Mnaouza mafuta ‘kidebe’, jifunzeni kutoka Same

Mafuta ya petroli yakiwa kwenye chupa 

Imepakiwa - Tuesday, March 12  2019 at  15:56

 Moja ya matukio ya huzuni na kusikitisha yaliyotokea wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, wiki iliyopita, ni lile la moto lililosababisha vifo vya watu saba. Moto huo uliotokea katika Kijiji cha Marwa, Kata ya Ruvu, Jumatano iliyopita ulitokana na biashara ya petroli iliyokuwa ikifanyika nyumbani, na kwa kuwa haikuwa ikizingatia taratibu za usalama wakati muuzaji akimpimia bidhaa hiyo mteja wake karibu na jiko la mkaa, moto uliripuka na kusababisha vifo vya watu watano papo hapo.

Miongoni mwa waliofariki dunia wapo watoto wawili, muuzaji mwenyewe ambaye alikuwa ni muuguzi katika zahanati ya kijiji hicho na mteja wa mafuta hayo.

Huo si msiba wa kijiji cha Marwa pekee, bali Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa zima kwa kuwa tumepoteza nguvu kazi iliyokuwa ikihitajika kuanzia ngazi ya familia.

Wakati ajali hiyo ikiwa imepita na kila mmoja akiendelea na shughuli zake, ni lazima tujiulize kisha kuchukua hatua kukabiliana na matukio kama hayo yanayoweza kujitokeza siku za usoni.

Huko nyuma biashara ya mafuta hasa ya petroli na gesi ilikuwa ni vitu vyenye kuogopwa mno kutokana na hatari yake katika kusababisha moto. Ni mara chache ilihifadhiwa ndani na hata inapohifadhiwa tahadhari ilikuwa ikichukuliwa ikiwamo kupunguza watu wanaoingia kwenye nyumba husika hasa watoto.

Hivi sasa kila mmoja ni shahidi wa biashara ya petroli kwamba imekuwa ikifanywa kiholela, na kwa vijijini karibu kila kijiji utakutana na ama mbao au vichanja vyenye chupa zilizojazwa petroli kwa ajili ya biashara maarufu kama petroli ya kidebe.

Licha ya hatari yake, lakini biashara, utolewaji na uhifadhi holela wa petroli umeendelea kuonekana karibu kila kona ya nchi na athari zake ni kwa matukio kama hili lililotokea Same.

Kwa sasa ni muda mwafaka kwa mamlaka husika kulitazama jambo hili kwa kina zaidi kabla hayajatokea madhara mengine ili kuepusha hatari na athari zinazoweza kutokea.

Mamlaka husika ni lazima zichukue hatua kukabiliana na suala hilo kwani hata kama biashara hiyo ikiwa ni sehemu ya watu kujikwamua kiuchumi, lakini wanaoihitaji ni lazima washauriwe, kuelekezwa na wao kufuata hatua kwa hatua yale wanayopaswa kuyafanya ili kuepuka madhara.

Biashara ya petroli na gesi ina miongozo yake iliyowekwa mahsusi ili kukabiliana na hatari zake, na mara nyingi ni matukio ya moto, hivyo zifuatwe kikamilifu.

Viongozi wa vijiji au mitaa wawe jicho la kwanza katika kusimamia na kutazama usalama wa wale wanaofanya biashara hiyo ambao ni sehemu ya wale wanaowaongoza kwani endapo hatari yoyote itajitokeza athari zake huanzia katika kijiji au mtaa husika.

Mbali na hilo, kwa wananchi wenyewe nao wanapaswa kuchukua tahadhari wanapohifadhi mafuta ya petroli na mengine yaliyo hatari kwa usalama wa watu na mali.

Itashangaza kuona mtoto mchanga au hata wale waliofikisha miaka zaidi mitano walazwa katika chumba chenye petroli ambao kujinusuru endapo moto utalipuka katika tukio kama la Same itawawia vigumu kujiokoa.

Ulinzi wa usalama wako na mali unapaswa kuanza na wewe mwenyewe kabla ya kushikiwa kitabu chenye orodha ya sheria, taratibu na miongozo ya kukuweka salama dhidi ya jambo lolote. Tunawapa pole walioondokewa na wapendwa wao katika tukio la Same, lakini hilo linapaswa kuwa somo kwa wengine wanaendelea na biashara ya mafuta ya kidebe. Tunawasihi kuchukua tahadhari kwani inaweza kumtokea yeyote wakati wowote.