Mwamba wa Kaskazini umetuachia ‘madini’ kwenye kitabu chako

Na Folrence Majani

Imepakiwa - Friday, May 10  2019 at  13:31

 

Tanzania imepoteza dhahabu, mwamba na nguzo. Buriani
Reginald Mengi, kimsingi wewe ulikuwa ni nguzo
iliyosimama imara na vyema katika kila sekta. Tangu
Mengi alipofariki dunia Mei 2 huko nchi za Falme za
Kiarabu, jijini Dubai, kila mmoja ameyakumbuka
aliyofanya wakati wa uhai wake.
Kwa mazuri aliyoyafanya Mengi, kama waandishi
wangeweza kuyakusanya na kuyachapisha basi huenda
kila gazeti lingejaza kurasa zake zote.
Pamoja na kuacha alama zisizofutika katika maisha ya
watu, kuna kitu cha muhimu na kinachodumu zaidi
ambacho tajiri huyu ametuachia.
Nacho ni kitabu chake cha; ‘I can, I must, I will’ kwa
lugha ya Kiswahili: ‘‘Ninaweza, Lazima nifanye,
Nitafanikisha’ Ilikuwa ni Julai 2, 2018 wakati Mengi
alipozindua kitabu chenye historia ya maisha yake na
safari yake ya kimaendeleo.
Nimekisoma kitabu chake mara tu baada ya kuzinduliwa
Julai mwaka jana. Jambo la kwanza ni kichwa cha habari

cha kitabu hicho ambacho mara moja kinakupa
mwongozo na matumaini, ‘Ninaweza, Lazima nifanye,
Nitafanikisha’
Mengi mwenyewe alisema kuna maana kubwa katika jina
la kitabu hicho, ambayo ni kuwa na moyo wa uthubutu,
kupiga moyo konde pindi unapoianza safari na pia
kusimamia yale matarajio yako hadi uyakamilishe.
Katika kitabu kile, ameonyesha namna alivyoiona ndoto
yake, kupata uthubutu wa kuifanikisha ndoto hiyo na
kisha kusimamia ndoto hiyo.
Mengi mara kadhaa amekuwa akisema kuwa;
“Nimezaliwa katika umaskini wa kutupwa, lakini jambo
hilo hata siku moja halikunikatisha tamaa.” Katika kitabu
hicho, anasema alianzisha Kalamu Company Limited,
wakati bado akiwa mwajiriwa wa C & L Expatriates
Company.
Alikutana na vikwazo vingi, lakini kilichomfanya asirudi
nyuma ni ile dhana aliyojijengea ya: “Ninaweza, Lazima
nifanye, Nitafanikisha”
Baada ya kampuni ya Kalamu kuendelea vyema, aliacha
kazi ya kuajiriwa na kubaki akiisimamia kampuni yake.
Anaeleza kuwa inahitaji uthubutu wa hali ya juu, kuacha
kazi na kusimamia biashara yako.

Madini mengine ametuachia Mengi ni pale aliposema
katika kitabu chake kuwa; “Ninaamini biashara siyo kwa
ajili tu ya kupata faida tu bali pia kwa ajili ya majukumu
ya kijamii kama vile ujasiriamali wa kijamii.” Alitoa
mfano namna alivyotembelea Kijiji cha Mbokomu Korini.
Kilikuwa na kikundi cha wanawake waliokuwa na miradi
yao binafsi ya kiuchumi kwa ajili ya kujiendeleza.
Alipotembelea kikundi hiki aliwasaidia katika mradi wao
wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Msaada huo
ulitolewa kwa kuwanunulia ng’ombe wa maziwa, vifaa
pamoja na gharama za kujifunza ufugaji wa ng’ombe.
Anasema msaada ulikuwa ni mdogo lakini matokeo
yalikuwa makubwa. Wanawake hao waliweza kujenga
nyumba zao wenyewe, kusomesha watoto na kuboresha
maisha yao kwa ujumla.
“Ujasiriamali wa kijamii na kusaidia miradi ya kukuza na
kuiendeleza jamii ndivyo vinatambulisha maisha yake,”
anasema Mengi. Kingine cha kujifunza ambacho
ameandika kwenye kitabu chake ni namna alivyochagua
watu wa kufanya nao kazi.
Anasema anaamini licha ya kipaji na uwezo kuwa vya
muhimu katika kazi lakini uaminifu, kujituma na kujitoa
ni muhimu zaidi kwake.
“Naamini uwezo mkubwa unaweza
kuendelezwa/kujengwa lakini huwezi kujenga uaminifu

na kujitoa sana kwa mtu,” anasema Mengi ambaye
amewataja Zoeb Hassuji wa Bonite Bottlers Limited na
Joyce Mhaville wa ITV na Radio One kama wakurugenzi
wake bora zaidi wanaofanya vizuri na wenye sifa hizo.
Urithi mwingine aliotuachia kupitia kitabu hiki ni kutoa
nafasi ya kusikia nini wengine wanasema. Anasema
inamaanisha kusikiliza wateja au watu unaofanya nao
kazi au wakati mwingine hata washindani wako wa
kibiashara ni njia bora sana ya kufanikiwa.
Leo Mengi hayupo duniani, lakini kupitia kitabu hiki,
vijana wengi zaidi wanaweza kujifunza na kuwa na
uthubutu, kujiamini, upendo na ustahamilivu kama
aliokuwa nao.
Kubwa kuliko yote ambalo linawafanya wengi wamlilie
Mengi, ni upendo wake kwa jamii. Atakumbukwa kwa
upendo wake kwa walemavu na wasiojiweza.
Pia, kwa Watanzania walio na nafasi, waandike historia
zao kitaaluma au za maisha ili kuwahamasisha wengine.
Tuendelee kuzienzi moja ya kauli zake za mwisho
aliposema: “ Naomba nichukue fursa hii kuwaomba
Watanzania wenzangu kuufanya mwaka 2019 kuwa
mwaka wa maridhiano na kusameheana. Chuki ni mzigo
mzito mno kuubeba mioyoni mwetu, njia pekee ya
kusonga mbele ni kusameheana na kudumisha upendo.”