http://www.swahilihub.com/image/view/-/5021572/medRes/2278547/-/ogrrbo/-/chambuzi+pic.jpg

 

Mpangomiji Jiji la Mbeya uyakumbuke haya

Kaimu Mkurugenzi jiji la Mbeya Dkt. Samuel Lazaro 

Na  Lauden Mwambona

Imepakiwa - Tuesday, March 12  2019 at  16:12

 

 Hivi karibuni Jiji la Mbeya kupitia viongozi wake limeingia mkataba na kampuni iitwayo Urban Solution kutoka Dar es Salaam kutengeneza mpango wa mji mpya utakaosimamia shughuli zote za ujenzi na maendeleo ndani ya jiji kwa miaka 20 ijayo.

Mkurugenzi wa jiji hilo, James Kasusula alitia saini kwa niaba ya jiji wakati kiongozi wa Urban Solution, Willy Kitonka aliweka wino huku viongozi wengine akiwamo meya wa jiji, David Mwashilindi wakishuhudia.

Mwashilindi anasema kazi hiyo itafanyika kwa miezi 18 kuanzia sasa na itagharimu zaidi ya Sh900 milioni, kwa lengo la kuweka utaratibu utakaofuatwa katika shughuli za kuendeleza maeneo.

Naye Kasusura aliwaomba wananchi watoe ushirikiano kwa wataalamu hao ili kazi ikamilike kwa wakati na kwamba mpango huo utachangia kulibadili jiji kuwa la kisasa zaidi.

Anasema mpango huko unatarajiwa kupunguza changamoto nyingi zinazolikabili jiji la Mbeya lenye eneo la kilomita za mraba karibu 214.

Hatua hiyo inachukuliwa baada ya wakazi wengi wa Jiji la Mbeya kujenga nyumba bila kufuata mpango wowote ama kutoka kwa uongozi wa jiji au kufuata taratibu na maelekezo ya jiji hilo.

Kwa mujibu wa Mwashilindi, kwa mara ya mwisho, ‘master plan’ ilikuwapo katika miaka ya 1984 hadi 2005 lakini kuanzia 2006 hadi sasa, jiji halikuwa na kitu hicho, jambo ambalo limechangia kwa asilimia kubwa kusambaa kwa ujenzi holela.

Miongoni mwa maeneo ya makazi mapya yaliyoanzishwa bila kuwapo mipango miji bora ni pamoja na mitaa ya Ilemi, Iganzo, milima James, Sistila, Nsalaga Ikuti, Kalobe na Igawilo Juu.

Mitaa hiyo yote na mingine mingi haijapimwa, licha ya kujengwa nyumba nzuri na za kupendeza huku kukiwa na shida ya kupata maeneo ya wazi, kujenga shule na kukabiliwa na hali ngumu ya kupitisha miundombinu ya barabara, maji na hata umeme.

Kwa jumla ujenzi holela katika Jiji la Mbeya ni kama jadi, kwani licha ya maeneo hayo mapya, mitaa mingi ya zamani ilijengwa kiholela.

Miongoni mwa mitaa iliyojengwa ovyo ni pamoja na Mwanjelwa, Nonde, Airport ya zamani, Nzovwe Iyunga, Mama John na hata Iyunga.

Hivyo upo uwezekano pia kwamba kutokana na kukosekana kwa mpango miji, Jiji la Mbeya limeshindwa kusimamia ujenzi wa maghorofa katika eneo la Iwambi ambalo lilipimwa miaka ya hivi karibuni na kuwapo agizo hilo.

Halikadhalika upo uwezekano kwamba kukosekana kwa ‘master plan’ kumechangia kwa asilimia kubwa kuliingiza jiji kwenye mtego mkubwa kwa kupima viwanja katika eneo tepetepe ambalo ni chanzo kikuu cha mto unaotoka Mbeya kwenda Ziwa Rukwa.

Eneo hilo ni la Isyesye - viwanja vipya ambako walipima viwanja baada ya 2005, lakini baadhi ya maeneo kimsingi hayakustahili kupimwa viwanja.

Watu waliojenga maeneo hayo kwa sasa wanakumbwa na mafuriko ya maji kutokana na ukweli kwamba bonde hilo ni tepetepe na linakusanya maji na hatimaye maji hayo yanaelekea ziwani kupitia mitaa ya Mama John, Makunguru, Ilolo, sabasaba, Mabatini, Kalobe hadi Mto Songwe kabla ya kuingia Rukwa.

Hali kadhalika ukosefu wa ‘master plan’ katika jiji hilo umeathiri pia umuhimu wa kusimamia kukosekana maeneo ya makaburi hususan huko Iwambi, Iyela na Mlima James.

Katika maeneo hayo makaburi yanachimbwa bila kufuata mpangalio wowote na kusababisha kwa barabara na hatimaye kusababisha usumbufu ambapo wanaozika sasa wanalazimika kubeba jeneza huku wakiruka rukaruka kwenye makaburi kwa muda mrefu.

Wapo waombolezaji wengine wamepata majeraha kwa kudondoka na majeneza maeneo hayo kutokana na kukosa njia sahihi ya kupita.

Bila shaka ni wakati mwafaka kwa mpango mji mpya kutenga eneo jipya la kuzika ambalo marehemu watazikwa kwa mistari, huku likiwa na barabara zinazogawa makaburi kwa idadi itakayokubalika

Eneo hilo halina budi pia kuwa na jengo la kupumzikia waombolezaji wanapokumbwa na mvua ama jua kali tofauti na hivi sasa ambapo hawana msaada wowote wanapokumbwa na kadhia hizo.

Tunaamini pia kwamba mpango huu mpya utazuia ujenzi kwenye makorongo na vilima vikali ambao kwa sasa umeshamiri na unazidi kushika kasi.

Lauden Mwambona ni mdau wa maendeleo anayeishi mkoani Mbeya anapatikana kwa simu namba 076738897