Muda mifuko ya plastiki unazidi kwenda

Imepakiwa - Tuesday, May 14  2019 at  11:26

 

Kuanzia Juni mosi, matumizi ya mifuko ya plastiki yatakuwa haramu baada ya Serikali kupiga marufuku kutokana na athari zake katika mazingira.

Serikali imechukua hatua hiyo baada ya majadiliano na wadau, hasa wazalishaji ambao kwa kiasi kikubwa wataathirika kibiashara kutokana na uwekezaji walioufanya katika teknolojia viwandani.

Pia mawakala wao watakuwa katika hali ngumu kutokana na ukweli kwamba watakuwa hawana uhakika wa kumaliza shehena waliyonayo kabla ya tarehe hiyo kufika.

Hata hivyo, tatizo kubwa zaidi litakuwa kwa watumiaji, na hasa wafanyabiashara ndogondogo ambao wamekuwa wakitumia kuwekea bidhaa wanazouza, ikiwa ni kama huduma kwa wateja.

Ukiacha wazalishaji, wadau wengine wa bidhaa hizo sasa wanasubiri kitakachotokea baada ya tarehe hiyo ya marufuku kufika. Baadhi wanadhani kuwa Serikali italeta bidhaa nyingine kuchukua nafasi ya mifuko ya plastiki na wengine wanadhani marufuku hiyo haiwezekani na hivyo ni lazima Serikali italegeza msimamo wake kwa kuongeza muda zaidi kwa wadau.

Kilicho dhahiri ni kwamba ni lazima matumizi ya bidhaa hiyo yapigwe marufuku kama kweli tunataka nchi yetu iwe sehemu bora ya kuishi sisi binadamu na viumbe wengine.

Maisha yetu yanategemea ardhi iliyo bora inayoweza kuzalisha mazao bora, isiyoharibiwa na plastiki ambazo ni kama zinajenga sehemu yake katika ardhi. Maisha ya binadamu pia yanategemea wanyama inaowatumia kwa chakula na ambao wanaathirika na ongezeko la plastiki katika maisha yao ya kila siku.

Inapotokea wanakula chakula kilichochanganyika na plastiki, maisha yao yanakuwa hatarini.

Hali kadhalika viumbe wa majini wanahitaji mazingira bora yatakayowawezesha kuishi bila tabu na hivyo kuweza kutegemeana na binadamu. Lakini plastiki zinaharibu ubora wa mazingira yao na kuweka maisha yao hatarini.

Plastiki inagusa karibu katika kila nyanja ya maisha ya binadamu na viumbe vingine anavyotegemeana navyo kwa maisha bora. Kwa kuwa plastiki haichangii kuboresha maisha kila nyanja inapoingia, ni lazima matumizi yake yadhibitiwe kama si kuondokana nayo kabisa.

Kwa hiyo, Serikali ilikuwa sahihi kabisa kupiga marufuku utengenezaji na matumizi ya mifuko ya plastiki, ikiwa ni moja ya hatua ya kulinda mazingira yasiharibiwe na kuwa hatarishi kwa viumbe wake.

Lakini kipindi kilichosalia kabla ya amri hiyo kuanza kutekelezwa kifupi na hatuoni juhudi kubwa za kutoa elimu kwa wadau ili wajiandae kwa maisha mapya bila ya mifuko ya plastiki.

Hata kasi ya wabunifu kugundua mbadala wa plastiki si kubwa ikilinganishwa na matumizi makubwa ya plastiki katika maisha ya kila siku. Maana yake ni kwamba haitakuwa rahisi plastiki kupotea ghafla Juni mosi, na kwa sababu haitawezekana kupotea ghafla kuna watakaoumia kwa kulipa faini kubwa au kupambana na vyombo vya dola vitakavyokuwa vinasimamia sheria.

Haitakuwa busara kufika huko. Hivyo ni jambo muhimu sasa kwa wahusika kuongeza juhudi kutafuta bidhaa mbadala itakayoweza kuziba kwa haraka pengo litakalotokana na marufuku dhidi ya mifuko ya plastiki.

Tunatarajia Serikali haitarudi nyuma katika uamuzi wake, lakini itafanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata suluhisho mapema ili kuepuka kuvunja agizo hilo kwa kulazimika.