wenye umri mdogo zisichekewe

Imepakiwa - Tuesday, April 9  2019 at  08:33

 

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amesema mwaka 2017 wasichana 71,076 wenye umri chini ya miaka 20 walipata ujauzito. Hali kadhalika 2018 wasichana 44,377 walio chini ya umri huo walipata ujauzito mkoani mwake.

Akizungumza mkoani humo juzi, Mwanri alisema takwimu hizo zinajumuisha wasichana waliopo na wasiokuwa shuleni.

Takwimu hizo zinasadifu na kauli iliyowahi kutolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustin Ndugulile kwamba wasichana 18,000 wenye umri wa chini ya miaka 18 mkoani humo pekee walipata mimba kati ya Januari hadi Machi mwaka jana.

Kwa mujibu wa Dk Ndugulile, ukiacha mkoa huo, kwa wastani kitaifa ni kuwa asilimia 27 ya wasichana kati ya miaka 15 na 19 walikuwa wamezaa au wana mimba.

Takwimu hizo zinatoa picha tofauti au kinzani ukilinganisha na juhudi zingine zinazochukuliwa na Serikali katika kuchochea maendeleo ya jamii kwenye nyanja mbalimbali hasa wakati huu nchi ikijielekeza katika uchumi wa viwanda na wa kati mwaka 2025.

Bila shaka juhudi zinazofanyika kuiondoa Tanzania katika umaskini mojawapo ya hatua zake ni kuwa na kizazi kilichopata elimu bora bila kuzingatia jinsia. Lakini hilo linaweza lisitimie kikamilifu kama maelfu ya wasichana wataendelea kupata ujauzito katika umri mdogo.

Madhara ya kubeba mimba katika umri mdogo mbali na kumnyima fursa ya elimu binti aliyebebeshwa ujauzito, pia humuweka hatarini kiafya kwa kuwa bado hajafikia umri mwafaka wa kubeba mimba.

Ndugulile alisema mimba za utotoni pia zimekuwa chanzo kikubwa cha ugonjwa wa fistula, na kuleta changamoto katika kukabiliana nao kwa kuwa watoto hao chini ya miaka 18 wanapata madhara zaidi.

Tunatambua kwamba ingawa kwa sasa mkoa uliotajwa ni Tabora, lakini tatizo hilo halipo Tabora pekee, bali katika mikoa mbalimbali ambako watoto wamekuwa wakibebeshwa mimba bila kujua na bila hiyari yao.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo tunadhani umuhimu wa haraka wa wadau wote ni kuamka na kuingilia kati suala hilo kabla halijaleta madhara makubwa zaidi.

Tunaposema wadau wanaotakiwa kuvalia njuga suala hili tunamaanisha Serikali na vyombo vyake, wazazi, walimu, asasi zisizo za kiserikali na vyombo vya habari.

Jukumu la kumlea, kumuongoza, kumlinda na kumwezesha kufikia malengo yake mtoto wa kike ni la kila mmoja kuanzia kwa familia na jamii inayojumuika naye katika maisha yake ya kila siku.

Hata hivyo, Serikali inapaswa kushika hatamu kuongoza safari ya kukabiliana na tatizo la mimba za utotoni kwa namna mbalimbali ikiwamo kuwabana wanaohusika wakiwamo wanaume wanaofanya nao mapenzi au wazazi wenye tamaa.

Tunafahamu kuwa katika baadhi ya matukio ya watoto wa kike kupata ujauzito watu wa karibu kama wazazi wamekuwa wakihusika kwa kuridhia kuwaoza mabinti zao kwa tamaa ya kupata fedha na mali.

Katika mazingira kama hayo Serikali iongoze kuwabana siyo wazazi pekee, bali hata walezi na wote wanaotambua mipango hiyo na wakati mwingine kukubali kushiriki ili kufanikisha mikakati hiyo.

Kama Taifa tunapaswa kuimba wimbo mmoja kuelekea kuwa na jamii iliyo huru na changamoto zinazoepukika kama ya mimba kwa wasichana ili hatimaye tuwakuze na kuwa na Taifa la kupigiwa mfano katika maendeleo. Ni vyema wanajamii wasikubali kuwa watu wanaochangia maovu kwa kufumbia macho vitendo vya wasichana kubebeshwa ujauzito katika umri mdogo, watoe taarifa kila wanapohisi harufu ya kutendeka jambo hilo ili kuiokoa jamii.