http://www.swahilihub.com/image/view/-/4843896/medRes/2165104/-/2v192q/-/patnk.jpg

 

Msomi India atahadharisha ujio wa wawekezaji

Profesa Prabhat Patnik  

Na Cledo Michael, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  11:42

Kwa Muhtasari

Kuwapo kwa sera rafiki za kuwalinda wakulima wadogo

 

cmichael@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mtaalamu wa masuala ya siasa kutoka India, Profesa Prabhat Patnik ameishauri Tanzania kuchagua mfumo utakaolinda maslahi ya wakulima wadogo ili wasipotezwe na ujio wa kampuni kubwa zinazowekeza nchini.

Licha ya kuangalia mbadala wa kimfumo, ameshauri kuwapo kwa sera rafiki za kuwalinda wakulima wadogo kwa kuhakikisha wanakuwa na ardhi na mbegu zisizoathiri kilimo.

Akihutubia mhadhara wa tano wa Kavazi la Mwalimu Nyerere jana, Profesa Patnik aligusia mambo mbalimbali yanayodhoofisha maendeleo ya nchi za Afrika ikiwamo mifumo isiyo rafiki kwa wakulima wadogo.

“Ujio wa ukoloni mamboleo umeibua matatizo mengi kwa wakulima wadogo na kuharibu uwezo wa taasisi za utafiti na kuwalazimisha kutumia mbegu za kisasa zisizo na tija,” alisema.

Naye mkurugenzi wa mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (Mviwata), Steven Ruvuga aliunga mkono hoja hizo akisema moja ya misingi ya Mwalimu Julius Nyerere ni kuhakikisha wakulima wananufaika na ardhi kwa maendeleo yao.

Awali, mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu alisema wameendelea kuwasimamia wakulima kwa kuwapa njia bora za kilimo na ushauri wa pembejeo.