Msako wa vyeti feki usiwe na upendeleo

Na MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, April 19  2017 at  15:04

Kwa Mukhtasari

RAIS John Magufuli wakati akizindua majengo mapya kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Jumamosi iliyopita alisema kuna watumishi wapatao  elfu tisa  serikalini wenye vyeti feki.

 

Orodha hiyo hajawasilishwa rasmi mezani kwake  ingawa imesemekana baada ya kazi ya miezi kadhaa ya kuhakiki wafanyakazi serikalini, utendaji kazi wao ikilinganishwa na elimu yao, majina yao katika vyeti vya sekondari na vyuo.

Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani  iliamua kuhakiki vyeti vya watumishi wake ili kujiridhisha  na taaluma zao  maana katika miaka ya hivi karibuni  wako waliofeli katika ngazi fulani ya elimu lakini wanakuja  kuonekana kuwa na vyeti vya elimu ambayo hawakuifanyia kazi.

Pia miaka ya hivi karibuni baadhi ya watu wamethubutu hata kughushi vyeti vya shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na ya uzamivu ndio maana wanaitwa madaktari fulani wakati hawana kiwango cha elimu hiyo.

Hivyo tunapongeza juhudi za Rais Magufuli kupambana na ufisadi wa elimu  na tunaamini atadhibiti sawa na alivyoshughulikia sakata la watumishi hewa waliobainika kufikia 50,000.

Mpango wa kuhakiki vyeti kwa watumishi wa umma ni mzuri kwa kuwa unalenga kuondoa wale wasio na elimu katika kuwahudumia wananchi.

Wako anaojenga majengo bila kufuata kanuni na taratibu  za ujenzi kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha na hivyo kusababisha baadhi ya majengo hayo kuanguka.

Tumeshuhudia pia maeneo kama hospitalini watu  wasio na sifa wamediriki kujiwekea ofisi na kutoa huduma kwa muda mrefu bila hata ya kujulikana.

Kwa hiyo mpango huo itasaiidia kurekebisha utumishi katika sekta ya umma. Tunaamini pia uhakiki huu utasaidia kupata ukweli na kuhitimisha mjadala mrefu kuhusu wateule wa Rais hasa mkuu wa mkoa mmoja.

Inadaiwa kuwa mteule huyu alifeli elimu ya sekondari lakini anaonekana na jina  jingine ambalo  licha ya kelele za kumtaka aeleze kiwango cha elimu yake ili kuwanyamazisha wapinzani wake na hadi sasa yuko kimya.

Wako waliokwenda hadi kijijini kwake na baadhi ya masanii wametunga nyimbo kumdhihaki. Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  wamezungunzia elimu ya mteule huyo wakitaka Rais atengue uteuzi wake  huku Meya wa Ubungo Boniface Jacob akiliwasilisha  suala hilo mbele ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kwa hiyo tunatarajia hiyo itahusisha suala hilo na kumpa Rais fursa ya kufanya uamuzi.

Tunaamini kuwa mteule huyo ni mmoja miongoni mwa watu wengi walio katika ripoti hiyo kwani Serikali ya Awamu ya Tano imepania kusafisha utumishi wa umma  na kuboresha utendaji kazi bila ya kuonea wala kupendelea kada fulani au kundi la watu fulani.