Mwarobaini kuharakisha afya kwa wote huu hapa

Na  Imeandaliwa na Herieth Makwetta, aliyekuwa Kampala Uganda

Imepakiwa - Monday, March 25  2019 at  11:44

Kwa Muhtasari

Wataalamu wakutana Liliana namna sekta za umma na binafsi zinavyoweza kushirikiana ili kurahisisha huduma

 

Kampala, Uganda. Nchi za Afrika Mashariki zimeshauriwa kuongeza kasi katika utekelezaji wa mchakato wa huduma za afya kwa wote bila vikwazo kiuchumi yaani ‘Universal Health Coverage’, na zimehimizwa kuungana kati ya sekta za umma na binafsi.

Pia zimetakiwa kuhakikisha zinaweka mfumo maalum wa kutoa mafunzo kwa watoa huduma ngazi za chini, ili kubaini katika hatua za awali wanaougua Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) na kuwapa tiba za mapema kabla ugonjwa haujafika hatua mbaya hasa magonjwa ya saratani na shinikizo la damu.

Hayo yameelezwa na wadau mbalimbali wa masuala ya afya jijini Kampala walipokutana katika kongamano lililojadili afya kwa wote lililojikita zaidi kuzungumzia magonjwa yasiyoambukiza.

Katika mambo yaliyoibua mjadala zaidi katika kongamano hilo ni pamoja na kuendeleza teknolojia ya kidijitali katika utoaji wa huduma za afya zenye viwango.

Sauti za wagonjwa na asasi za kiraia katika haki za kupata huduma bora, pamoja na kuchambua vitu muhimu, matatizo na changamoto katika upatikanaji wa fedha kuchangia huduma za afya kwa wasiojiweza.

Mjadala uliochukua nafasi kubwa zaidi ilikuwa ni kuhusu ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma katika kutoa huduma za afya kuelekea utekelezaji wa Huduma za Afya kwa Wote (UHC).

Katika hilo, mchokoza mada wa awali mkuu wa kampuni ya utafiti wa madawa ya Novartis, Dk Harald Nusser alisema ni wakati sasa sekta binafsi zikaamua kuungana na za umma katika kuimarisha huduma za matibabu ili kwenda hatua zaidi.

“Hakuna kitakachofanikiwa kama kila mmoja atasimama mwenyewe, ili kusonga mbele sekta za umma zishirikiane na binafsi katika kuchambua vitu muhimu kwenye utekelezaji huo ili angalau makundi ya wasio katika mfumo rasmi wa ajira na wale wasiojiweza wafikiwe tusimwache yeyote nyuma,” alisema Dk Nusser.

Katika mjadala huo elimu kwa watoa huduma za afya ilielezwa kuwa utakuwa mwarobaini wa ugunduzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza, hivyo ilishauriwa kufundisha wataalamu katika ngazi za chini za utoaji huduma za afya.

Mkurugenzi mtendaji mkuu wa Amref Health Africa, Dk Githinji Gitahi alisema kwa nchi nyingi wastani wa mapato yatokanayo na kodi katika pato la taifa (GDP) ni kati ya asilimia 17 hadi 18 ambayo ni ndogo sana.

“Kusimamia huduma kwa wote ambao huwezi kuwatoza kodi ni vigumu lakini hili linaweza kuwezeshwa kupitia bima, inasaidia watu kujinasua katika gharama kubwa za matibabu.

Kama Uganda imekuwa ikifanya hivyo kupitia mfumo wake wa bima ya afya,” alisema Dk Gitahi na kuongeza; “Kwa Afrika asilimia 80 ya watu wake wako katika sekta isiyo rasmi, lakini haimaanishi kuwa ni masikini. Tunatumai wale walioko katika sekta rasmi kama kigezo cha watu wanaoweza kupata bima kwa sababu ni wazi kuwatoza kodi watu wasiokuwa kwenye sekta rasmi ni vigumu.

“Sasa hapa tunaweza kuangalia tunavyoweza kuwapata hawa wanaoendesha biashara au shughuli ndogo ndogo, kama kuuza matunda, kusafisha viatu, shughuli za kilimo kwa kuangalia tunavyoweza kuwatoza kodi kupitia huduma ya bima yao ya afya, ikiwa ni sehemu ya huduma za jamii.”

Dk Gitahi alisema ni wakati muafaka sasa kila nchi kuamua kuwa afya kwa wote si ya kuchagua bali ni lazima na haki.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Uganda, Dk Diana Atwine Kanzira alisema wazalishaji pia wanatakiwa kuhakikisha wanawekeza kuwezesha bidhaa zao kuwa sehemu muhimu ya ushirikishwaji katika hilo.

“Suala la pili kama taifa tunahakikisha tunaimarisha mamlaka ya dawa ya taifa ili kuongeza uwezo wa ufuatiliaji na kuhakikisha wasiotekeleza wajibu wao katika uzalishaji dawa wanawajibishwa,” alisema Dk Kanzira.

Mjadala uliohusu muundo wa usambazaji na manunuzi yatakayosababisha upatikanaji wa dawa zenye viwango bora na kwa bei rahisi, ulisimamiwa na mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu na mkurugenzi mtendaji mkuu kutoka MedSource, Dk Peter Kamunyo.

Akizungumzia hali ilivyo Tanzania, Bwanakunu alisema kwa kawaida dawa lazima ziwe zimesajiliwa na TFDA hivyo dawa zote zinazonunuliwa na Serikali ya Tanzania zina ubora.