http://www.swahilihub.com/image/view/-/4564904/medRes/455907/-/firgegz/-/MutulaKCPE.jpg

 

Marehemu Mutula Kilonzo: Alipenda sana wanyamapori

Mutula Kilonzo

Marehemu Mutula Kilonzo. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  14:33

Kwa Muhtasari

Mutula Kilonzo alizaliwa Julai 2, 1948, katika familia ya Mzee Wilson Kilonzo Musembi na Mama Rhoda Koki Kilonzo katika kijiji cha Mbooni.

 

MAREHEMU Wakili Mutula Kilonzo alikuwa akimpa mawaidha Rais wa pili wa Kenya huru, Daniel Arap Moi.

Kilonzo alizaliwa Julai 2, 1948, katika familia ya Mzee Wilson Kilonzo Musembi na Mama Rhoda Koki Kilonzo katika kijiji cha Mbooni.

Kuna wakati ambapo bwanyenye aliyefanikiwa kutumia ulaghai alimpokonya babake mzazi Mutula shamba lake na ndipo hamasa ya kuwa wakili ikamwingia.

Akiwa na umri wa miaka 12 pekee, alitoka shuleni na kuwapata wazazi wake wamesononeka wasijue la kufanya kufuatia amri ya kwamba waondoke kutoka shamba hilo na ndipo papo hapo ‘pepo’ wa kuwa wakili akampanda.

Mutula alitia bidii katika masomo na hatimaye akahitimu kuwa wakili aliyezindulia huduma yake Jijini Nairobi katika jengo lililopo karibu na bustani ya Jevanjee.

Katika jengo hilo linalofahamika kama Kirima, kukazinduliwa kampuni ya Kilonzo and Company Advocates mwaka wa 1975, na ikajengwa hadi kuwa miongoni mwa maarufu katika usajali wa huduma za uwakili nchini.

Mashine ya kupiga chapa

Babake mzazi ndiye alimnunulia meza na kiti huku naye Mutula akijinunulia taipureta kwa Sh250.

Kesi zake zikawa ni za kutetea waadhiliwa wa utapeli wa mashamba na akawa anashinda kesi hizo kutokana na zile hisia za kulipiza kisasi ulaghai uliotekelezewa babake.

Kutokana na pato lake la ushindi wa kesi hizo, alijinunulia gari na akaanza kujinunulia mashamba, likiwemo lile babake alikuwa ametapeliwa.

Akiaga dunia, tayari alikuwa amejinunulia mashamba katika kila pembe ya Kenya na katika shamba moja, akaweka mbuga yake ya wanyama ya kibinafsi, akifuga simba.

Alifanikiwa kujipa kuridhika kwa nafsi yake alipohakikisha kuwa nyanyake, babuye, babake na pia mamake walizikwa katika lile shamba ambalo walilia kwa mahangaiko ya kupokonywa kwa kuwa aliishia kulinunua.

Mwaka wa 1969 alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam na akapita kwa gredi za juu zaidi katika mtihani wao na safari yake ya uwakili ikaanza.

Katika kila mtihani wake wa kisheria, alikuwa akiibuka wa kwanza na akafanikiwa kujipa hadhi katika soko la kutoa huduma, wakati huo safu hiyo ikitawaliwa na Wazungu na Wahindi.

Jaji Philip Waki ni wa ukoo wa Mutula Kilonzo na kwa kuwa walifuzu pamoja kuwa mawakili, wakajipa ratiba ya kuwa matajiri kupitia huduma za uhakika.

Waki akaamua ratiba yake ni kuajiriwa, Mutula akaamua ni kuzindua kampuni yake ya uwakili.

Aliponunua gari lake la kwanza, Mutula aliliacha katika duka la DT Dobie kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kuliendesha na ilibidi kwanza akasake uwezo huo ili aliendee.

Siku hizo, hakuna muuzaji gari ambaye angekubali uchukue lile umenunua kabla ya umwonyeshe leseni yako ya uendeshaji magari na kisha uliondoe dukani wewe mwenyewe ukiliendesha.

Katika huduma yake ya mwaka mmoja, Mutula alikuwa ameunda milioni yake ya kwanza na kuendelea mbele, ikawa habari ndiyo hiyo amejipa ukwasi kupindukia na hayo yakazidishwa mwaka wa 1980 aliposajiliwa rasmi kuwa wakili wa Moi.

Amehudumu kisiasa nchini kama mbunge na pia waziri, cheo chake mwishoni akielekea kwa mauti akiwa ni Seneta wa Makueni ambapo akiwa mwandani wa Kalonzo Musyoka kisiasa, wadhifa wake ulirithiwa na mwanaye, Mutula Kilonzo Junior.

Mutula Kilonzo aliaga dunia Aprili 27, 2013, katika mbuga yake ya wanyama ya Maanzoni; kifo ambacho hadi leo hii huwa ni gumzo mtaani kwa kuwa kiini chake bado hakijafichuliwa.