http://www.swahilihub.com/image/view/-/4758106/medRes/2108991/-/our4vbz/-/seda.jpg

 

Mugumo waanguka na kunyanyuka tena kijijini Yamumbi

Yamumbi

Wakazi wa Kapseret kaunti ya Uasin Gishu wamekuwa wakifurika katika kijiji cha Yamumbi katika eneobunge hilo kutazama mti wa mugumo unaodaiwa 'kunyanyuka' baada ya kuanguka. Picha/GERALD BWISA 

Na DENNIS LUBANGA na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, September 13  2018 at  17:52

Kwa Muhtasari

Wakazi wa Kapseret kaunti ya Uasin Gishu wamekuwa wakifurika katika kijiji cha Yamumbi katika eneobunge hilo kutazama mti wa mugumo unaodaiwa 'kunyanyuka' baada ya kuanguka.

 

WAKAZI wa Kapseret kaunti ya Uasin Gishu wamekuwa wakifurika katika kijiji cha Yamumbi katika eneobunge hilo kutazama mti wa mugumo unaodaiwa 'kunyanyuka' baada ya kuanguka.

Makundi ya wakazi wamekuwa wamekuwa wakielekea mahala hapo kushuhudia tukio hilo ambalo limekuwa likizungumziwa kwa wingi na wakazi.

Kijiji cha Yamumbi kilichoko viungani mwa mji wa Eldoret huwa ni mahala tulivu lakini kwa siku mbili zilizopita kimekuwa kikitembelewa na wageni wenye hamu ya kuona na kuuguza mtu huo.

Baadhi yao wanataka eneo hilo kutawazwa kama eneo takatifu.

“Mtoto wangu kiume alikuwa akielekea shuleni ndipo akashuhudia tukio hilo la kiajabu. Aliona mti wa Mugumo ukianguka na kuinuka tena lakini aliogopa kurejea nyumba kuripoti alichoona kwa sababu angechelewa shuleni,” akasema Susan Lelei, mamake Fabian Kiptanui.

Bi Mary Chebet mkazi wa eneo hilo alisema hakushtuka kwa sababu ya tukio hilo.

“Tumefurahi kufuatia kile kimetendeka kwa sababu ni kazi ya Mungu. Hili ni tukio ambalo linaweza kutokea mahala popote na hivyo sio sababu ya watu kushtuka,” Bi Chebet akasema.

Swahili Hub ilipofika eneo hilo, Fabian ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya msingi ya Gitwe alisema aliona mti huo ukiinuka juu alipokuwa akielekea shuleni.

“Nilikuwa nikielekea shuleni mwendo wa asubuhi. Nilipokaribia mto ambako Mugumo ulikuwa, niliona ukianguka na kisha kunyanyuka . Lakini sikutaka kwenda nyumbani kuripoti kwa sababu sikutaka kuchelewa shuleni,” Fabian akasema mbele ya mamake.

Maelezo

Huku aina mbalimbali ya maelezo yakitolewa kuhusu tukio hilo, baadhi ya wakazi wanawataka wazee kulivalia njuga suala hilo na kutoa maelezo kulihusu.

“Wazee kutoka jamii za Wakikuyu na Wakalenjin wanafaa kufanya mkutano wa dharura na kuvumbua sababu ya kutokea kwa kisa hiki,” akasema Paul Kiplimo, mkazi.

Wazee kutoka jamii ya Wakikuyu wakiongozwa na wasemaji wao Kamunu Kabari na George Kinyanjui walisema kuwa wanafahamu kuhusu kisa hicho na kwamba watakutana na wenzao kutoka jamii ya Wakalenjin ili kujadili suala hilo.

“Ninaweza kuthibitisha kwamba tunafahamu kuhusu kisa hiki na tunajaribu kujadiliana na wenzatu kutoka jamii ya Kalenjin ili tuketi chini ya kujadili suala hili kwa sababu tukio kama hilo halijawahi kushuhudiwa hapa,” akasema Mzee Kamunu.